Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani wa Nepal anayehudumu DRC ashinda tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke

Mrakibu wa polisi Sanya Malla kutoka Nepal ambaye kwa asasa anahudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, ameshinda tuzo ya mwaka 2021 ya Askari Mwanamke wa mwaka wa Umoja wa Mataifa
United Nations
Mrakibu wa polisi Sanya Malla kutoka Nepal ambaye kwa asasa anahudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, ameshinda tuzo ya mwaka 2021 ya Askari Mwanamke wa mwaka wa Umoja wa Mataifa

Mlinda amani wa Nepal anayehudumu DRC ashinda tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke

Amani na Usalama

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Nepal Sangya Malla anayehudumu katika ujumbe wa Umoja huo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo -DRC, MONUSCO ameshinda tuzo ya Afisa Polisi Mwanamke wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2021.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikabidhi tuzo hiyo amesema“ kwa heshima kubwa napenda kutunuku tuzo ya 11 ya Afisa Polisi Mwanamke wa Umoja wa Mataifa kwa Mrakibu wa Polisi Sangya Malla wa Nepal. Malla umeifanya nchi yako, pamoja na MONUSCO na familia nzima ya Umoja wa Mataifa kujivunia.” 
 
Guterres amesema hayo kupitia ujumbe wake kwa njia ya video kwa mkutano wa kuadhimisha kuanza kwa wiki ya Polisi wa Umoja wa Mataifa, mkutano unaofanyika kwa njia ya mtandao. 
  
Mrakibu Malla mbali ya kuwa polisi pia ana taaluma ya utabibu ambapo kwa kutumia taaluma hizo yeye na timu anaoiongoza wameweza kuhakikisha wanasimamia na kuhamasisha masuala ya afya na mazingira huku wakiendelea na shughuli za kulinda amani nchini DRC. 
 
Miongoni mwa yale aliyoweza kufanikisha ni pamoja na kuandaa semina zaidi ya 300 kwa mwaka huu pekee kuelimisha wananchi wa DRC kuhusu ugonjwa wa Corona au COVID-19 na majanga mengine ikiwemo Ebola. 
  
Halikadhalika wakati wa mlipuko wa volkano ya mlima Nyiragongo huko Goma mwezi Mei mwaka huu 2021, Mrakibu wa Polisi Malla na kitengo chake ndio haswa walitahadharisha wakazi wa eneo hilo na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatua za tahadhari na watu wakafanikiwa kuondoka kwenye enoe hatari na kuelekea maeneo salama ikiwemo nchi jirani ili kuokoa maisha yao. 
 

Mshindi wa tuzo ya Askari mwanamke wa mwaka wa Umoja wa Mataifa 2021 Mrakibu Sangya Malla anayehudumu nchini DRC akiwa katika shughuli za mazingira
Sangya Malla
Mshindi wa tuzo ya Askari mwanamke wa mwaka wa Umoja wa Mataifa 2021 Mrakibu Sangya Malla anayehudumu nchini DRC akiwa katika shughuli za mazingira


Katibu Mkuu alimwagia sifa kwa kazi nzuri anayofanya na kusema “Alisaidia kuanzisha na sasa anaongoza Kitengo cha Afya na Mazingia cha MONUSCO, akiimarisha usalama na ustawi wa walinda amani wetu kwa kupunguza hatari za  COVID-19 na vitisho vingine. Anawakilisha kitu kikubwa zaidi, michango mingi ya maafisa wa polisi wanawake katika kuendeleza amani na usalama duniani kote. Kupitia kazi yake, Mrakibu wa polisi Malla anaonesha kazi bora inayofanywa na Umoja wa Mataifa”  
 
Akipokea tuzo hiyo Mrakibu Malla ameshukuru na kusema "Nimefurahi kupokea tuzo hii, na ninatumai itawapa moyo wanawake vijana zaidi katika nchi yangu na kote ulimwenguni kufuata taaluma ya polisi, ambayo bado inatazamwa kama kazi ya wanaume". 
  
Naye Mshauri wa Polisi wa Umoja wa Mataifa Luis Carrilho amesema “kama walinda amani wengi wakati huu wa changamoto za usalama huku kukiwa na janga hili la Corona, Mrakibu Malla amevuka wito wa kuhudumia jamii, pamoja na timu yake, juhudi zake za kuongeza ufahamu kuhusu afya ya umma na hatari za asili hatimaye zimewafanya wafanyakazi wenzake na watu wa DRC kuwa salama zaidi ambayo ni kazi kuu ya polisi." 
  
Kitendo cha polisi wa Umoja wa Mataifa kimefikia lengo la usawa kijinsia katika ngazi zote za wafanyakazi.