Ahadi ni hewa iwapo miradi ya makaa ya mawe na mafuta ya kisukuku inaendelea kupatiwa fedha- Guterres

11 Novemba 2021

Mkutano wa COP26 ukifikia ukingoni huko Glasgow, Scotland, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amezisihi serikali zioneshe hatua nyingi zaidi za kukabili, kuhimili na kufadhili miradi ya tabianchi kwa njia bora zaidi iwapo haziwezi kufikia kiwango cha chini zaidi kilichowekwa.

Guterres amesema hayo leo akihutubia mkutano huo huko Glasgow wakati huu ambapo uchambuzi wa mashirika ya mazingira ya Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa ahadi za kitaifa za miradi ya tabianchi haziwezi kuzuia joto halivuki nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwaka 2030.

“Tunafahamu tunachopaswa kufanya kufikia kiwango hicho, lakini NDCs hata kama zitatekelezwa kwa viwango vya sasa haziwezi kufanya hivyo. Joto litaongezeka ifikapo mwaka 2030. Bado tuko kwenye mwelekeo wa kuwa na joto katika nyuzijoto 2 kipimo cha selsiyasi,” kasema Guterres.

Hata hivyo Guterres ameelezea kuvutiwa kwake na uhamasishaji kutoka mashirika ya kiraia, wakiwemo vijana, jamii za watu wa asili, vikundi vya wanawake, majiij na sekta binafsi kwa kuangazia ya kwamba harakati dhidi ya tabianchi zinahitaji kila mtu.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa COP26 huko Glasgow Scotland
UNRIC/Miranda Alexander-Webber
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa COP26 huko Glasgow Scotland

Ahadi za debe tupu hazitatuokoa

Katibu Mkuu pamoja na kupongeza makubaliano ya China na Marekani  kushirikiana katika kukabilia mabadiliko ya tabianchi akisema ni hatua muhimu katika mwelekeo sahihi, “lakini ahadi zinaonekana ni hewa pindi sekta ya mafuta ya kisukuku inaendelea kupatiwa matrilioni ya dola kama ruzuku kupitia vipimo vya IMF. Au pindi nchi zinaendelea kujenga viwanda vya makaa yam awe au pindi hewa ya ukaa inaendelea kuzalishwa na hakuna fedha za ununuzi zinalipwa wale wanaotekeleza miradi ya kupunguza hewa chafuzi,”

Guterres ametaka kila nchi, jiji, mji, kampuni na taasisi za fedha kuweka bayana na kwa njia inayoweza kuthibitishwa mikakati ya kupunguza utoaji hwa chafuzi kuanzia sasa.

Licha ya mkwamo kuna hatua chanya

Licha ya kuona kuna kusuasua, Katibu Mkuu amepongeza maendeleo katika mkutano huo wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 huko Glasgow ikiwemo ahadi za kuondokana na ukataji miti hovyo, kuondokana na uzalishaji wa hewa chafuzi na uwekezaji katika nishati salama na endelevu na ahadi za kuondokana na makaa ya mawe.

Bwana Guterres amesema ataunda kundi la jopo la ngazi ya juu la wataalamu kupendekeza viwango vya kupima ahadi za kutozalisha hewa ya ukaa, na jopo hilo kutoka kwa watendaji wasio wa kiserikali litawasilisha mapendekezo yao mwakani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter