Wajumbe wa Baraza la Usalama wawasili Mali kupata taswira halisi

23 Oktoba 2021

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamewasili nchini Mali kwa ziara ya siku mbili, ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya siku 5 kwenye ukanda wa Sahel, ziara ambayo pia  itawapeleka nchini Niger.
 

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili mjini Bamako, Mali Mwakilishi wa kudumu wa Kenya, Balozi Martin Kimani ambaye ndiye Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Oktoba amesema ziara yao inalenga kuwapatia taswira halisi ya taifa hilo la ukanda wa Sahel ili hatimaye waweze kuwa na mashauriano ya kina jijini New York, Marekani.

Balozi Kimani amesema, “kama taifa lenzetu la Afrika, hali ya Mali na Sahel inatugusa sana Kenya. Tuna wasiwasi mkubwa na ukosefu wa usalama unaoendelea Mali na kusambaa kwa ugaidi na athari zake kwa wananchi wa Mali. Baraza la Usalama limekuwa linasaidia Mali kwa takribani miaka 10 sasa, na ujumbe wetu ni kwamba usaidizi wetu ni thabiti na hautetereki na utaendelea. Tuko hapa kusikiliza mamlaka za mpito na kubaini njia bora zaidi za kuwasaidia ili kufanikisha mpito huu.”

Balozi Kimani amesema wana ujumbe pia thabiti kuhusu umuhimu wa kufanya uchaguzi nchini Mali na kutekeleza mkataba wa amani na kurejesha utulivu eneo la kati la Mali.

Amesisitiza kuwa wanaona juhudi za Baraza hilo kuwa zinaunga mkono na kuimarisha zile za Muungano wa Afrika, AU, na Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.

Walinda amani kutoka kikosi cha Ivory Coast katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani Mali, MINUSMA, wanashika doria.
MINUSMA
Walinda amani kutoka kikosi cha Ivory Coast katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani Mali, MINUSMA, wanashika doria.

Kenya tumepitia mnayopitia – Balozi Kimani

Balozi Kimani amesema “kama Kenya tunaunga mkono juhudi zozote za kukabiliana na ugaidi na kudhibiti misimamo mikali inayounga mkono ugaidi katika ukanda ambao nchi nyingi zinakabiliwa na mashambulizi kutoka vikundi vya kigaidi. Kenya nasi tulikumbwa na mashambulizi ya kigaidi na tuna uzoefu wa kile ambacho Mali inapitia. Ni kwa mshikamano tu ndio tunaweza kushinda. Tuko hapa kufanya kazi na Mali.”
Ziara hii ya wajumbe wa Baraza la Usalama ni ya kwamba tangu mlipuko wa ugonjwa wa Corona au COVID-19 mwaka jana.

Wakiwa nchini Mali, wajumbe hao 15 wa Baraza la Usalama watakuwa na mikutano na wawakilishi wa serikali ya mpito, pande zilizotia saini mkataba wa amani wa mwaka 2015, jopo la usuluhishi na wawakilishi wa ECOWAS.

Halikadhalika watakutana na wawakilishi wa mashirika ya kiraia, wanawake, vijana na viongozi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA na wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Mpito Mali

Serikali ya mpito nchini Mali ilianzishwa kwa kipindi cha miezi 18 baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Agosti mwaka jana wa 2020 yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keïta. 

Awamu ya kwanza ya uchaguzi wa wabunge na rais imepangwa kufanyika tarehe 27 mwezi Februari mwaka 2022.

Hata hivyo tangu mapinduzi ya pili ya kijeshi  ya tarehe 24 mwezi Mei mwaka huu ya kuwaondoa viongozi wa serikali ya mpito na kumweka madarakani Kanali Assimi Goïta, kuna wasiwasi iwapo uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.

Kutoka Mali, wajumbe wa Baraza watakwenda Niamey, Niger kukutana na viongozi wa serikali na wale wa Umoja wa Mataifa. Halikadhalika watakuwana na Meja Jenerali Oumar Bikimo ambaye ni Kamanda wa jeshi la kundi la nchi 5 kwa ajili ya Sahel, G5S ambalo linajumuisha nchi za Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter