Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP26 unafunga pazia huko Glasgow Scotland ambapo mwanaharakati wa Mazingira Dkt. Sixbert Mwanga kutoka nchini Tanzania anasema Afrika pamoja na kuwa na kauli moja lakini haijafanikiwa kwenye mkutano huo.
Dkt. Mwanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika la mtandao wa Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania – CANTz amesema hayo alipohojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, UNNEws kando mwa mkutano huo uliofanyika baada ya miaka 2 kutokana na kuahirishwa mwaka jana sababu ya janga la Corona au COVID-19.
Amesema mkutano umefanyika wakati nchi nyingi duniani zikiwa zimeathirika zaidi na madhara y mabadiliko ya tabianchi hivyo ilitegemewa kuwe na matokeo mengi chanya kitu ambacho hakijatokea.
“Tumekutana muda huu ambapo ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi ikionesha kwamba bara la Afrika litaendelea kuathirika na mafuriko na vitu mbalimbali hasa ukame kwa hiyo ni mkutano ambao ni wa tofauti kwasababu tunaangalia ni kwa jinsi gani tunaweza kupata rasilimali fedha”
Dkt Sixbert anasema Afrika ilienda mkutanoni hapo ikiwa na ajenda zake kamili “Ajenda zetu zilikuwa zipo dhahiri, tulikuwa tunahitaji rasilimali fedha na uwezeshaji wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwepo kwa mifumo ya usaidizi katika teknolojia lakini pia kujengewa uwezo, lakini fedha ndio kitu muhimu sio ziende kupunguza hewa ukaa pekee bali kusaidia uwezo wa kustahilisha mabadiliko ya tabianchi.”
Vijana wameeleza kutoridhishwa na ahadi tupu zinazotolewa na viongozi pamoja na kueleza namna ambavyo hawajashirikishwa katika masuala ya tabianchi suala ambalo Dkt.Mwanga anasema ni muhimu kuhakikisha wanajumuishwa katika miradi.
Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP27 unatarajiwa kufanyika mwakani 2022 nchink Misri barani Afrika na Dkt. Sixbert Mwanga anasema ‘mwakani tutakuwa na kazi kubwa kuhakikisha fedha zinapatikana’’.
Pia amesema ni muhimu nchi za Afrika zikiwa zinaondoka katika mkutano huu kuzingatia kuwa zina jukumu kubwa la kushuhhulikia madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kushirikisha vijana, wanawake asasi za kiraia na serikali kwa ujumla.
Mkutano wa COP26 ulianza tarehe 31 Oktoba na kukamilika leo 12 Novemba 13, 2021.