Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP26: Jamii ndogo zina mchango mkubwa katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:Rahma Kivugo

Mikoko baharini
Maktaba
Mikoko baharini

COP26: Jamii ndogo zina mchango mkubwa katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:Rahma Kivugo

Tabianchi na mazingira

Jamii ndogo ndogo za mashinani zina mchango mkubwa katika kusongesha ajenda ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi amesema mmoja wa wanaharakatio wa mazingira Rahma Rashid Kivugo mratibu wa mradi wa kijamii wa Mikoko Pamoja kutoka Pwani ya Kenya.

Akiwa ni miongoni mwa washiriki wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi au COP26 unaoendelea mjini Glasgow Scotland Bi.Kivugo ameiambia Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kwamba huo ndio ujumbe alioubeba kutoka kwa wnamradi wa vitongoji vya Gazi Bay na Makongeni

“Ujumbe niliokuja nao kwenye mkutano huu ni kwamba jamii ndogo za asili zinachangia pakubwa katika uhifadhi wa mazingira hususan katika upunguzaji wa hewa chafu katika mazingira yetu. Kama mwana jamii nimekuja hapa kuwakilisha jamii yangu ili niweze kuonyesha kuwa hata zile jamii ndogondogo ziko na uwezo mkubwa katika kusuluhisha hili tatizo kubwa la mabadiliko ya tabnianchi.”

Kivugo akaenda mbali zaidi na kufafanua jinsi wanavyochangia kupunguza hewa ukaa katika mradi wao “Kile kitu tunafanya kama mradi wa mikoko pamoja ni kusafisha hewa yetu kutumia miti ile tuliyonayo, kupitia unyonyaji wa hewa kutoka kwa mazingira kama hewa ukaa na nyinginezo ambazo si nzuri kwa wanadamu na mazingira. Kupitia miti tunayopanda ya mikoko katika ile hali yake ya kuvyonja hewa ukaa ili ijipatie chakula ndio tunapopunguza hewa hiyo angani. Tunapima urefu na upana wa miti na tunajua kwa kiasi gani hewa hiyo imevyonzwa nah apo ndipo nchi ambazio zimechafua zaidi mazingira au wadai wa kuchangia vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi hutulipa kwa kupunguza hewa hiyo kupitia mikoko ambayo huvyonza hewa ukaa mara sita au mara kumi zaidi ya miti mingine.”

COP26 inahimiza ushirikishwaji wa vijana katika vita hii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kama kijana Rahma Kivugo anasema wito umeitikiwa na vijana wanashiriki miradi mbalimbali lakini ombi lake kwa viongozi wanaoshiriki mkutano huo ni moja”Chenye ningependa kuona ni kuwa chochote kitakachoongelewa hata kama si mapendekezo makubwa sana , ni kuhiza kuwa hata kile kidogo mtu anachoweza kuchangia ni muhimu sana. Na kwa nchi au mataifa yaliyoendelea yawasaidie nchi masikini kwani hawahusiki pakubwa kuchafua mazingira lakini ndio wanaobeba gharama za athari zake. Na nchi hizo zijifunze kupitia miradi midogo kama mikoko pamoja katika kudhibiti janga hili.”

Na kwa serikali ya Kenya atokako ana wito “Ningependa serikali yetu iweze kutuunga mkono katika jitihada zetu maanake ukiangalia kuna miradi mingi ya mazingira na inayojitokeza lakini usaidizi hakuna u ni mdogo sana. Na kama serikali inaweza kutuunga mkono na ikatuonyesha ni wapi pa kuelekea huo utakuwa muongozo wetu katika kutuhamasisha na kujiendeleza katika juhudi hizi hivyo ingekuwa vizuri sana.”
Na hakuwasahau vijana wenzie “ Kwa vijana wenzangu nawaambia kila kitu kinatokana na hamasa na ari uliyonayo, kama mimi nisingeweza kufikia hapa bila ari ya kuipenda kazi yangu, hivyo vijana wasijishushe  wala kujidharau, chochote ulichonacho kama una nia utafanikiwa, Mwanzo mgumu na changamoto sipo lakini cha msingi kutokata tamaa.”