Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 5 wameaga dunia kwa COVID-19 , usawa wa chanjo utawaenzi: Guterres

Idadi wa wagonjwa wa COVID-19 imeendelea kupungua barani Afrika, ikiwemo nchini Rwanda
WHO
Idadi wa wagonjwa wa COVID-19 imeendelea kupungua barani Afrika, ikiwemo nchini Rwanda

Watu milioni 5 wameaga dunia kwa COVID-19 , usawa wa chanjo utawaenzi: Guterres

Afya

Wakati dunia Jumatatu ya leo Novemba Mosi ikitafakari machungu ya COVID-19 kwa kupoteza maisha ya watu milioni 5, Katibu Mkuu António Guterres ametoa wito kwa viongozi wa kimataifa kuunga mkono mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kufanya usawa wa chanjo kuwa hali halisi kwa kuharakisha na kuongeza juhudi na kuhakikisha umakini wa hali ya juu ili kuvishinda virusi hivi.

Katika taarifa iliyotolewa kuashiria kuvuka kwa "kizingiti hiki cha uchungu mkubwa ", Guterres amesema "hatua hii mbaya inatukumbusha kwamba tunaiangusha sehemu kubwa ya dunia. Wakati nchi tajiri zikitoa dozi ya tatu ya chanjo ya COVID-19, ni takriban asilimia tano tu ya watu barani Afrika ndio wamepata chanjo kikamilifu.”

Aibu ya kimataifa

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yake amesema "Hii ni aibu ya kimataifa. Vifo milioni tano pia vinapaswa kuwa onyo la wazi kwamba hatuwezi kujisahau, "Bwana Guterres amesema, akielezea kwambadunia bado inashuhudia vifo vingi, hospitali zilizojaa na wafanyikazi wa afya waliochoka, pamoja na hatari mpya ya kuenea kwa ugonjwa huo na kukatili maisha zaidi.

Wakati huo huo, amebainisha kuwa vitisho vingine hatari vinaendelea kuruhusu COVID-19 kusshamiri  ikiwemo habari potofu, uhifadhi wa chanjo na utaifa na ubinafsi wa chanjo, na ukosefu wa mshikamano wa kimataifa.

Usawa wa chanjo unaweza kudhibiti virusi

"Ninawaomba viongozi wa dunia kuunga mkono kikamilifu mkakati wa kimataifa wa chanjo niliouzindua na shirika la afya duniani (WHO) mwezi uliopita," amesisistiza Katibu Mkuu, na kuongeza kuwa "Tunahitaji kuwachanja  asilimia 40 ya watu katika nchi zote ifikapo mwisho wa mwaka huu, na asilimia 70 ifikapo katikati ya 2022.”

Pia ametoa wito kwa viongozi wa dunia kutekeleza kwa uharaka na kwa kiwango cha juu, pia kushughulikia mapungufu ya ufadhili na kuratibu hatua zao kwa ajili ya mafanikio ya mkakati huo.

Linganisha chanjo kwa uangalifu

Bwana Guterres amesema kuwa itakuwa makosa kufikiria kuwa janga hilo limeisha. Vizuizi vinapopungua katika maeneo mengi, "lazima pia tulinganishe chanjo kwa uangalifu  ikijumuisha kupitia hatua mahiri na zilizothibitishwa za afya ya umma kama vile kuvaa barakoa na kuzingatia umbali baina ya mt una mtu katika kijamii."

"Njia bora ya kuwaenzi wale watu milioni tano waliopotea na kusaidia wafanyikazi wa afya wanaopambana na virusi hivi kila siku ni kufanya usawa wa chanjo kuwa kutimia kwa kuharakisha juhudi zetu na kuhakikisha umakini wa hali ya juu katika kuvishinda virusi hivi," amehitimisha Guterres.