Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunapimwa kwa vitendo vyetu na si kwa ahadi kubwa kubwa- Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia mjadala wa viongozi kuhusu mshikamano kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow, Scotland
UN WebTV Video
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia mjadala wa viongozi kuhusu mshikamano kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow, Scotland

Tunapimwa kwa vitendo vyetu na si kwa ahadi kubwa kubwa- Rais Samia

Tabianchi na mazingira

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezungumza katika mjadala wa wazi wa viongozi kwenye mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, CO26 huko Glasgow, Scotland na kusema mshikamano na juhudi zao kama viongozi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi vitapimwa si kwa ahadi kubwa wanazotoa kwenye mkutano huo bali kwa jinsi wanatekeleza vipengele vyote vya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.
 

Ametaja vipengele hivyo kuwa ni pamoja na kupunguza makali ya mabadiliko ya tabianchi, kuhimili mabadiliko hayo sambamba na uchangiaji wa fedha kulingana na kiwango cha changamoto zilizoko hivi sasa.

Tweet URL

Rais Samia amesema, “mabadiliko ya tabianchi ni suala la dunia nzima na hivyo majawabu yake ni lazima yawe ya kimataifa na hivyo tunatoa wito kwa nchi zilizoendelea ambazo ndio zinaongoza kwa uchafuzi zitekeleze kwa vitendo ahadi zao za kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fedha za kutosha kutuwezesha sisi nchi za kipato cha chini kufanikisha malengo yetu kwenye michango ya kitaifa ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa uendelevu.”

Amesisitiza kuwa fedha za kutosha hususan kupitia misaada ya fedha itakuwa ni msingi katika mikakati yetu ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Amesema nchi yake ya Tanzania na nyingine za kipato cha chini zimeandaa mipango ya kina ya NDCs ikiwa na mikakati dhahiri ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

“Mipango yetu ni mtambuka katika sekta zote muhimu lakini hatuwezi kufanikisha bila usaidizi wa kutosha na teknolojia inayotakiwa ili kujenga uwezo wetu. Waheshimiwa kama hatutachukua hatua sasa tena kwa mshikamano, lengo la kuwa na kiwango cha joto katika nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi litatoweka punde na hatutalifikia.”