Vijana tunaweza ni wakati wa kutushirikisha kwa vitendo katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:Nzambi

5 Novemba 2021

Wakati mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP26 ukiendelea mjini Glasgow Scotland, vijana wanatoa wito kwa viongozi kutekeleza kwa vitendo ushirikishwaji wa vijana katika vita dhidi ya janga hilo.

Mkutano huo wa wiki mbili leo umejikita na mada ya ushirikishwaji wa vijana na umma katika kuhakikisha janga hili ambalo tayari limeadhiri mamilioni ya watu duniani haliendeleo kuleta zahma.

Miongoni mwa vijana walio msitari wa mbele katika kuitikia kwa vitendo wito huo ni Nzambo Matee mwanasayansi, mhandisi na mjasiriamali kutoka nchini Kenya ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya mazingira ya shirika la Umoja wa Mataifa la UNEP, ya Champion of the Earth 2020.  

Nzambi ambaye pia ni mwanzilishi wa kampuni ya Gjenge markers inayobadili taka za plastiki kuwa tofali za ujenzi akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema “Mkutano huu ni muhimu sana na tunatarajia utoe mwongozo na mwelekeo wa wapi tunakwenda na kile ambacho kitatusaidia vijana kuonyesha mchango wetu.”

Akisistiza kuwa sasa ni wakati wa vitendo na sio kupiga domo Nzambi amesema “Kama ni kusema tumesema sana na viongozi wamekuwa wakikutana na kuzungumza kila mara sasa ni wakati wa kuacha kuzungumza tu na kuchukua hatua. Kwani vijana tumedhihirisha uwezo tunao, ubunifu tunao sasa tunahitaji kushikwa mkono na kupewa mwongozo unaostahili kwa vitendo.”

Bi. Nzambi ameiasa dunia kwamba “Tusipochukua hatua sasa wakati tunafikia umri wa uzee athari za mabadiliko ya tabianchi zitakazotukumba tutajutia ni kwa nini hatukuchukua hatua sasa na hakutakuwa na mtu mwingine wa kumlaumu bali sisi wenyewe.”

Kwa vijana wenzake amewaambia kwamba “hakuna lisilowezekana ukitia bidi na ukiwa na ari, na ni wakati wa vijana kushika usukani kupambana na janga hili ambalo litatuathiri zaidi sisi. Tuanze kuonyesha uwezo wet una tutangulie mbele kisha serikali itatukuta tumeshaanza na tunaendelea. Tusisubiri kufanyiwa kidogo tulichonacho kinatosha kuanza kupanda mbegu.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter