Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita Sudan Kusini havijakatili maisha na kutawanya watu tu, pia vimewatowesha wengi:UNMISS

Machafuko yamesababisha watu kukimbia maeneo ya vijijini karibu na Yei jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Machafuko yamesababisha watu kukimbia maeneo ya vijijini karibu na Yei jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.

Vita Sudan Kusini havijakatili maisha na kutawanya watu tu, pia vimewatowesha wengi:UNMISS

Amani na Usalama

Vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa nchini Sudan Kusini vimeambatana na athari nyingi, mbali ya kukatili maisha ya maelfu ya watu, kuwatawanya mamilioni sasa watu wengi wanawasaka ndugu zao kwa udi na uvumba kwani hawajulikani waliko, wametekwa ama wametoweka kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS.

“Ilikuwa giza totoro nilipotekwa na watu wenye silaha tulifungiwa kwenye chumba na kufungwa kamba, tulikuwa wawili na wakatuambia leo ndio siku yenu ya mwisho hapa duniani hivyo tuwe tayari kufa”

Huyo ni Mario Michael mmoja wa watu waliotekwa nyara mjini Tambura kwenye jimbo la Equatorial Magharibi Sudan Kusini, ana bahati kwani kwa jitihada za UNMISS aliachiliwa sababu mapigano yanayoendelea eneo hilo yameziacha familia nyingi na majonzi sio tu ya kupoteza ndugu zao waliouawa bali waliotoweka bila kujua hatma yao.

Kwa sasa UNMISS imeweka makazi ya muda kwa maelfu ya wakimbizi wa ndani hapa kwa lengo la kurejesha utulivu na kupunguza mvutano, lakini uharibifu mkubwa wa mali na kuvurugika kwa mfumo wa mawasiliano inamaanisha wanajamii wana fursa ndogo sana ya kuwasiliana na jamaa zao waliotoweka.

Na usalama mdogo nao unachangia kupoteza kabisa matumaini ya jamii hizi kuwatafuta ndugu zao wao wenyewe .

Shukran kwa juhudi kubwa zinazofanywa na UNMISS na wadau kwani sasa baadhi ya watu waliotekwa kama Mario  wameachiliwa.

Na ili kuzuia wakimbizi wengi zaidi wa ndani wasitekwe wakienda kusaka chakula au kuchota maji UNMISS imezidisha doria eneo hili. Na kwa wale walionusurika na kuachiliwa kama Baptistor John wanamshukuru Mungu kwani anasema walipotekwa hakutarajia kurejea salama, waliteswa na hawakupewa chakula kwa siku mbili na iku ya tatu ndio walipewa chakula na maji kidogo.

Hata hivyo licha ya juhudi za UNMISS na wadau hali bado ni tete tambura na wazazi wanaishi kwa hofu kubwa ya watoto wao kutekwa,

Madelina Michael ni mama ambaye mwanaye alitekwa “Wakati mwanangu alipotekwa na watu wenye silaha sikufikiria nitakuja kumuona tena, kwani nilijua ameshauawa kwa sababu hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kurejea akiwa hai. Nilianza kumuomboleza na kuomba kwa ajili ya usalama wake popote alikokuwa.”

Kwa sasa UNMISS inashirikisha wadau mbalimbali kuweza kudhibiti athari za machafuko yanayoendelea Tambura na kuweza kuwalinda raia.