Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yashambulia zaidi wagonjwa wa Kisukari Afrika

Afisa wa afya akifanya uchunguzi wa kisukari kwa mgonjwa barani Afrika.
WHO/Africa
Afisa wa afya akifanya uchunguzi wa kisukari kwa mgonjwa barani Afrika.

COVID-19 yashambulia zaidi wagonjwa wa Kisukari Afrika

Afya

Uchambuzi wa awali wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO umeonesha kuwa idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona au COVID-19 barani Afrika ni kwa wagonjwa wa kisukari.
 

Taarifa ya WHO kanda ya Afrika iliyotolewa leo huko Brazaville, Jamhuri ya Congo imesema uchambuzi huo umefanyika kuelekea siku ya kimataifa ya kutokomeza kisukari duniani taree 14 mwezi huu wa Novemba.

Nchi zilizohusika kwenye uchambuzi huo wa awali ni  Burkina Faso, Chad, Cote d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eswatini, Guinea, Namibia, Niger, Rwanda, Senegal, Seychelles, Sao Tome naPrincipe, na Uganda.

WHO inasema ugonjwa wa kisukari unadhoofisha uwezo wa mwili kuzalisha au kuchakata Insulini ambayo ni kimeng’enyo muhimu cha kukabili ongezeko la kiwango cha sukari mwilini. Kisukari kinasababisha uvimbe na kukwamisha mzunguko wa damu hali ambazo zinaongeza tatizo la afya na uwezekano wa mtu kufa kwa COVID-19.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “COVID-19 inatuma ujumbe dhahiri ya kwamba kukabili janga la kisukari Afrika kwa njia nyingi ni muhimu kama vile watu wanavyokabili Corona.”

Amesema janga la COVID-19 litatulia lakini Afrika inatarajiwa kuendelea kukabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa kisukari katika miaka ijayo, “lazima tuchukue hatua sasa kuepusha wagonjwa wapya wa Corona, tupatie chanjo wagonjwa wa kisukari na muhimu zaidi kubainisha na kusaidia mamilioni ya waafrika ambao bado hawatambui kuwa wanaugua ugonjwa huu wa kisukari unaoua kimya kimya.”

Kwa mwaka huu wa 2021, takribani watu milioni 24 barani Afrika wanakadiriwa kuugua kisukari na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 55 mwaka 2045.