Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wakimbizi 60,000 wa Burundi warejea nyumbani mwaka huu pekee

Wakimbizi wa Burundi waliorejea nyumbani wakiwa katika kijiji cha Higiro kaskazini mwa Burundi. (Maktaba)
© UNHCR/Georgina Goodwin
Wakimbizi wa Burundi waliorejea nyumbani wakiwa katika kijiji cha Higiro kaskazini mwa Burundi. (Maktaba)

Zaidi ya wakimbizi 60,000 wa Burundi warejea nyumbani mwaka huu pekee

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema wakimbizi 343 wa Burundi waliokuwa wanaishi  nchini Uganda wamerejea nyumbani jana Jumatatu na hivyo kufanya idadi ya warundi waliorejea nyumbani mwaka huu pekee kuwa zaidi ya 60,000.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi Shabia Mantoo amewaeleza waandishi wa habari hii leo kuwa nusu ya wakimbizi hao 60,000 wanatoka Tanzania huku wengine waliosalia walikuwa wamesaka hifadhi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kenya na Rwanda na Uganda.

“UNHCR inachofanya sasani kusaidia kufanikisha uamuzi wao wa kurejea nyumbani kwa hiari na imefanya tathmini kuhakikisha wanarejea kwa hiari, kwa uhuru na kwa utu na  kwa kutambua hali ilivyo nyumbani,” amesema Bi. Mantoo akiongeza kuwa kila wiki msafara unawasili na watu 1,500.

Punde baada ya kuwasili katika moja ya vituo vitano vya mapokezi, familia zinapatiwa vifaa vya nyumbani na msaada wa fedha ili waweze kuanza maisha yao.

Hata hivyo amesema misaada zaidi inahitajika ili kufanikisha lengo la kuwajumuisha vyema katika jamii zao sambamba na kusaidia jamii zinazowapokea ambako “hakuna miundombinu ya kijamii na kiuchumi. Kuna majanga mengi ya ukimbizi wa ndani duniani lakini hali ya Burundi ni tofauti sana ambako wakimbizi wanarejea nyumbani kwa kiasi kikubwa. Lakini bila mipango bora ya kuwajumuisha kwenye jamii, basi mzunguko wa ukimbizi unaweza kurejea tena.”

Fedha zahitajika zaidi

Ni kwa mantiki hiyo UNHCR inatoa wito wa fedha zaidi kwa ombi la pamoja la mwaka 2021 la kusaidia wakimbizi kurejea na kujumuishwa vema katika jamii zao, ombi lililotolewa mwanzoni mwa mwaka huu likitaja mahitaji ya wadau 19 wa kibinadamu na maendeleo ya kusaidia wakimbizi kurejea na kujumuishwa vema kwenye jamii.

“Kama mfano wa juhudi zetu, UNHCR ilizindua kituo cha kwanza cha kitaifa cha kinga na tiba dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 huko jimboni Cankuzo ambako wakimbizi wengi wanarejea mashariki mwa nchi.” Ametoa mfano Bi Mantoo.

Ametanabaisha kuwa kati yad ola milioni 104.3 zinazohitajika, ni asilimia 10 tu ya fedha zinazohitaijka kusaidia wakimbizi kurejea na kujumuishwa kwenye jamii ndio zimetolewa licha ya ongezeko la idadi ya wakimbizi wanaorejea nyumbani kwa hiari.

Tangu mwaka 2017 wakati ambapo mpango wa usaidizi wa kurejea nyumbani kwa  hiari ulipoanza, zaidi ya wakimbizi 180,000 wa Burundi wamerejea nyumbani na kumekuweko na ongezeko kubwa tangu mwezi Julai mwaka jana wa 2020 baada ya uchaguzi mkuu nchini humo.

Takribain wakimbizi 270,000 wa Burundi bado wanaishi ukimbizini nchini Tanzania, Uganda, Rwanda, DRC, Kenya, Msumbiji, Malawi, Afrika Kusini na Zambia.