Nusu ya watu duniani watakuwa katika hatari ya mafuriko, vimbunga na Tsunami ifikapo 2030:UN

Nusu ya watu duniani watakuwa katika hatari ya mafuriko, vimbunga na Tsunami ifikapo 2030:UN
Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu Tsunami Umoja wa Mataifa umeonya kwamba kufikia mwaka wa 2030, inakadiriwa kuwa asilimia 50 ya watu wote duniani wataishi katika maeneo ya pwani ambayo yanakabiliwa na mafuriko, vimbunga na tsunami.
Ndio maana Umoja huo umechagua “kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa nchi zinazoendelea”, kama maudhui ya mwaka huu ya siku ya kuelimisha umma kuhusu uelewa wa Tsunami.
Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi zote, mashirika ya kimataifa, na mashirika ya kiraia, kuongeza uelewa wa tishio hilo hatari, na kubadilishana mbinu za ubunifu za kupunguza hatari zake.
Antonio Guterres amesema "Tunaweza kuendeleza hatua zilizofikiwa kuanzia kwa elimu bora hadi kwa jamii zilizoathiriwa na tsunami kote ulimwenguni, hadi kujumuishwa kwa mpango wa Tsunami katika muongo wa Umoja wa Mataifa wa sayansi ya bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu".
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya, hata hivyo, kwamba hatari "zinasalia kuwa kubwa. Kuongezeka kwa viwango vya kina cha bahari kunakosababishwa na dharura ya mabadiliko ya tabianchi kutazidisha nguvu za uharibifu za tsunami".
Kwa mantiki hiyo amesema ni "Lazima tupunguze ongezeko la joto duniani hadi kusalia katika nyuzijoto 1.5 juu ya wastani wa kabla ya mapinduzi ya viwanda na kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika kujenga mnepo wa jamii za pwani."
Ujumbe wake umeongeza kuwa ukuaji wa haraka wa miji na utalii unaokua katika maeneo yanayokumbwa na Tsunami, pia unawaweka watu wengi zaidi katika hatari.

Juhudi za pamoja
Kwa Bw. Guterres, sayansi, ushirikiano wa kimataifa, kujitayarisha na hatua za mapema lazima ziwe kiini cha juhudi zote za kuweka watu na jamii salama zaidi.
Amesisitiza kuwa "Kuongeza msaada kwa nchi zinazoendelea na kuboresha utambuzi na mfumo wa tahadhari za mapema ni muhimu. Katika kukabiliana na kuongezeka kwa migogoro migumu ya kimataifa, tunahitaji kujiandaa vyema,”
Mwaka huu wa 2021, siku ya kimataifa ya uelimishaji umaa kuhusu Tsunami inaangazia "Kampeni ya Sendai Seven," lengo ambalo mahsusi linatazamiwa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa nchi zinazoendelea.
Katibu Mkuu anahitimisha ujumbe wake kwa wito wa kutekeleza mkakati wa Sendai, na, kwa pamoja, kujenga mnepo dhidi ya majanga yote.

Nadra lakini inaangamiza
Tsunami ni matukio ya nadra lakini yanaweza kuangamiza kwa kiasi kikubwa. Katika miaka 100 iliyopita, matukio 58 yamekatili maisha ya watu zaidi ya 260,000, au wastani wa watu 4,600 kwa kila jangaidadi ikiwa ni zaidi ya majanga mengine yoyote hatari ya asili.
Idadi kubwa zaidi ya vifo ilitokea katika tsunami ya bahari ya Hindi ya Desemba 2004, ambayo ilisababisha vifo vya takriban watu 227,000 katika nchi 14 na Indonesia, Sri Lanka, India na Thailand ndizo zilizoathirika zaidi.
Wiki tatu tu baada ya maafa, jumuiya ya kimataifa ilikutana Kobe, Japani, na kupitisha mfumo wa utekelezaji wa miaka 10 wa Hyogo, ambayo ni makubaliano ya kwanza ya kina ya kimataifa kuhusu kupunguza hatari ya maafa.
Pia waliunda mkakati wa tahadhari na kupunguza Tsunami Bahari ya Hindi, ambao unatumia vituo vya ufuatiliaji wa hali ya hewa na usawa wa kina cha bahari ili kutuma taarifa kwa vituo vya kitaifa vyataarifa kuhusu tsunami.
Baada ya mfumo wa utekelezaji wa Hyogo kumalizika, mwaka 2014, ulimwengu ulipitisha mkakati wa Sendai wa kupunguza hatari za majanga wa mwaka 2015-2030, ukielezea malengo saba ya wazi na vipaumbele vinne vya kuzuia na kupunguza hatari za majanga.