Tusaidie wanaopata madhara kutokana na dawa za kulevya: UNAIDS

1 Novemba 2021

Katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Watumiaji wa dawa za Kulevya, shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI UNAIDS linataka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya uhalifu wa watu wanaotumia dawa za kulevya, kuwasaidia wanaopata madhara yatokanayo na Virusi vya Ukimwi VVU, homa ya ini na masuala mengine ya afya, kwa ajili ya kuheshimu haki za binadamu na pia wameomba ufadhili zaidi wa programu za kupunguza madhara zinazoongozwa na jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima katika taarifa kwa waandishi wa habari kutoka Geneva nchini Uswisi amesema shirika lake limejitolea kusaidia nchi katika safari ya kukomesha umiliki wa madawa ya kulevya na kutekeleza kikamilifu mipango ya kupunguza madhara.

 "UNAIDS inataka ushiriki kamili wa jumuiya za watu wanaotumia madawa ya kulevya katika kufikia mageuzi ya kisheria yenye lengo la kuondoa uhalifu na kuandaa programu za kupunguza madhara katika ngazi ya nchi. Hii itatusaidia kukomesha ukosefu wa usawa na kumaliza UKIMWI.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNAIDS ameongeza kuwa “Watu wanaotumia na kujidunga madawa ya kulevya ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kupata VVU lakini wanabakia kutengwa na mara nyingi wamezuiwa kupata huduma za afya na kijamii.”

Ameeleza kuanzishwa kwa wakati na utekelezaji kamili wa mipango ya kupunguza madhara inaweza kuzuia maambukizi ya VVU, pamoja na matukio mengi ya virusi vya hepatitis B na C, kifua kikuu na overdose ya madawa ya kulevya.

Akisoma takwimu amesema mnamo 2020, asilimia 9 ya maambukizo yote mapya ya VVU yalikuwa miongoni mwa watu wanaojidunga dawa za kulevya. Nje ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara takwimu zinaonesha ongezeko hadi asilimia 20.

Ingawa wanawake wanawakilisha chini ya asilimia 30 ya idadi ya watu wanaotumia madawa ya kulevya, wanawake wanaotumia madawa ya kulevya wana uwezekano mkubwa wa kuishi na VVU kuliko wenzao wa kiume.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter