Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi nyingi hazijawasilisha rasmi ahadi mpya za kupunguza hewa chafuzi:UNEP

Viwanda vikubwa hutoa hewa chafuzi ambayo inasababisha shida kadhaa za kiafya.
Unsplash/ Sergio Rodriguez
Viwanda vikubwa hutoa hewa chafuzi ambayo inasababisha shida kadhaa za kiafya.

Nchi nyingi hazijawasilisha rasmi ahadi mpya za kupunguza hewa chafuzi:UNEP

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP imeeleza kuwa ahadi mpya na zilizorekebishwa kuhusu viwango vya nchi vya kukabili mabadiliko ya tabianchi, NDCs hazijafikia lengo lililowekwa katika mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na hivyo ulimwenguni kuwa hatarini kuwa na ongezeko la joto la angalau nyuzijoto angalau 2.7 katika karne hii.

Ripoti hiyo ya 12 ikipatiwa jina la “Ripoti ya Pengo la Utoaji hewa chafuzi mwaka  2021: Joto Linaongezeka” imetolewa leo jijini Nairobi, Kenya ikiwa ni siku chache kuelekea katika mkutano wa 26 nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen amesema "dunia inapaswa kuamka na kuondokana na hatari inayotukabili. Mataifa yanahitaji kuweka sera ili kutimiza ahadi zao mpya, na kuanza kuzitekeleza ndani ya miezi kadhaa. Yanahitaji kufanya ahadi zao za kutozalisha kabisa hewa chafuzi ziwe thabiti zaidi, kuhakikisha ahadi hizi zinajumuishwa katika viwango vya nchi vya kuchangia kukabili mabadiliko ya tabianchi (NDCs), na hatua zinaletwa mbele. Kisha wanahitaji kupata sera ili kuunga mkono azma hii iliyoibuliwa na tena, kuanza kuzitekeleza kwa haraka.”

Ripoti hiyo imegundua kuwa, marekebisho yaliyofanywa na nchi katika viwango vyao vya kuchangia kukabili mabadiliko ya tabianchi na ahadi zingine zilizotolewa kuelekea mwaka 2030 bado hazijawasilishwa katika tovuti maalum kwa ajili ya marekebisho hayo kurekodiwa kwa ajili ya kujumuishwa pamoja na kupata taswira kamili ya marekebisho ambayo nchi zinadhamiria kufanya ili kuhakikisha hewa ukaa inapungua duniani.

“Mabadiliko ya tabianchi si tatizo tena la siku zijazo. Ni tatizo la sasa,” amesema Andersen, na kuongeza kuwa “Ili kupata nafasi ya kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiasi, tuna miaka minane ya karibu kupunguza nusu ya uzalishaji wa gesi chafuzi: miaka minane ya kufanya mipango, kuweka sera, kuzitekeleza na hatimaye kupunguza. Saa inasogea kwa sauti kubwa."

Waandishi wa ripoti hiyo wameeleza kuwa ahadi ya kufikia kutozalisha kabisa hewa chafuzi na utekelezaji mzuri zinaweza kuleta mabadiliko makubwa, lakini mipango ya sasa ni ya utata na haijaoneshwa katika NDCs. Jumla ya nchi 49 pamoja na Muungano wa Ulaya EU zimeahidi kufikia lengo la kutozalisha kabisa hewa chafuzi.

Lengo hili linawezesha kupunguza zaidi ya nusu ya uzalishaji wa gesi chafuzi duniani, zaidi ya nusu ya Pato la Taifa na theluthi moja ya idadi ya watu duniani. Malengo kumi na moja yamewekwa katika sheria, yanajumuisha asilimia 12 ya uzalishaji wa kimataifa.
 
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNEP amesisitiza kuwa ni muhimu kutoa usaidizi wa kifedha na kiteknolojia kwa mataifa yanayoendelea ili waweze kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuanzisha muelekeo mpya wa ukuaji wa chini wa uzalishaji wa hewa chafuzi.