Lazima kuwe na uwajibikaji katika ukiukwaji mkubwa wa haki Tigray:OHCHR Ripoti

Mwanamke akiwa amemleta mtoto wake katika kituo cha afya huko Wajirat Kusini mwa Ethiopia kufanyiwa uchunguzi wa Utapiamlo
© UNICEF/Christine Nesbitt
Mwanamke akiwa amemleta mtoto wake katika kituo cha afya huko Wajirat Kusini mwa Ethiopia kufanyiwa uchunguzi wa Utapiamlo

Lazima kuwe na uwajibikaji katika ukiukwaji mkubwa wa haki Tigray:OHCHR Ripoti

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Utafiti wa Pamoja uliofanywa na tume ya haki za binadamu nchini Ethiopia (EHRC) na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) umebaini kwamba kuna sababu za msingi za kuamini kwamba pande zote katika mzozo wa Tigray nchini Ethiopia kwa kiasi fulani wamekiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu, sheria za ubinadamu na sheria za wakimbizi, ukiukwaji ambao unaweza kuwa ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Katika ripoti iliyochapishwa leo, ambayo inachunguza athari mbaya ambazo mzozo umekuwa nazo kwa raia, timu ya pamoja ya uchunguzi (JIT) imeelezea mfululizo wa vitendo vya ukiukwaji na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na mauaji ya  kinyume cha sheria na watu kunyongwa, mateso, unyanyasaji wa kingono na kijinsia, ukiukwaji wa haki dhidi ya wakimbizi, na kulazimisha  maelfu ya raia kukimbia makwao

Kuhusu ripoti

Ripoti hiyo inajumuisha kipindi cha kuanzia tarehe 3 Novemba 2020, wakati mzozo wa kivita ulipoanza kati ya jeshi la ulinzi la taifa la Ethiopia (ENDF), jeshi la ulinzi la Eritrea (EDF), kikosi maalum cha Amhara (ASF), Amhara Fano na wanamgambo wengine kwa upande mmoja , na kikosi maalum cha Tigray (TSF), wanamgambo wa Tigray na vikundi vingine washirika kwa upande mwingine, hadi tarehe 28 Juni 2021 wakati serikali ya Ethiopia ilipotangaza kusitisha mapigano.

Timu hiyo ya pamoja, JIT ilitembelea maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Mekelle, Mashariki mwa Tigray (Wukro), Kusini Mashariki mwa Tigray (Samre na maeneo ya karibu), Kusini mwa Tigray (Alamata, Bora na Maichew), Magharibi mwa Tigray (Dansha, Humera na Mai Kadra), na Bahir Dar na Gondar. katika eneo la Amhara, na katika mji mkuu Addis Ababa.  

JIT ilifanya mahojiano ya siri  na waathirika 269 na mashahidi wa madai ya ukiukaji na unyanyasaji, na vyanzo vingine na pia kufanya mikutano zaidi ya 60 na maafisa wa shirikisho la kikanda, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs, kamati za kijamii, wahudumu wa afya na vyanzo vingine.
Changamoto kubwa na uwajibikaji

Timu hiyo ya uchunguzi wa pamoja, JIT ilikabiliwa na changamoto kadhaa za kiusalama, kiutendaji na kiutawala katika kutekeleza kazi yake, hasa kushindwa kufanya ziara zote zilizopangwa katika sehemu za Tigray.  
Ripoti inawashukuru waathiriwa na mashahidi wengi walioshiriki uzoefu wao na inazishukuru taasisi za serikali ya Ethiopia na zisizo za kiserikali kwa ushirikiano wao.
"Wakati mzozo unavyoongezeka na ripoti zaidi za ukiukwaji na unyanyasaji, ripoti hii inatoa fursa kwa pande zote kukiri kuwajibika na kujitolea kuchukua hatua madhubuti za uwajibikaji, kushughulikia waathirika na kutafuta suluhisho endelevu kumaliza mateso kwa mamilioni ya raia," Amesema Daniel Bekele, kamishna mkuu wa baraza la haki za binadamu nchini Ethipia EHRC.  
Ameongeza kuwa "EHRC bado inajishughulisha na ufuatiliaji wa hali ya haki za binadamu tangu mwisho wa Juni na itatoa matokeo yake kwa wakati ufaao."  

Kwa upande wake Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema "Mgogoro wa Tigray unaambatana na ukatili wa kupindukia. Uzito na kiwango cha ukiukwaji  wa haki na unyanyasaji ambao tumeuorodhesha unasisitiza haja ya kuwawajibisha wahalifu waliohusika katika pande zote.” 

Ameongeza kuwa "Wakati mzozo umeongezeka, huku raia wakiwa wamejikuta katikati ya mzozo huo, ni muhimu kwamba pande zote zisikilize wito unaorudiwa wa kukomesha uhasama na kuhakikisha ni wa kudumu," Bachelet pia leo ametoa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya Tigray tangu tarehe ya mwisho ya ripoti ambayo ni mwezi Juni.

Chakula kimesambazwa kwa watu wa mkoa wa Afar nchini Ethiopia
© WFP/Claire Nevill
Chakula kimesambazwa kwa watu wa mkoa wa Afar nchini Ethiopia

Mambo yaliyobainiwa na JIT

Mashambulizi dhidi ya raia na mashambulizi ya kiholela: Kuna sababu za kuridhisha za kuamini wahusika wote katika mzozo huo ikiwa ni pamoja na vikosi vya ENDF, EDF na jeshi maalum la Tigraya ama walishambulia moja kwa moja raia na miundombinu ya kiraia, kama vile nyumba, shule, hospitali, na maeneo ya ibada, au vilifanya mashambulizi ya kiholela na kusababisha vifo vya raia na uharibifu au uharibifu wa miundombinu ya raia.

Mauaji na mauaji yasiyo ya halali au ya kiholela: JIT inahitimisha kuwa mauaji  haya yalifanywa na wanamgambo wa ENDF, EDF na Amhara, pamoja na TSF na wanamgambo wanaoshirikiana na jeshi la ukombozi la watu wa Tigray (TPLF).

Ripoti hiyo inaeleza jinsi tarehe 9 na 10 Novemba kundi la vijana la Tigray linalojulikana kama Samri lilivyowaua zaidi ya raia 200 wa kabila la Amhara huko Mai Kadra. Mauaji ya kulipiza kisasi yalifanywa huko Mai Kadra dhidi ya watu wa kabila la Tigraya baada ya ENDF na ASF kuuteka mji huo.  

Mnamo tarehe 28 Novemba, EDF iliua zaidi ya raia 100, wengi wao wakiwa vijana, huko Axum katikati mwa Tigray. "Uhalifu wa kivita unaweza kuwa umetendwa kwani kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba watu ambao hawakushiriki moja kwa moja katika uhasama waliuawa kwa makusudi na wahusika kwenye mzozo," ripoti hiyo inasema.  

Kwa kuongezea, mauaji katika baadhi ya matukio yanaonekana kufanywa kama sehemu ya mashambulio yaliyoenea ya kimfumo dhidi ya idadi fulani ya raia na kwa hivyo inaweza pia kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mateso: "Mateso na unyanyasaji wa raia na wapiganaji waliotekwa yamekuwa dhihirisho la ukatili ulioonyeshwa na pande zote wakati wa vita," ripoti hiyo inasema. Waathirika walipigwa kwa nyaya za umeme na mabomba ya chuma, waliwekwa kizuizini, kutishiwa kwa bunduki vichwani mwao na kunyimwa chakula au maji.

Kushikiliwa kiholela, utekaji nyara na kutoweshwa: Ripoti inasema ENDF iliwaweka kizuizini kiholela watu katika maeneo ya siri na kambi za kijeshi, katika visa vingi.

Vikosi vya Tigraya na vikundi vilivyoshirikiana nao viliwaweka kizuizini kiholela na kuwateka nyara raia wasio wa Tigray ambao baadhi yao waliuawa au kutoweka.

Uporaji na uharibifu wa mali: Kwa mujibu wa ripoti mgogoro huo umesababisha uharibifu mkubwa na upokonyaji wa mali kwa pande zote kwenye mzozo. Familia ambazo mazao na chakula vilichukuliwa zimelazimika kutegemea wanajamii na usaidizi wa kibinadamu ili kuishi. Uporaji wa vituo vya afya umesababisha raia kukosa huduma za afya. Wanafunzi kote Tigray wameona elimu yao ikikatizwa kwa sababu shule zao zilitumiwa kwa madhumuni ya kijeshi.

Unyanyasaji wa kingono na kijinsia: Kwa mujibu wa ripoti kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba wahusika wote kwenye mzozo huo walifanya unyanyasaji wa kingono na kijinsia, huku ENDF, EDF, na TSF wakihusishwa katika ripoti nyingi za ubakaji wa magenge.  
Katika visa vingi, ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono vilitumiwa “kuwaadhibu na kuwadhalilisha waathirika,” ripoti hiyo imesema.

Raia kuhamishwa kwa nguvu: Maelfu ya raia wamelazimika kukimbia kutokana na mauaji, ubakaji, uharibifu na uporaji wa mali, hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi, na kutokana na mashambulizi ya kikabila na vitambulisho, ambayo yalifanyika zaidi katika eneo la Tigray ya Magharibi.

