Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usanifu majengo ni msingi wa mnepo wa majengo mijini

Nyumba za kuhimili vimbunga huko nchini Ufulipino
Rappler.com
Nyumba za kuhimili vimbunga huko nchini Ufulipino

Usanifu majengo ni msingi wa mnepo wa majengo mijini

Tabianchi na mazingira

Tarehe 31 ya mwezi Oktoba kila mwaka ni siku ya majiji na miji duniani ambapo kwa mwaka huu maudhui ni Kuwezesha miji kuwa na mnepo kwa tabianchi. Maudhui haya yamekuja wakati ambapo miji inapaswa kuwa na mnepo kuliko wakati wowote ule.
 

 

Jengo hili pindi mvua ikija na mafuriko linaelea. Jengo liko nchini Bangladesh
Giant Grass
Jengo hili pindi mvua ikija na mafuriko linaelea. Jengo liko nchini Bangladesh

Miji hiyo hiyo hivi sasa imekuwa kitovu cha janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 na wakati huo huo inakabiliana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.

Duniani kote, zaidi ya watu bilioni 1 wanaishi katika makazi yasiyo rasmi ambapo asilimia 70 wako katika hatari ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi iwe ni mafuriko, vimbunga, dhoruba, joto kali na ongezeko la kina cha maji ya bahari.

Hivi karibuni shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEP katika ripoti lilisisitiza mchango wa majengo katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Usanifu majengo ni zaidi ya uchoraji wa ramani

Hata hivyo Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, UN News ilitaka kwenda mbali zaidi kuona uhalisia wa kauli hiyo na ikazungumza na msanifu majengo Shabani Mwatawala ambaye alikiri kuwa “suala la ujenzi wa nyumba zinazohimili mabadiliko ya tabianchi linaanza na wasanifu majengo kwa sababu wasanifu majengo ndio wamebeba dhamana ya kutayarisha miongozo ambayo inakuwa katika njia ya michoro kwa ajili ya ujenzi wa majengo yoyote, achilia mbali haya tunayozungumza kuwa yana umuhimu wake katika uhimili wa mabadiliko ya tabianchi. Kwa hivyo wanapokuwa wamefanya kazi yao vizuri, wanakuwa wamewatengenezea wateja wao au wananchi kiujumla, makazi ambayo yanaweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi.”

Amesema usanifu majengo unaanzia mwanzoni mtu anapotaka kufanya usanifu akiangalia eneo ambalo linasanifiwa jengo liko mahali gani, na mahali hapo pana hali gani kitabianchi mfano mvua zinanyeshwa kwa kiasi gani, upepo unavuma kwenda upande gani na jengo lenyewe linatazama jua linachomoza na kuzama upande gani ili vitu hivyo vinapotokea watu wawe wanakingwa na vitu hivyo.

Mtaalamu huyo amesema “kama nyumba inaangalia mashariki ina maana jua lote la asubuhi linaingia ndani na kama nyumba inaangalia magharibi, jua lote la mchana linaingia ndani. Na hii kama ni jua kali na inabidi kutumia viyoyozi basi utatumia nishati nyingi ya umeme na hii inasababisha hasara ya kiuchumi.”
Na iwapo mtu hakuzingatia eneo la mafuriko, Bwana Mwatawala amesema mafuriko yakitokea atapoteza mali kwani maji yataingia ndani ya nyumba na jengo kudondoka. 

Msanifu huyo wa majengo amezungumzia nyumba zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi akitolea mfano Thailand ambako nyumba zinainuliwa juu halikadhalika Nigeria, hata mafuriko yakitokea maji hayaingii ndani.

Uwekaji wa mabomba ya kuvuna mvua kutoka kwenye paa za nyumba nchini Tanzania.
UNEP
Uwekaji wa mabomba ya kuvuna mvua kutoka kwenye paa za nyumba nchini Tanzania.

Kuna udongo mahsusi wa kujenga nyumba kuzuia joto

Kwenye maeneo ya joto ametolea mfano maeneo ya Afrika ya Kaskazini ambako wanatumia udongo unaozuia joto au baridi kupenya ndani.

Kwa upande wa maeneo yenye upepo, mtaalamu amesema nyumba zinajengwa kwa mfano wa duara au bakuli na hivyo upepo hauna fursa ya kujikinga mahali na kuezua paa, na kusema nyumba hizo zinapatikana maeneo yenye upepo.

Kuhusu vifaa amesema vinaweza kufanana lakini utumiaji wake unatofautiana akitolea mfano mabati. “unaweza kutumia mabati kuezeka sehemu yenye joto lakini kwenye dari kuna vifaa unaweka ili kuzuia joto kupenda ndani.”

Shule ilioko mkoa wa Bujumbura vijijini ambapo mafuriko yamekatiza shughuli za masomo.
IOM 2021/Triffin Ntore
Shule ilioko mkoa wa Bujumbura vijijini ambapo mafuriko yamekatiza shughuli za masomo.

Bwana Mwatawala amesema pamoja na kwamba wasanifu majengo wana jukumu kubwa la kuzingatia usanifu wa majengo na kueliemisha jamii, sheria thabiti ni muhimu ili kusimamia. “Katika nchi nyingi kuna sheria za majenzi ambazo zinakuwa zinazuia ukiukwaji wa ujenzi holela. Sheria zikiwepo lile suala la kwamba ni fedha zangu naweza kujenga chochote halitakuwepo.”