Ni wakati wa kuchukua hatua haraka kwa ajili ya maji na mabadiliko ya tabianchi

29 Oktoba 2021

Mkuu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO na mashirika mengine tisa ya kimataifa yametoa wito wa pamoja na wa dharura kwa serikali kuweka kipaumbele kwa hatua jumuishi za maji na mabadiliko ya tabianchi kutokana na athari zinazoenea za masuala hayo kwa maendeleo endelevu.

"Hatua za haraka zinahitajika kwa dharura kushughulikia matokeo yanayohusiana na maji na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri watu na sayari," inasema barua iliyotolewa kwa pamoja na wakuu wa nchi na serikali ambayo imetolewa kuelekea mkesha wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi , COP26.

Viongozi wa muungano wa maji na hali ya hewa watakuwa katika mkutano wa COP26 kutanabaisha udharura wa changamoto hizo.

Barua hiyo inazitaka serikali kushughulikia kwa ufanisi zaidi vipimo vya maji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga mnepo, kama ilivyoelezwa katika mfumo uliokubaliwa na Umoja wa Mataifa ili kuharakisha maendeleo kufikia lengo la 6 la maendeleo endelevu SDG’s la kuhakikisha upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote.

Barua hiyo imetiwa saini na wakuu wa WMO, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), shirika la afya duniani (WHO), mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo. IFAD), shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP),shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), chuo kikuu cha Umoja wa Mataifa (UNU), Tume ya Umoja wa Mataifa ya kiuchumi kwa ajili ya Ulaya (UNECE) na Ushirikiano wa kimataifa wa maji (GWP).

Madadiliko ya tabianchi yanaathiri mzunguko wa maji

"Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kwa kiasi kikubwa mzunguko wa maji, na kufanya mara kwa mara ukame na mafuriko kuwa mbaya zaidi na kupunguza hifadhi ya asili ya maji katika barafu na theluji. Kuongezeka kwa joto na kutofautiana kwa mifumo ya mtiririko wa maji, pia huathiri sana ubora wa maji katika ardhini na chini ya ardhi” imesema barua hiyo.

Barua hiyo ikaenda mbali zaidi na kusema "Kubadilika kwa mifumo ya mvua tayari kunaathiri kilimo, mifumo ya chakula, na maisha yanazidi kuwa hatarini, pamoja na mifumo ya ikolojia, na bayoanuwai. Kupanda kwa kina cha bahari kunatishia jamii, miundombinu, mazingira ya pwani na vyanzo vya maji.”

Imeongeza kuwa "Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya UNICEF kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto, zaidi ya theluthi moja ya watoto duniani sawa na watoto milioni 920 kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa maji.” 

Zaidi ya hayo, ripoti ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo ya maji duniani ya mwaka 2020, inasisitiza kuwa maji ni "kiunganishi cha hali ya hewa" kinachoruhusu ushirikiano na uratibu zaidi katika malengo mengi ya mabadiliko ya tabianchi yaliyowekwa kwenye Mkataba wa Paris, malengo ya maendeleo endelevu (Ajenda ya 2030 na SDGs), na kupunguza hatari ya maafa (Mkataba wa Sendai.)

Orodha ya vipaumbele kwa serikali

Baria hiyo imeorodhesha idadi ya vipaumbele vya haraka kwa viongozi wa serikali vikiwa ni pamoja na

  • Kuunganisha ajenda za maji na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya kitaifa kupitia mpango wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko na ustahimilivu na katika ngazi ya kikanda, kupitia ushirikiano wa kimataifa;
  • Kukuza na kufadhili mifumo ya kimataifa ya ufuatiliaji wa maji ili kutoa ujuzi kwa wakati kuhusu upatikanaji wa maji wa sasa na wa siku zijazo na viwango vya ubora katika ngazi za kimataifa, kikanda na ya mitaa;
  • Kusaidia ushirikiano wa kiufundi, kisiasa na kisayansi katikamaeneo ya mabonde, kikanda na kimataifa
  • Kuhimiza upatikanaji wa tahadhari ya mapema kwa wakati unaofaa kuhusu majanga yanayohusiana na maji ili kusaidia kuokoa maisha na kulinda maisha.
  • Kuhusisha masuala ya maji katika michango ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (NDC) 
  • Kuchagiza mbinu madhubuti za kudhibiti mafuriko na ukame kwa kuzingatia nguzo tatu: ufuatiliaji, utabiri na tahadhari ya mapema; hatari na tathmini ya athari; na kujiandaa, kupunguza na kukabiliana;
  • Kusaidia ujumuishaji wa takwimu na makadirio juu ya hatari za mabadiliko ya tabianchi na maji katika uundaji wa miundombinu inayostahimili, ikijumuisha huduma za maji na usafi wa mazingira, haswa kwa walio hatarini zaidi.

"Mfumo wa Umoja wa Mataifa, ukijihusisha kwa njia iliyoratibiwa katika miongo kadhaa ya hatua za maji na hatua za SDGs, na mfumo wa kuongeza kasi ya kimataifa ya kufikia  SDG 6, uko tayari kusaidia nchi yako katika kuhakikisha kuwa mabadiliko ya tabianchi na maji vinaenda sambamba," umehitimisha wito huo wa pamoja.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter