Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana washika hatamu COP26 wakitaka vitendo kulinda tabianchi

Wanaharakati vijana wa mazingira wakiwa kwenye maandamano huko Glasgow, Scotland Ijumaa 05 Novemba 2021 wakati wa COP26
UN News/Laura Quinones
Wanaharakati vijana wa mazingira wakiwa kwenye maandamano huko Glasgow, Scotland Ijumaa 05 Novemba 2021 wakati wa COP26

Vijana washika hatamu COP26 wakitaka vitendo kulinda tabianchi

Tabianchi na mazingira

“Tunataka nini? Haki kwa tabianchi! Tunataka lini? Sasa!” Kauli hizo zimesikika zikipazwa na vijana eneo lote la kati la mji wa Glasgow huko Scotland hii leo Ijumaa wakati maelfu ya waandamanaji walipoingia mitaa ya mji katika siku ambayo mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 ulitenga kwa ajili ya vijana

.Ijapokuwa maandamano hayo yaliandaliwa na kikundi kiitwacho Fridays for Future kinachoongozwa na mwanaharakati kijana kutoka Sweden, Greta Thunberg, watu wa rika mbalimbali walikusanyika bustani ya George mjini humo wakitaka hatua na vitendo zaidi kulinda tabianchi.
Kuanzia watoto wadogo wakiwa na vipeperushi vilivyotengenezwa kwa mikono hadi watu wazima wakidai mustakabali salama kwa vizazi vijavyo.

Maandamano makubwa zaidi yanatarajiwa Jumamosi

Jane Mansfield, raia wa Wales moja ya nchi zinazojumuisha Uingereza alibeba kibango kimeandikwa, “alama nyekundu kwa ubinadamu,” kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliyotumia baada ya ripoti ya jopo la wataalamu la IPCC kueleza mapema mwaka huu kuwa kuna janga kubwa la tabianchi.

"Kwa kweli ninajali sana kuhsu dunia ambayo tunaachia vizazi vijavyo na kile tunachofanyia nchi za kusini. Ninaishi kusini-magharibi mwa Wales, na mabadiliko ya tabianchi kweli yanatokea, lakini hatujafikia hata kile kinachotokea katika maeneo mengine ya dunia na nina hofu kubwa,” Bi. Mansfield amemweleza mwandishi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa aliyeko Glasgow.

Viongozi wa jamii ya asili kutoka Amerika ya Kusini nao walikuwepo kwenye maandamano ya leo. Walikuwa wanaongoza maandamano hayo na wengi wao walisikika wakituma ujumbe kwa viongozi wa dunia wakisema: acheni kuzidua rasilimali na acheni hewa ya ukaa ardhini.’

“Watu wa jamii ya asili wanafia mtoni, wanasombwa na mafuriko makubwa. Nyumba zao zinasombwa na maji, shule zilizofurika watoto, madaraja, vyakula vyetu na kila kitu vimesombwa,” walisikika wakitoa kauli hizo kwenye bustani ya George.

Wakati huo huo, baadhi ya wanaharakati walivaa vichwa vya vikaragosi vya marais na mawaziri wakuu huku wameshika vibao vikiwa vimeandikwa ‘kamata wahalifu watabianchi’.

Wanaharakati vijana wakiandamana katika mitaa ya Glasgow, Scotland kunakofanyika mkutano wa COP26
UN News/Laura Quinones
Wanaharakati vijana wakiandamana katika mitaa ya Glasgow, Scotland kunakofanyika mkutano wa COP26

Vitendo zaidi vinahitaijka

Mwanaharakati kutoka Sweden Greta Thunberf alikuwa wa mwisho kuzungumza kwenye jukwaa la maandamano hayo ambako amekosoa vongozi wa dunia kwa ‘longolongo’ au maneno matupu miaka 26 tangu kuanza kwa mikutano ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi na kutilia shaka uwazi wa ahadi ambazo wametoa wakati wa mkutano wa sasa wa COP.

“Viongozi hawafanyi chochote; wako wanajiwekea upenyo wa kukwepa na kuweka mifumo ya kujinufaisha na kuendelea kufaidia na mfumo haribifu wa sasa. Hiki ndio kitu wamechagua wenyewe kuendelea kuharibu mazingira ya sasa na ya vizazi vijavyo”, amesema Greta huku akiita mkutano wa COP26 kuwa ni tukio la ulaghai.

Wajumbe wengine wa shirika la Fridays for Future wakizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa wametaka ushiriki zaidi na bora wa vijana katika mashauriano yanayoendelea hivi sasa kwenye COP26.

“Kila mwaka tumekuwa tunakatishwa tamaa na COP, na sifikirii mwaka huu itakuwa tofauti. Kuna matumaini lakini wakati huo huo hatuoni hatua za kutosha, hatuwezi kufanikisha kituo chochote kwa ahadi hewa”- Mwanaharakati kijana

“Kila mwaka tumekuwa tunakatishwa tamaa na COP, na sifikirii mwaka huu itakuwa tofauti. Kuna matumaini lakini wakati huo huo hatuoni hatua za kutosha, hatuwezi kufanikisha kituo chochote kwa ahadi hewa”, mwakilishi wa wachechemuzi vijana kwa ajili ya tabianchi kutoka Ufilipino.
“Mashauriano yanaendelea lakini bado tuko hapa mitaani kwa sababu hatujajumuishwa. Matajiri wanakuja kwa ndege za kukodi na kupitisha uamuzi. Tuko hapa na tunapuuzwa. Tutajiwekea nafasi yetu.”, amesema mchechemuzi mwingine kijana.

Kauli ya vijana

Wito huo huo umetolewa kwenye mkutano uliopatiwa jina, Blue Zote ambako wanaharakati wa mazingira kutoka YOUNGO ambacho ni uwakilishi wa watoto na vijana katika Umoja wa Mataifa wamempatia Rais wa COP26 na viongozi wengine taarifa iliyotiwa saini na vijana 40,000 wakitaka mabadiliko.

Taarifa yao inajumuisha maeneo kadhaa yanayowatia hofu ikiwemo kujumuishwa kwao katka mashauriano kuhusu tabianchi. Wanataka pia Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC Patricia Espinosa, kuunga mkono juhudi zao za kutaka kuwepo na ibara katika azimio la mwisho la mkutano huo inayotaja umuhimu wa vijana katika kulinda tabianchi.

“Tutakuwa tunaleta masuala haya na matakwa yetu kwa wajumbe na yote haya ni sawa na yanaelezeka,” amesema Bi. Espinosa wakati akizungumza na viongozi vijana.

Taarifa  hiyo ambayo pia iliwasilishwa kwa mawaziri inataka hatua zaidi katika ufadhili kwa tabianchi, usafirishaji, ulinzi wa wanyamapori na mazingira.

“Kokote pale nilikotembelea duniani, nimeguswa na mguso na ari ya vijana ya hatua kwa tabianchi. Sauti za vijana zinapaswa kusikilizwa na kuakisiwa katika mashauriano hapa COP. Vitendo na uchambuzi unaofanywa na vijana ni muhimu katika kuhakikisha kiwango cha joto hakizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi na hatimaye kuacha kabisa kuzalisha hewa ya ukaa,” amesema Alok Sharma Rais wa COP26.