COVID-19 na bwawa la kienyeji vyarejesha uhai wa kijiji kilichotelekezwa Tunisia

Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maeneo ya pwani ya Tunisia yanayoathiri wanadamu na viumbe hai vya baharini.
UNDP Tunisia
Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maeneo ya pwani ya Tunisia yanayoathiri wanadamu na viumbe hai vya baharini.

COVID-19 na bwawa la kienyeji vyarejesha uhai wa kijiji kilichotelekezwa Tunisia

Tabianchi na mazingira

Nchini Tunisia, kitendo cha mwanamke kuamua kubeba jukumu la kilimo cha familia baada ya baba mzazi na kaka yake kufariki dunia kimerejesha uhai katika kijiji hicho ambacho vijana walikimbia kutokana na ukame na mmomonyoko wa udongo.

Saida Zouaoui kutoka familia ya wakulima, akiwa kwenye shamba lililostawi mizeituni nchini Tunisia, anasema babu yao ndiye aliwarithisha mbinu za kienyeji za kutumia udongo maalum kujenga bwawa la kumwagilia maji shambani. 

Hata hivyo bwawa lililojengwa liliharibika na ndoto ya baba yake ilikuwa kulijenga, kwa hiyo ukosefu wa maji ulikimbiza vijana wengi akisema, “Vijana wengi walikimbilia mji mkuu Tunis kufanya kazi za ujenzi, wengine walienda kusoma. Walitelekeza mashamba yao, lakini tulikuwa na matumaini.” 

Hali ikawa mbayá zaidi baada ya kaka na baba yake kufariki dunia na ndipo Saida akaamua kurejea kwenye shamba la familia akisema, “Niliamua kurejesha hali kama wakati wa baba yangu kwa kutimiza ndoto yake. Watu walitambua tu kuna njia moja nataka kufanya, kurekebisha bwawa ili lifanye kazi na kumwagilia eneo lote. Hatukujua la kufanya, ndipo shirika la kazi duniani, ILO lilipoingilia kati likaandaa mkutano nikazungumza kuhusu uhaba wa maji,  mmomonyoko wa udongo na ukame! Bwawa likajengwa! Asante Mungu, tangu wakati huo vijana wameanza kurejea, COVID-19 ilikosesha watu ajira na hivyo wakageukia kilimo kwa kuwa sasa kuna maji.” 

Saida anasema vijana  wamekomboa mashamba yao waliyotelekeza na kwamba kilimo kimekuwa mkombozi wakati wa janga COVID-19 na zaidi ya yote vijana wanaosoma sasa wanabobea kwenye uchumi wa kilimo ili kuwa na mbinu za kisasa zaidi za kilimo biashara kuliko yeye ambaye amejifunza mwenyewe.