JIT ina misingi ya kuridhisha ya kuamini kwamba watu kushinikizwa kuzikimbia nyumba zao kulifanywa kwa kiwango kikubwa na kinyume cha kisheria za kawaida za nchi na za kimataifa za kibinadamu.  
Vitendo kama hivyo vinaweza pia kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Wakimbizi:  Ripoti inasema kati ya Novemba 2020 na Januari 2021, TSF na EDF, walikiuka sheria za kiraia za kambi za wakimbizi huko Tigray kwa uwepo wao katika kambi ya wakimbizi ya Shimelba, ambayo inahifadhi wakimbizi wa Eritrea. TSF na EDF ziliweka usalama na maisha ya maelfu ya wakimbizi hatarini kwa kuendesha mapigano kuzunguka kambi, na kusababisha maelfu ya wakimbizi kuyahama makazi yao, kupotea kwa mamia ya wakimbizi, na kuharibiwa kwa kambi ya wakimbizi.

Mtaalamu wa Lishe wa UNICEF na Timu ya Kukabiliana na Dharura akiwaapima utapiamlo wananchi huko Adikeh huko Wajirat Kusini mwa Tigray nchini Ethiopia.
© UNICEF/Christine Nesbitt
Mtaalamu wa Lishe wa UNICEF na Timu ya Kukabiliana na Dharura akiwaapima utapiamlo wananchi huko Adikeh huko Wajirat Kusini mwa Tigray nchini Ethiopia.

Ukiukaji mwingine

Ripoti hiyo pia inaelezea athari zingine za mzozo kwenye baadhi ya haki za binadamu, zikijumuisha haki za Watoto, haki za wazee na watu wenye ulemavu, kunyimwa msaada wa msaada, kwa uhuru wa kutembea, pamoja na vikwazo vya uhuru wa kujieleza na kupata taarifa huku mitandao na njia nyingine za mawasiliano zikiwa zimekatwa kwa kiasi kikubwa.

"Kuzimwa kwa mawasiliano kumesababisha msongo wa mawazo na dhiki miongoni mwa raia huko Tigray, pamoja na familia na wapendwa wao ndani ya nchi na nje ya nchi," inasema ripoti hiyo.  
Kukamatwa na kutishwa kwa wanahabari kumetishia uhuru wa wa sauti za watu na kuleta athari ya kudhibiti kazi ya waandishi wa Habari.

Mapendekezo

Ripoti ya JIT inatoa mapendekezo ya kina. Mapendeko hayo ni pamoja na wito kwa pande zote kwenye mzozo kukomesha ukiukaji na unyanyasaji wote na kuchukua hatua zote muhimu kulinda raia na miundombinu ya kiraia.  

Inatoa wito kwao kukubaliana, bila masharti ukiukwaji wa haki, kukomesha mara moja uhasama na kukomesha hatua zozote zinazoweza kuzidisha mzozo mkubwa wa kibinadamu ambao tayari umekithiri.

Miongoni mwa mapendekezo yake kwa Serikali ya Ethiopia, JIT inataka uchunguzi wa haraka, wa kina na madhubuti wa vyombo huru na visivyopendelea upande wowote kuhusu madai ya ukiukaji  wa haki za binadamu na kuwawajibisha wale waliohusika.  

Uchunguzi na mashtaka ya kesi zote zilizoripotiwa za mauaji na unyongaji kinyume cha sheria au nje ya mahakama unapaswa kuwa kipaumbele, na waathiriwa na familia zao wahusishwe na kufahamishwa kikamilifu.

Serikali ya Eritrea inapaswa pia kufanya uchunguzi unaokidhi viwango vya kimataifa. Inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha vitendo vyote vya unyanyasaji vinavyofanywa na vikosi vyake dhidi ya raia vinakoma, huku ikiwaondoa kwenye majukumu ya kazi wale wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo wakati uchunguzi ukiendelea.  

Ripoti hiyo inaitaka Serikali ya Eritrea kuwaachilia mara moja wakimbizi wa Eritrea wanaozuiliwa nchini humo na kuhakikisha ulinzi na usalama wao, pamoja na haki yao ya kutafuta hifadhi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Pia kuna mapendekezo mengi kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa. Haya ni pamoja na kukuza na kuunga mkono juhudi zote za kukomesha uhasama na kufikia amani endelevu na shirikishi, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono hatua madhubuti za uwajibikaji.

Uwajibikaji

Ripoti hiyo inaelezea wito uliotolewa na waathirika na manusura kwa tume hiyo ya JIT kwa wahusika kufikishwa mahakamani.  

Wamewasilisha madai yenye nguvu ya kurejeshewa maisha yao na fidia kwa kile walichopoteza, na ukweli wa kile kilichotokea kwa wapendwa wao kuthibitishwa.

Hii inaweza kukusanya ushahidi juu ya ukiukaji mkubwa zaidi uliofanywa wakati wa mzozo na kuandaa mafaili kwa ajili ya mashtaka ya jinai kwa njia huru, ripoti inasema.