Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chini ya 10% ya nchi za Afrika ndizo zitakazofikia lengo la chanjo ya COVID-19:WHO

Kituo cha kupima COVID-19 jimboni Ogun, kusini-magharibi mwa Nigeria
WHO
Kituo cha kupima COVID-19 jimboni Ogun, kusini-magharibi mwa Nigeria

Chini ya 10% ya nchi za Afrika ndizo zitakazofikia lengo la chanjo ya COVID-19:WHO

Afya

Nchi tano tu za Kiafrika, ambazo ni chini ya asilimia 10% ya mataifa  yote 54 ya bara hilo , ndio zinakadiriwa kufikia lengo la mwisho wa mwaka la chanjo kamili ya COVID-19 kwa asilimia 40% ya watu wao, endapo hakutochukuliwa hatua madhuburi za kuharakisha kasi ya mchakato wa chanjo, limesema leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO.

Haya yanajiri huku ukanda huo ukikabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya bidhaa muhimu za chanjo, kama vile sindano.

Nchi tatu za Afrika, Ushelisheli, Mauritius na Morocco, tayari zimefikia lengo lililowekwa mwezi Mei na Baraza  la Afya Duniani WHA, chombo cha juu zaidi cha kuweka sera za afya duniani.

Kwa kasi ya sasa ni nchi mbili tu zaidi, Tunisia na Cabo Verde, ndio pia zitafikia lengo hilo.

Kwa kuongezea, WHO inasema upatikanaji mdogo wa bidhaa muhimu kama vile mabomba ya sindano unaweza kupunguza kasi ya utoaji wa chanjo za coronavirus">COVID-19 barani Afrika. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeripoti upungufu unaokaribia hadi mabomba ya sindano bilioni 2.2 kwa ajili ya kutumika kwa chanjo ya coronavirus">COVID-19 na chanjo ya kawaida kwa mwaka wa 2022.

Hii ni pamoja na sindano za ujazo wa 0.3ml zinazotumika kwa ajili ya chanjo ya Pfizer-BioNTech COVID-19.

Hakuna akiba ya mabomba ya ujazo wa 0.3ml

WHO inasema hakuna hifadhi ya kimataifa ya sindano maalum za ujazo wa 0.3ml, ambazo ni tofauti na sindano za ujazo wa 0.5ml zinazotumiwa kwa aina zingine za chanjo za COVID-19 na chanjo ya kawaida.  
Soko la sindano za ujazo wa 0.3ml ni gumu na lina ushindani mkubwa. Kwa hivyo, hizi zina upungufu na zitabaki hivyo katika angalau robo ya kwanza ya mwaka ujao.

Tayari baadhi ya nchi za Afrika, kama vile Kenya, Rwanda na Afrika Kusini, zimekabiliwa na ucheleweshaji wa kupokea mabomba ya sindano hizo.

"Tishio linalokuja la shida ya bidhaa za chanjo liko katika bara zima. Mapema mwaka ujao chanjo za COVID-19 zitaanza kumiminika barani Afrika, lakini uhaba wa mabomba ya sindano unaweza kuathiri hatua zilizopigwa. Hatua kali lazima zichukuliwe ili kuongeza uzalishaji wa mabomba ya sindano haraka. Maisha yasiyohesabika ya Waafrika yanategemea mabomba hayo,” amesema Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.

Jukwaa la kimataifa la kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo, COVAX kinafanya kazi kushughulikia tishio hili kwa kupata mikataba na watengenezaji wa mabomba ya sindano,kwa kupitia mipango bora ili kuzuia uwasilishaji unaopita usambazaji wa mambomba ya sindano.

Dozi za chanjo zilizowasili Afrika

Kwa mujibu wa WHO kuanzia mwanzo wa mwezi Oktoba hadi sasa, karibu dozi milioni 50 za chanjo ya COVID-19 zimewasili barani Afrika, ambayo ni karibu mara mbili ya ile iliyosafirishwa mwezi Septemba.

COVAX, jukwaa la kimataifa la kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo, limetoa karibu asilimia 90 ya chanjo zilizotumwa mwezi huu na limeongeza kasi ya usafirishaji wake tangu Julai.

Hata hivyo, kwa kasi ya sasa, Afrika bado inakabiliwa na upungufu wa dozi milioni 275 za chanjo za COVID-19 ili kufikia lengo la mwisho wa mwaka la kuwapa chanjo kamili  asilimia 40% ya watu wake.

Afrika imeshawapa chanjo kamili watu milioni 77, ambayo ni asilimia 6 tu ya wakazi wake wote ulinganisha, na zaidi ya asilimia 70% ya nchi zenye kipato cha juu ambazo tayari zimechanja zaidi ya  asilimia 40% ya watu wake.

WHO inasema nchi bado zinahitaji kuboresha utayari wao wa kusambaza chanjo ya COVID-19.  

Asilimia 42 ya nchi katika Kanda ya Afrika bado hazijakamilisha mipango ya ngazi ya wilaya kwa ajili ya kampeni zao, wakati karibu asilimia 40% bado hazijafanya mapitio ya ndani ambayo ni muhimu katika kuboresha na kuimarisha kampeni zao za chanjo.

Dk Moeti ameongeza kuwa "Barani Afrika, mipango lazima iwe ya punjepunje zaidi. Kwa njia hii tunaweza kuona changamoto kabla hazijatokea na kutatua matatizo yoyote mapema. WHO inazisaidia nchi za Kiafrika katika kuendeleza, kuboresha na kutekeleza Mipango yao ya Kitaifa ya usambazaji wa chanjo na kuendelea kuboresha utoaji wao wa chanjo ya COVID-19 kadri zinavyoendelea," 

WHO inaendesha msaada wa dharura Afrika

WHO inafanya mpango wa msaada wa dharura kwa nchi tano za Kiafrika kusaidia, kuharakisha na kuboresha utoaji wao wa chanjo ya COVID-19, na mipango kwa nchi zingine 10 mwaka huu.

Wataalamu wa WHO wanafanya kazi na mamlaka za mitaa na washirika mashinani ili kuchanganua sababu za ucheleweshaji wowote, na jnjia bora ya kuzishughulikia.  

Nchini Sudan Kusini, mamlaka inalenga kuhakikisha kuwa ujumbe wa WHO utasaidia nchi hiyo kufikia lengo lake la kufikia ongezeko mara kumi la kiwango cha chanjo ya COVID-19, kila siku kutoka  chanjo 2,000 hadi 2,5000.

Takriban wagonjwa milioni 8.5 wa COVID-19 na zaidi ya vifo 217,000 vimerekodiwa barani Afrika.  
WHo inasema katika wiki iliyoishia ya Oktoba 24, kulikuwa na zaidi ya wagonjwa wapya 29, 300, idadi ikiwa imeshuka kwa karibu asilimia 30% ikilinganishwa na wiki iliyopita.  

Lakini nchi 10 za Afrika bado ziko katika awamu nyingine ya mlipuko, zikiwemo nne zenye mwelekeo wa kupanda juu ambazo ni Gabon, Congo, Cameroon na Misri.  

Viruzi aina ya Delta vimepatikana katika nchi 41, aina ya Alpha katika nchi 47, na aina ya Beta katika 43.
TAGS: WHO, Afrika, COVID-19, COVAX, chanjo