Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasioona na viziwi wanahudumiwaje ikiwa watoa huduma hawaelewi kinachosemwa? Vijana Tanzania waja na suluhisho.

Muigizaji Daryl Mitchell (aliyekaa) akihutubia mkutano huku mkalimani wa lugha ya alama akieleza kinachosemwa.
UN Photo/Manuel Elías
Muigizaji Daryl Mitchell (aliyekaa) akihutubia mkutano huku mkalimani wa lugha ya alama akieleza kinachosemwa.

Wasioona na viziwi wanahudumiwaje ikiwa watoa huduma hawaelewi kinachosemwa? Vijana Tanzania waja na suluhisho.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu na afya ya uzazi duniani UNFPA, limeshatangaza kuwa ubinifu utakuwa kitovu cha shughuli zake katika miradi ya mwaka huu na inayoanzia miaka ijayo na tayari vijana katika mataifa mbalimbali na taasisi mbili za vijana nchini Tanzania ni moja ya waliouelewa mtazamo huo kwa haraka na kuanza kuufanyia kazi.  

“Kwa majina naitwa Habibu Mrisho, ni mmoja kati ya viongozi wa Eafya…” Ni kijana wa nchini Tanzania akianza kutambulisha mradi wao walioubuni kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu ili kuwasaidia watu walio na changamoto ya macho, kuweza kuwasiliana. 

“Sisi tunachokifanya tunawasaidia kwa kuwaletea simu za mkononi ambazo wanaweza kuzipata taarifa kwa usahihi na kwa haraka zaidi.” Kijana Habibu Mrisho anaendelea kueleza kuhusu ubunifu wao akisema kuwa tayari mfumo wao uko katika matumizi ya majaribio katika vifaa vya kielekroniki kama simu za mkononi ambazo zinamruhusu mtu asiyeona kuweza kupata taarifa za afya ya uzazi na ujinsia na pia yeye mwenyewe kuweza kujieleza kupitia mifumo waliyoiandaa kama iCast kwa ajili ya watu wenye ulemavu. 

Kijana mwingine ni Salum Abdalah Mauga. Yeye anajitambulisha kuwa anatoka mkoani Iringa. Ni mmmoja wa waanzilishi wa mradi mwingine mpya unaoitwa Frendlicom. Nao unalenga kuwasaidia watu wenye ulemavu, lakini ytofauti na mradi ulioanzishwa na vijana wenzao, huu wa kwao unalenga kwa wale wenye changamoto ya masikio au uziwi. 

“Tunatengeneza mazingira rafiki ya mawasiliano. Tukianza kwenye eneo la afya ambalo ni eneo mama ambalo ndilo tulianza nalo, tumeanza kutengeneza mfumo wa kielektroniki ambao tumeupa jina la Clean Kit.” Salum Mauga anafafanua akiongeza, “ni kiti ambayo inamsaidia mtoa huduma, katika kilniki ya mama mjamzito na mtoto, kuweza kumuhudumia mtu mwenye ulemavu wa kusikia. Kwa sababu changamoto inaonekana kuwa mtu mwenye changamoto ya ukiziwi, anapozungumza katika lugha ya alama, mtoa huduma anakuwa haelewi ile lugha na mtoa huduma anapoongea katika lugha ya kawaida, huyu mwingine anakuwa hasikii kwa hivyo kunakuwa na changamoto pale. Hivyo ili kuondoa changamoto hiyo, mfumo wetu unakuwa na kamera, anapozungumza kwa lugha ya alama, kamera inadaka zile alama zake, ambazo yeye anazungumza, halafu kompyuta kupitia mfumo wetu inaweza kutafsiri zile alama kwenda kwenye lugha ya kawaida ya maandishi na maneno ambayo mtoa huduma anaweza akaelewa na akamjibu au akampatia huduma ambayo anaihitaji.” 

Felister Bwana ni Afisa wa UNFPA ambaye ni mtaalamu wa katika mifumo ya afya lakini pia kiongozoi katika kitengo cha afya ya uzazi ambaye pia anasimamia masuala ya ubunifu. Bi Bwana anasema uvumbuzi kama huu wanaoufanya vijana unawasaidia UNFPA kwani suala la afya ya uzazi na ujinsia ni masuala tata ambayo kwa kutumia njia zilizozooeleka inakuwa vigumu kupata matokeo chanya kwa haraka, “bila kuangalia njia mbala ya kuweza kusaidia Agenda 2030 ambayo inatakiwa kwenda haraka, tutaendelea kubaki palepale kwa hiyo ubunifu umetufanya sisi kama UNFPA tubadilike namna ya kufanya programu. Mwanzo tulikuwa hatuwazi kutumia ubunifu lakini mara ya kwanza tulivyoanza sisi Tanzania, sasa hivi mpango mkakati wa UNFPA yote huu unaoisha mwaka huu na unaokuja, yote imeweka ubunifu kama kitovu cha programu.”