Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtanzania Imani Nsamila mpigapicha za mazingira, ashinda tuzo ya EU GCCA+

Imani Nsamila (wa nne nyuma kutoka kushoto) akiwa na kundi la wasichana waliohudhuria warsha ya upigaji picha.
UN/Imani Nsamila
Imani Nsamila (wa nne nyuma kutoka kushoto) akiwa na kundi la wasichana waliohudhuria warsha ya upigaji picha.

Mtanzania Imani Nsamila mpigapicha za mazingira, ashinda tuzo ya EU GCCA+

Tabianchi na mazingira

Kijana Mtanzania mpigapicha za mazingira Imani Nsamila ametangazwa kuwa mshindi wa Tuzo za Vijana za EU GCCA+ zinazolenga kuwasaidia wanahabari wachanga, waandishi na wapiga picha kusimulia taarifa au simulizi zenye nguvu za tabianchi kote ulimwenguni.

GCCA+ au The Global Climate Change Alliance Plus Initiative ni mpango mkuu wa Umoja wa Ulaya ambao unasaidia nchi zilizo hatarini zaidi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ushindi wa Nsamila umetangazwa hii leo mjini Brussels, Ubeligiji katika moja ya mikutano ya kandoni mwa mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26, unaoendelea Glasgow Uskochi. Nsamila amezipokea taarifa za ushindi akiwa jijini Dar es Salaam Tanzania ambako amezungumza na Stella Vuzo wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa kuhusu tuzo hii. Nsamila anasema,“picha iliyonipa ushindi sio moja. Kwa sababu wao walikuwa wanataka simulizi kwamba wewe unataka kueleza simulizi fulani na walikuwa mahususi kabisa kwamba sisi hatutafuti habar iza papo kwa papo au zile za kila siku, tunatafuta watu wanaoweza kutumia ubunifu w atalanta zao kwenye kuangazia mabadikilo ya tabianchi.”


Kijana huyo anasema baada ya kuyaona masharti hayo na baada ya kujitathimini yeye mwenyewe kwamba hapendi kuonesha matatizo bali majawabu, “kwa hiyo nilichoamua mimi nilifanya utafiti nikampata mwananchi mmoja mkoani Dodoma anaishi Chamwino, ambAye katika kufuatilia yeye ni mnufaika wa mradi wa WFP wa Boresha lishe ambao ulipata ufadhili kutoka Muungano wa Ulaya, EU.”


Imani Nsamila anaendelea kueleza kuwa mwananchi huyo alikuwa amepata ujuzi na elimu ya kilimo kutoka katika mradi huo na hivyo alianzisha shughuli za kilimo cha kutumia umwagiliaji ambacho ni sitahimilivu katika mabadiliko ya tabianchi.


“Kwa hivyo mimi nilipenda kwamba Dodoma ni sehemu kame, lakini kuna namna na kuna mbinu ambazo zinafanyika, wananchi wa Dodoma wanaweza wakafanya kilimo cha umwagiliaji na wakapata faida kwa hivyo huyu bwana alikuwa anafanya kilimo cha bustani, analima mbogamboga na mbogamboga zimembadilishia maisha kwa sababu ameongeza kipato na ameiweka hiyo fedha kwenye miradi mbalimbali.” Anaeleza Nsamila.


Aidha Nsamila anasema kilichomfurahisha pia kwa mkulima huyo ni msimamo wa mkulima huyo kuhusu usawa wa kijinsia kwani anao watoto wa kike na wa kiume lakini anasema anataka kutumia mapato kutoka kwenye kilimo hicho kuwasomesha watoto wake wote bila kujali jinsia.


Mpiga picha huyo amewashauri pia vijana wenzake kujituma na kujitolea kwani mafanikio yako mbele na kw hivyo wasitangulize kutaka kupata faida kabla ya kuwekekeza ujuzi, maarifa na hata ikiwezekana rasilimali kidogo walizonazo, “kwa mfano hata hii taarifa ambayo imenipa Ushindi, mimi niliwekeza pesa yangu mwenyewe. Niliamini kwamba ili nipate Ushindi lazima nifanye kitu tofauti. Lakini kitu tofauti hakikuwa karibu na mimi ninakoishi ambako ni Dar es Salaam. Kilikuwa Dodoma.” 


Tuzo na zawadi nyingine


Bada ya ushindi huu wa Tuzo ya vijana ya EU GCCA+ kwa ukanda wa Afrika Mashariki na kati, mbali ya fedha atakazopata, pia Imani Nsamila atapata mafunzo zaidi ya kuongeza maarifa ya upigaji picha za mazingira na mabadiliko ya tabianchi kutoka Climate Tracker ambao ni mtandao wa wanahabari unaoangazia masuala ya tabianchi duniani kote . Aidha ataongezewa nguvu ya kiuchumi ya kuboresha vifaa vyake vya kazi.