Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukifanya kazi pamoja tunaweza kukabili changamoto za mabadiliko ya tabianchi:UN

Wasichana wakiwa wamesimama nje ya shule yao iliyoharibiwa na dhoruba kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Nicolas Rice-Chudeau
Wasichana wakiwa wamesimama nje ya shule yao iliyoharibiwa na dhoruba kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tukifanya kazi pamoja tunaweza kukabili changamoto za mabadiliko ya tabianchi:UN

Tabianchi na mazingira

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekutana katika mjadala wa wazi kujadili mabadiliko ya tabianchi ukijikita na mada “Utekelezaji wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya watu, sayari dunia na ustawi.”

Mkutano huo ulioandaliwa na Rais wa Baraza Kuu Abdulla Shahidi ni wa kuchagiza na kutoa matumaini kwa dunia kwamba bado kuna fursa ya kulishinda janga la mabadiliko ya tabianchi duniani ikiwa ni siku chache tu kabla ya kuanza kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP26 utakaofanyika mjini Glasgow nchini Uingereza.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Rais wa Baraza hilo Shahidi amesema “ Matumaini yangu yanatokana na tathimini ya kweli ya changamoto iliyo mbele yet una uelewa kwamba tunauwezo wa pamoja wa kukabili changamoto hizo endapo tutashirikiana na kufanyakazi pamoja.”

Ameongeza kuwa lengo kubwa la mkutano wa leo ni “Kutathmini maendeleo yaliyopatikana tangu COP25 kwenye njia ya kuelekea COP26, na kutafakari yale tuliyojifunza katika jitihada zetu za kuongeza na kuharakisha hatua katika maeneo na sekta ambazo zimechelewa. Unazingatia pia baadhi ya suluhu zenye athari na ubunifu ambazo sote tunaweza kuunga mkono.”

Nyenzo tunazo za kutusaidia kutimiza leo

Shahidi amesisitiza kuwa licha ya safari kuwa ndefu kuna kila sababu ya kuwa na matumaini.
Mathalani amesema vyanzo mbadala sasa vinapunguza kwa kiasi kikubwa nishati ya mafuta kisukuku kama chanzo cha bei nafuu zaidi cha nishati duniani. Upatikanaji na matumizi yake yanaongezeka kwa viwango vya kutisha. 

Hatua za ulinzi wa pwani zinafanywa nchini India kutokana na kupanda kwa kina cha bahari.
Climate Visuals Countdown/Debsuddha Banerjee
Hatua za ulinzi wa pwani zinafanywa nchini India kutokana na kupanda kwa kina cha bahari.


Bidhaa zinazoweza kurejeshwa kwa bei nafuu huzipa nchi sababu za msingi za kuachana na makaa ya mawe huku zikikidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati, kuokoa gharama na kuongeza kazi.

Kuunga mkono sera za nishati safi kote ulimwenguni kama vile:
•    Ruzuku na punguzo la bei kwa kwa nishati ya sola inayowekwa kwenye paa za nyumba
•    kanuni zinazohitaji kuongezeka kwa nishati mbadala kama sehemu ya kuwa na mchanganyiko wa nishati; na
•     Kurejeshewa kodi kwa magari yanayotumia umeme, upepo na nishati ya jua imesaidia kwa kasi kuboresha na kueneza teknolojia huku ikipunguza gharama.

Shahidi amesema dunia bado haijafikia lengo la kukusanya dola bilioni 100 kwa mwaka kwa ajili ya ufadhili dhidi ya mabadiliko ya tabianchi  tathimini inaonyesha nchi zilizoendelea zitachelewa kwa miaka mitatu kutimiza ahadi zao na matumaini yoyote ya kufikia malengo ya ahadi zao yatawezekana mwanzoni mwa mwaka 2023.

Hata hivyo amehimiza kuwa “Juhudi zetu lazima zilenge sio tu kwenda zaidi ya ahadi tu bali kuhakikisha angalau dola trilioni 1 zinapatikana katika kusaidia nchi zinazoendelea ifikapo 2030.”

Kwa mantiki hiyo ameihimiza dunia “Hebu tufanye kazi kuhamasisha matumaini na ari kwa vijana wa leo. Hebu tuwarejeshee imani yao kwamba kwa hakika wanaweza kutegemea Umoja wa Mataifa kwa ishara kwamba amani, maendeleo, na ufanisi vinaweza kupatikana, kwa ajili ya sayari yetu na viumbe vyote vilivyomo kwani sayansi tunayo, uwezo tunao, rasilimali tunazo lililosalia tufanye kazi kwa pamoja. Naamini tunaweza, na tunapaswa kusaka utashi wa kumaliza janga la mabadiliko ya tabianchi.” 
 

Mafuriko nchini Bangladesh yalizamisha zaidi ya asilimia 25 ya nchi hiyo mwaka 2020.
Climate Visuals Countdown/Moniruzzaman Sazal
Mafuriko nchini Bangladesh yalizamisha zaidi ya asilimia 25 ya nchi hiyo mwaka 2020.

