Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kwanza la aina yake kulinda madarasa katika mizozo

Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa  mjini Idlib Syria.
UNICEF
Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa mjini Idlib Syria.

Baraza la Usalama lapitisha azimio la kwanza la aina yake kulinda madarasa katika mizozo

Amani na Usalama

Kwa kauli moja siku ya Ijumaa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kipekee la kulaani vikali mashambulizi dhidi ya shule, watoto na walimu na kuzitaka pande zinazozozana kulinda mara moja haki ya elimu.

Wakati Baraza hilo lenye wanachama 15 limetoa taarifa za awali za kulaani mashambulizi dhidi ya shule, hili ni azimio lake la kwanza kuangazia kwa kina na uwazi uhusiano kati ya elimu na amani na usalama.

Jukumu la thamani ala elimu

Kupitia azimio namba 2601 la mwaka (2021), wajumbe wamesisitiza jukumu muhimu la elimu kwa watu binafsi na jamii, likiijumuisha kama maeneo salama ya kuokoa maisha. 

Wajumbe wamebainisha kuwa kutoa, kulinda na kuwezesha kuendelea kwa elimu katika  maeneo ya vita vya silaha, kunapaswa kusalia kuwa kipaumbele muhimu kwa jumuiya ya kimataifa.

Baraza pia limezitaka nchi kuendeleza mifumo ya kisheria ya ndani ili kuhakikisha kuheshimiwa kwa wajibu wao wa kisheria wa kimataifa ikiwa ni pamoja na hatua za kina za kuzuia mashambulizi dhidi ya shule, watoto, walimu na raia wengine wanaohusiana na elimu.

Miongoni mwa vipengele vingine vya kifungu hicho, wajumbe wameomba kuanzishwa kwa mikakati na taratibu za uratibu wa kubadilishana taarifa kuhusu ulinzi wa shule na elimu, miongoni mwa mataifa, ofisi ya mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa kwa ajili ya watoto na migogoro ya kivita, na operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani na ujumbe wa kisiasa.

Kuongezeka kwa mashambulizi

Suala la elimu katika mazingira ya migogoro limepata umaarufu katika Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa kwa katika miaka ya hivi karibuni, huku mashambulizi mabaya dhidi ya shule na raia wanaohusiana nayo yakiongezeka duniani kote.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya wanafunzi 22,000, walimu na wanazuoni walijeruhiwa, kuuawa au kulemazwa katika mashambulizi dhidi ya maeneo ya elimu wakati wa vita au ukosefu wa usalama katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ripoti ya Katibu Mkuu ya mwaka 2020 na 2021 kuhusu watoto na migogoro ya kivita pia iliangazia ongezeko la mashambulizi dhidi ya shule.

Tarehe 10 Septemba 2020, ujumbe wa Niger uliitisha mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama kuhusu mashambulizi dhidi ya shule, ambapo wajumbe walipitisha taarifa ya rais inayothibitisha haki ya elimu na mchango wake kwa amani na usalama. 

Pia ilitoa wito kwa nchi kuchukua hatua kuzuia mashambulizi na vitisho vya mashambulizi dhidi ya shule.

Azimio la kwanza na la aina yake

Wajumbe wa Baraza, wakizungumza baada ya kura ya Ijumaa, wamekaribisha kwa kupitishwa kwa azimio hilo, ambalo ni la kwanza lililowekwa maalum kwa ulinzi wa madarasa na shule.

Mwakilishi wa Norway mmoja kati ya wawezeshaji wa azimio hilo, pamoja na mwakilishi wa Niger walisema maandishi hayo yatasaidia Baraza kutoa sauti yake dhidi ya kuongezeka kwa usumbufu wa elimu katika migogoro. 

Alibainisha kuwa shule, walimu au wanafunzi walishambuliwa katika nchi 93 kati ya mwaka 2014 na 2019.

Mjumbe wa Niger aliongeza kuwa zaidi ya watoto milioni 75 duniani kote wameona elimu yao ikivurugwa na migogoro, huku mashambulizi dhidi ya shule na miundombinu ya shule yakiongezeka kwa kiwano cha kutisha.