Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP26: Watu wa asili wana nafasi kubwa ya pekee katika kuzuia mabadiliko ya tabianchi 

Wanaharakati kutoka makundi ya watu wa asili wameandamana katika mitaa ya jiji la Glasgow wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa tabianchi, COP26
UN News/Grace Barret
Wanaharakati kutoka makundi ya watu wa asili wameandamana katika mitaa ya jiji la Glasgow wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa tabianchi, COP26

COP26: Watu wa asili wana nafasi kubwa ya pekee katika kuzuia mabadiliko ya tabianchi 

Tabianchi na mazingira

Mamilioni ya watu wameingia kwenye mitaa ya miji kote ulimwenguni ikiwa ni pamoja na viunga vya mji wa Glasgow nchini Uskochi unakofanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi COP26 wakidai hatua kubwa zaidi ya tabianchi huku nchi zinazoshiriki katika mazungumzo ya COP26 zikiwa zimeahidi kuwekeza katika masuluhisho yasiyoharibu tabianchi kupitia kilimo.  

Katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi, COP26, ambao unaendelea Glasgow, Uskochi, ‘Mother Nature’ au Mama Asili, au "Pachamama", kama baadhi ya watu wa asili wa Amerika ya Kusini wanavyosema, limekuwa neno muhimu zaidi Jumamosi hii na watu wa kiasili wamekuwa katikati ya shughuli za Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka huu yaani COP26. 

Asili ni muhimu kwa maisha yetu: hutoa oksijeni muhimu, hudhibiti tabianchi, hutoa chakula na maji kwa viumbe vyote vilivyo hai, na ni nyumbani kwa aina nyingi za maisha ya wanyama. 

Nguvu ya watu wa asili 

Na hakuna anayejua vyema jinsi ya kulinda asili kuliko watu wa asili, ambao wanashiriki kikamilifu ndani na nje ya COP26 huko Glasgow, wakifanya kazi kushawishi mazungumzo kwa kila njia iwezekanavyo, ikiwa ni pamoja na maandamano ya mitaani. 

Wakili na mwanaharakati wa haki za ardhi kwa watu wa asili Eloy Terena alisafiri kutoka Brazil hadi Glasgow na kueleza UN News kwa nini ni muhimu kujumuisha watu wa asili katika mazungumzo. Anasema,"tulikuja kuleta ujumbe wazi kabisa, kwamba haiwezekani kufikiria kukabiliana na janga la tabianchi bila mazungumzo na watu wa asili na bila kufikiria juu ya ulinzi wa himaya hizi. Kwa sababu maeneo yetu, bila shaka, yana jukumu la msingi katika usawa wa tabianchi. 

UN News pia imezungumza na Mjumbe Maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa asili Victoria Tauli-Corpuz. Anakumbuka kwamba jamii za kiasili ndizo wataalamu wakubwa katika kuishi kwa amani na asili, na kwamba maeneo yao yana asilimia 80 ya baiyonuai duniani.