WFP yaonya watu milioni 3 zaidi sasa 'wanakabiliwa na makali ya njaa'

Wazee na watoto wenye utapiamlo katika maeneo ya kusini ya Madagascar wako hatarini zaidi.
© WFP/Krystyna Kovalenko
Wazee na watoto wenye utapiamlo katika maeneo ya kusini ya Madagascar wako hatarini zaidi.

WFP yaonya watu milioni 3 zaidi sasa 'wanakabiliwa na makali ya njaa'

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limeonya kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa katika nchi 43, imeongezeka hadi kufikia milioni 45, yaani juu kwa ongezeko la watu milioni tatu mwaka huu huku njaa kali ikiongezeka kote ulimwenguni. 

Idadi hii imeongezeka kutoka milioni 42 mapema mwaka huu, na milioni 27 mnamo mwaka 2019, shirika hilo limesema katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Roma Italia. 

Taarifa hiyo ya WFP imeendelea kueleza kuwa ongezeko hilo linatokana na wale ambao wanaishi katika maeneo yaliyowekwa katika kiwango cha njaa 4 cha njaa yaani IPC4 na zaidi, kama vile nchini Afghanistan, pamoja na ongezeko nchini Ethiopia, Haiti, Somalia, Angola, Kenya na Burundi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP David Beasley amesema, "mamilioni ya watu wanachungulia kwenye shimo. Tuna mgogoro, mabadiliko ya tabianchi na COVID-19 inayoongeza idadi ya walio na njaa kali, na takwimu za hivi karibuni zinaonesha sasa kuna zaidi ya watu milioni 45 wanaojongea kuelekea kwenye njaa. "  

"Gharama za mafuta zimepanda, bei za vyakula zinapanda, mbolea ni ghali zaidi, na yote haya yanaingia kwenye majanga mapya kama ile inayotokea sasa nchini Afghanistan, pamoja na dharura za muda mrefu kama Yemen na Syria." Beasley ameongeza. 

Mahitaji yanazidi rasilimali  

Aidha WFP imesema kuwa kwa  pamoja na washirika wa kibinadamu katika maeneo yenye njaa duniani kote, wanafanya kila linalowezekana kuongeza misaada kwa mamilioni ambao ambao wako katika hatari ya njaa. Hata hivyo, rasilimali zilizopo haziwezi kuendana na mahitaji, wakati ambapo njia za ufadhili za jadi au zilizozooeleka ziko katika shida kubwa. 

WFP inakadiria kuwa gharama ya kuzuia njaa duniani sasa inafikia dola bilioni 7 za kimarekani, kutoka bilioni 6.6 mapema mwaka huu. 

"Gharama ya usaidizi wa kibinadamu inapopanda kwa kasi, tunahitaji fedha zaidi kufikia familia kote ulimwenguni ambao tayari wamemaliza uwezo wao wa kukabiliana na njaa kali.” Amesema mkuu huyo wa WFP, Bwana Beasley. 

Shirika hilo limeongeza kuwa familia zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, zinalazimika kufanya "machaguo ya kutisha ili kukabiliana na njaa inayoongezeka." 

Uchambuzi wa uwezekano wa kuathirika katika nchi 43 zilizofanyiwa utafiti, unaonesha familia zikilazimishwa kula kidogo, au kuruka milo kabisa. Wakati fulani watoto wanalishwa, wakati wazazi wanajitolea kukosa chakula, na wanalazimishwa kukaa na njaa. 

Huko Madagascar, ambako tayari kuna njaa, WFP inasema wengine wanalazimika kula nzige, majani-mwitu, au dungusi kakati ili kuishi.