Watu 11,000 walazimika kusaka usalama Uganda wakikimbia mapigano DRC:UNHCR

Kundi la waomba hifadhi raia wa Kongo wakiwa wameketi wanasubiri kuingia nchini Uganda kupitia mpaka wa Bunagana wakitokea nchini DRC
© UNHCR
Kundi la waomba hifadhi raia wa Kongo wakiwa wameketi wanasubiri kuingia nchini Uganda kupitia mpaka wa Bunagana wakitokea nchini DRC

Watu 11,000 walazimika kusaka usalama Uganda wakikimbia mapigano DRC:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Wimbi la mapigano mapya yaliyozuka Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC limewalazimisha takriban watu 11,000 kukimbia na kuvuka mpaka kuingia nchi Jirani ya Uganda kusaka usalama tangu Jumapili usiku limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. 

Akizungumza na waandishi wa Habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo amesema “Hii inawakilisha wimbi kubwa la wakimbizi kukimbia katika siku moja nchini kwa zaidi ya mwaka mmoja.”  

Ameongeza kuwa mapigano kati ya makundi ya wanamgambo na wanajeshi wa Congo yanafanyika katika wilaya ya Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini na idadi kubwa ya waliovuka mpaka ni wanawake na watoto. 
Baadhi ya waomba hifadhi 8,000 walivuka katika mji wa Bunagana na wengine 3,000 katika mpaka wa Kibaya wilayani Kisoro.  

Mipaka yote miwili iko kilomita 500 Kusini Magharibi mwa mji mkuu wa Uganda Kampala.  
Wahamiaji hao wapya wamewaambia wafanyakazi wa UNHCR kwamba mapigano yalikuwa yakiendelea katika vijiji vya Binja, Kinyarugwe na Chanzu. 

UNHCR inasema watu wengi waliokimbia walikuja na vyombo vya kupikia, mikeka ya kulalia, nguo na mifugo, na walikusanyika kwa haraka huku wakikimbia.  

Baadhi wanaonekana kuanza kurudi katika maeneo ya mbali kutoka katika maeneo ya mpakani. 

UNHCR na serikali ya Uganda wanawasaidia 

UNHCR na ofisi ya waziri mkuu wa Uganda, ambayo inasimamia vituo kadhaa vya usafiri kwa wanaotafuta hifadhi kwenye mpaka wa Congo, wanashughulikia dharura hiyo kwa uratibu na mamlaka za wilaya na mitaa. UNHCR tayari imehamisha takriban watu 500 wanaotafuta hifadhi hadi kituo cha karibu cha Nyakabande, ambacho kinaweza kuhifadhi hadi watu 1,500. 

Wanaotafuta hifadhi huko Nyakabande wanapimwa COVID-19, kusajiliwa na kupewa maji, chakula, malazi na vitu vingine kama vile blanketi.  

Mfumo maalum umewekwa ili kutambua na kufuatilia haraka watu wanaohitaji usaidizi wa dharura.  

Kwa mujibu wa UNHCR washirika kadhaa pia wanashughulikia dharura hii ikiwa ni pamoja na shirika la huduma na msaada kwa watu waliolazimika kufurushwa makwao, Timu za Kimataifa za Matibabu, shirika la Save the Children, shirika la msalaba mwekundu la Uganda na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP

Mipaka ya Uganda imefungwa kwa wanaotafuta hifadhi kutokana na vikwazo vya COVID-19, lakini serikali kwa mara nyingine imetumia utu wa kibinadamu na kuwapokea watu wanaosaka usalama. 

UNHCR inaipongeza Uganda kwa kuruhusu wale wanaotafuta hifadhi kuingia nchini humo.  

“Hata hivyo, tuna wasiwasi kwamba uwezo na huduma za ndani unaweza kuzidiwa hivi karibuni na kuomba rasilimali za haraka kushughulikia mahitaji ya watu wapya wanaowawasili.” 

Hadi kufikia sasa mwaka huu, UNHCR imepokea asilimia 45 pekee ya fedha inazohitaji kwa ajili ya shughuli zake nchini Uganda, nchi ambayo inahifadhi wakimbizi wengi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika.  
Duniani kote kuna nchi tatu pekee zinazohifadhi wakimbizi zaidi.