Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wanabeba mzigo mkubwa wa janga la tabianchi – COP26 

Mwanaharakati kutoka Samoa Brianna Fruean akiwa na kikaragosi Little Amal katika jukwaa moja kwenye COP26. Kikaragosi kikubwa hicho kinamuwakilisha msichana mdogo mkimbizi raia wa Syria
UN News/Laura Quinones
Mwanaharakati kutoka Samoa Brianna Fruean akiwa na kikaragosi Little Amal katika jukwaa moja kwenye COP26. Kikaragosi kikubwa hicho kinamuwakilisha msichana mdogo mkimbizi raia wa Syria

Wanawake wanabeba mzigo mkubwa wa janga la tabianchi – COP26 

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP26 unaoendelea mjini Glasgow nchini Uskochi umeonesha kuwa kundi la wanawake linachukua asilimia 80 ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi na kwa hivyo kundi hilo linabeba zaidi mzigo mkubwa wa janga la tabianchi. 

Leo Jumanne, wanawake wametawala jukwaa la COP26 kuonesha kwamba mabadiliko ya tabianchi hayana usawia kijinsia na kwamba hatua katika nyanja hii zinahitaji ushiriki wa wanawake. 

Hoja ni kwamba kuwekeza kwa wanawake na wasichana kunaleta matokeo makubwa ambayo yanaigusa jamii nzima, na maarifa ya mstari wa mbele ambayo wanayo yanahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote. 

Ongezeko la joto 

Jukumu la wanawake linakuwa muhimu zaidi baada ya kutolewa kwa uchambuzi mpya unaoonesha kuwa matangazo ya viongozi wa dunia katika COP26 bado yanaiacha sayari kwenye njia ya janga la ongezeko la joto duniani. 

Baada ya kusafiri takribani kilomita elfu 13 kote Ulaya, Little Amal, kikaragosi mkubwa anayewakilisha msichana mdogo mkimbizi wa Syria, aliwasili Glasgow kwa wakati, kwa ajili ya "Siku ya Wanawake" katika COP26. 

Kikaragosi huyo mwenye urefu wa mita 3.5 amewashangaza waliohudhuria mkutano huo alipopanda ngazi na kuungana na mwanaharakati wa tabianchi kutoka Samoa, Brianna Fruean kukumbatiana na kubadilishana zawadi. Brianna alimpa ua, likiwakilisha matumaini na mwanga, na Amal akalirudisha na mfuko wa mbegu. 

Mwanaharakati huyo amesema, “tunaanza safari hapa, kutoka sehemu mbili tofauti, lakini tumeunganishwa kwa kuwa tunaishi katika ulimwengu uliovunjika ambao umewatenga wanawake na wasichana kwa utaratibu. Hasa wanawake na wasichana kutoka jamii zilizo hatarini.” 

Rasilimali asilia na ikolojia 

Katika nchi zinazoendelea, wanawake huwa wa kwanza kusimamia mazingira yanayowazunguka. Kutokana na kukusanya maji kwa ajili ya kupikia na kusafisha, kutumia ardhi kwa ajili ya mifugo, kupata chakula kwenye mito na miamba, na kukusanya kuni, wanawake katika sayari nzima hutumia na kuingiliana na maliasili na mifumo ikolojia kila siku. 

Kwa mujibu wa Shiŕika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, na mashiŕika mengine ya Umoja wa Mataifa, wanawake pia ni watu wa kwanza kuhisi madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwani wanalazimika kusafiri umbali mkubwa zaidi kutafuta kile wanachohitaji kulisha familia zao. 

Zaidi ya hayo, pamoja na kwamba uharibifu wa mazingira una madhara makubwa kwa binadamu wote, unaathiri hasa sekta zilizo hatarini zaidi katika jamii, hasa wanawake ambao afya zao ni tete wakati wa ujauzito na uzazi. 

Ahadi 

Inger Andersen amesema kwamba akiangalia matokeo yanayotokana na ahadi zinazotolewa, kwa uwazi kabisa ni kama "tembo anayezaa panya". 

Kwake, Inger Anderson, inahitajika kufikiria ikiwa hii ni nzuri vya kutosha au ikiwa ulimwengu unaweza kupanua zaidi, pamoja na mipango iliyoboreshwa na ahadi kwa sababu "ulimwengu utapunguza tu asilimia 8 ya uzalishaji mwishoni mwa miaka hii kumi". 

Bi Andersen anaona kuwa ni chanya kuona nchi zinakubali takwimu na kushiriki katika mazungumzo kama ilivyokuwa huko Paris, lakini kwamba haikuwa vizuri kutambua kwamba ahadi kwa ujumla hazieleweki, sio wazi. 

Mkuu huyo wa UNEP amesisitiza kuwa mwelekeo katika baadhi ya nchi msisitizo umekuwa kwenye gesi zinazochafua mazingira, wengine kwenye hewa ukaa pekee.