Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yapongeza makubaliano ya upatikanaji wa dawa za COVID-19 kwa urahisi na bei nafuu

Mhudumu wa afya nchini Brazil akichomwa chanjo ya COVID-19
© UNICEF/PAHO/Karina Zambrana
Mhudumu wa afya nchini Brazil akichomwa chanjo ya COVID-19

WHO yapongeza makubaliano ya upatikanaji wa dawa za COVID-19 kwa urahisi na bei nafuu

Afya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Afya ulimwenguni WHO na la kufanikisha upatikanaji wa tiba nafuu, UNITAID yamemekaribisha kutiwa saini kwa makubaliano ya leseni ya hiari kati ya kitengo cha haki miliki cha dawa -MPP na Kampuni kubwa ya famasia ulimwenguni - MSD ili kuwezesha dawa ya molnupiravir iweze kupatikana kwa bei nafuu na kwa mataifa mengi zaidi, kwa kuzingatia kuwa dawa hiyo mpya inaweza kupendekezwa kutibu mgonjwa mtu mzima wa COVID-19 asiye mahututi. 

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na WHO kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa makubaliano ya leseni ya MPP/MSD ni hatua chanya kuelekea kuunda ufikiaji mpana wa matibabu haraka iwezekanavyo kwa kuruhusu wenye leseni za generic kutoka kote ulimwenguni kuandaa vifaa na kuunda matoleo ya bei nafuu ya dawa, ikisubiri mapendekezo ya WHO na uidhinishaji mwingine wa udhibiti. 

Molnupiravir ni dawa ya kumeza ya kuzuia virusi, iliripotiwa kupunguza hatari ya kulazwa hospitalini au kifo kutokana na COVID-19 kwa asilimia 50 katika matokeo ya majaribio ya kliniki ya awamu ya 3 ya muda, na inasubiri kuidhinishwa kwa matumizi yake. Ikiidhinishwa, itakuwa dawa ya kwanza ya kumeza kwa wagonjwa wa COVID-19 wasiolazwa hospitalini ambao ugonjwa uko hali ya kati.

Hatua hii inaelezwa kusaidia kufupisha muda kutoka kwa idhini ya dawa hadi kupatikana kwake katika nchi 105 za kipato cha chini na cha kati zilizo chini ya leseni na ambako hakuna ukiukwaji wa hakimiliki na ujuzi wenye leseni haujatumiwa. 
WHO imesema inatumaini kutakuwa na ujumuishi wa nchi nyingine muhimu katika wigo wa makubaliano katika siku za usoni na kumshauri mtengenezaji atoe tamwimu za majaribio ya kimatibabu kwa WHO haraka iwezekanavyo, ili shirika hilo liweze kutathmini dawa kwa matumizi ya kimataifa.

Kampuni nyingine zinazounda chanjo, matibabu na uchunguzi nazo pia zimekumbushwa kuzingatia leseni zilizo wazi bila usiri haswa kwa teknolojia zingine za afya za COVID-19, ambazo zinahitaji kuhakikisha usambazaji mpana na unafuu katika nchi zote ili kumaliza janga hili