Huu ni wakati wa kukabili ukweli

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antinio Guterres akisisitiza umuhimu wa kukabili changamoto ya mabadiliko ya tabianchi amesema “Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ni ishara ya hatari kwa ubinadamu. Baraza hili  na nchi zote ulimwenguni zinakabiliwa na wakati wa kukabili ukweli. Katika siku sita zijazo viongozi wa dunia watajaribiwa katika katika mkutano wa COP26 huko Glasgow. Vitendo vyao au kutotenda kwao vitaonyesha umakini wao juu ya kushughulikia dharura hii ya dunia. Ishara za onyo ni vigumu kuzikosa.

Uchafuzi wa mazingira unaua watu milioni tisa kila mwaka. Kila siku, makumi ya viumbe hupotea. Hali ya joto kali hugeuza mashamba kuwa mandhari ya ukame. Miji na nchi nzima zinatazama viwango vya bahari vinavyoongezeka.m Kuongezeka kwa hali ya joto kutafanya sehemu kubwa za sayari yetu zishindwe kuishi kufikia mwisho wa karne hii.”

Guterres amekumbusha kwamba licha ya kengele ya inayogonga japo kwa sauti ya chini kunashuhudiwa ushahidi leo hii kwamba “hatua zinazochukuliwa hazikidhi haja ya kasi inayohitajika kwa haraka. Kwani bado tuko katika njia ya kufikia ongezeko la jotp duniani la nyuzijoto 2.7C kiwango kilicho juu zaidi ya lengo lililowekwa na viongozi kwenye mkutano wa Paris la nyuzi joto 1.5C lengo ambalo sayansi inatuambia ndio njia pekee ya kusonga mbele kwa dunia yetu. Na ambayo inaweza kutimizika”

Bwana Guterres ameongeza kuwa “Iwapo tunaweza kupunguza uzalishaji wa wa hewa chafuzi duniani  kwa asilimia 45 ikilinganishwa na viwango vya 2010 muongo huu. Iwapo tunaweza kufikia uzalishaji sifuri duniani kote ifikapo 2050, Na iwapo viongozi wa dunia watawasili Glasgow wakiwa na malengo ya 2030 ya ujasiri, yenye shauku na yanayoweza kuthibitishwa, na sera mpya thabiti za kutengua janga hili. Viongozi wa G20 haswa wanahitaji kutimiza ahadi zao kwani wakati umepita wa mambo mazuri ya kidiplomasia. Ikiwa serikali na haswa serikali za G20  hazitasimama kidete na kuongoza juhudi hii, tunaelekea kwenye mateso mabaya ya kibinadamu.”

Amesisitiza kuwa nchi zote duniani zinapaswa kutambua kwamba “muundo wa zamani wa kuchoma hewa ukaa kwa ajili ya maendfeleo ni hukumu ya kifo, kwa ajili ya uchumi wao na sayari yetu.”

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mjadala wangazi za juu kuchagiza na kutoa matuini kwa dunia kwamba bado kuna fursa ya kulishinda janga kuhusu mabadiliko ya tabianchi duniani
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mjadala wangazi za juu kuchagiza na kutoa matuini kwa dunia kwamba bado kuna fursa ya kulishinda janga kuhusu mabadiliko ya tabianchi duniani

Hewa ukaa lazima ipunguzwe hakuna jinsi

Katibu Mkuu ametaka hewa ukaa ipunguzwe sasa katika sekata zote na katika kila nchi.
Pia ametaka kubadili mwelekeo wa ruzuku kutoka kwenye mafuta kisukuku na kuingia kwenye nishati jadidifu na kuweka kodi katika masuala ya uchagfuzi  wa hew ana sio kwa watu.

Guterres pia amesema dunia inahitaji kuweka bei kwenye hewa ukaa, na njia ambazo zinarudisha nyuma miundomsingi na kazi zinazostahimili.  

Na kuongeza kuwa dunia inahitaji kuondoa makaa ya mawe ifikapo mwaka 2030 katika nchi za OECD na ifikapo 2040 katika nchi zingine zote. Serikali zinazidi kukubali kusitisha ufadhili wa makaa ya mawe  sasa fedha za kibinafsi zinahitaji kufanya vivyo hivyo, haraka.
 
Na ametaka vijana na wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi kuendelea kufanya kile wanachofanya: kudai hatua kutoka kwa viongozi wao. “Kwa muda wote, tunahitaji mshikamano wa kimataifa ili kusaidia nchi zote kufanya mabadiliko haya. Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na migogoro ya madeni na ukwasi. Narejea wito wangu kwa wafadhili na benki za maendeleo za kimataifa kutoa angalau asilimia 50 ya msaada wao wa mabadiliko ya tabianchi katika kukabiliana na hali na kujenga mnepo katika nchi zinazoendelea. Kuna njia moja tu ya kusonga mbele ambayo ni mustakbali wenye nyuzi joto 1.5C kwa binadamu wote. Natoa wito kwa viongozi kulifanyia kazi hili kabla hatujachelewa zaidi.”