Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakuu wa G-20 onyesheni uongozi kuokoa maisha:Guterres

Viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani wanahudhuria mkutano wa G20 unaofanyika Roma Italia 30 Oktoba 2021
G20 Summit/Italy
Viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani wanahudhuria mkutano wa G20 unaofanyika Roma Italia 30 Oktoba 2021

Wakuu wa G-20 onyesheni uongozi kuokoa maisha:Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amehudhuria ufunzi rasmi wa mkutano wa viongozi wa mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi duniani G-20 .

Akizungumza katika kikao kilichopewa jina “Uchumi wa dunia na afya ya dunia” Guterres amewasihi wakuu wa mataifa hayo 20 kuonyesha uongozi shupavu ili kuokoa maisha, kuzuia madhila zaidi na kuwezesha dunia kujikwamua kikamilifu kutoka kwenye janga la COVID-19.

Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa G20 kupitisha na kuratibu hatua za kusaidia mpango wa chanjo wa WHO

Amesema “Mpango huo unalenga kuchanja asilimia 40 ya watu katika nchi zote ifikapo mwisho wa mwaka huu na asilimia 70 ifikapo katikati ya 2022.” 

Zaidi ya hayo, amewahimiza viongozi kuangalia jinsi tunavyoweza, wakati huo huo kufufua upya uchumi wa dunia wakati wa kupigana na ukosefu wa usawa, pamoja na kurejesha uaminifu kati ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea.

Kandoni mwa mkutano huo Katibu Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na viongozi mbalimbali wa dunia katika majadiliano yasiyo rasmi.

Pia Guterres amefanya mkutano na Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

 Na kabla ya kuungana na viongozi wa G20 kushiriki mlo rasmi wa jioni ulioandaliwa na Rais wa Italia Sergio Matterella, Katibu Mkuu amekutana na viongozi wa jamii ya San’Egidio na kuwashukuru kwa kazi kubwa ya upatanishi wanayoifanya katika sehemu mbalimbali duniani.