Madagascar: Njaa kali inayochochewa na mabadiliko ya tabianchi?

23 Oktoba 2021

Zaidi ya watu milioni moja kusini mwa Madagascar wanahaha kupata mlo, nah ii inaweza kuwa ni tukio la kwanza kabisa duniani la watu kukumbwa na njaa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP.
 

Eneo hilo la kusini limeshuhudia mfululizo wa vipindi vya ukame na kulazimsha familia za vijijini kusaka mbinu mbalimbali kuweza kuishi.

Madagascar, kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani, ina mfumo wa ekolojia wa kipekee, ikiwemo wanyama na mimea ambayo haiwezi kupatikana eneo lolote lile duniani. Nchi hiyo imekumbwa na vipindi vya ukame, hususan kuanzia mwezi Mei hadi Oktoba na msimu wa mvua huanza mwezi Novemba.

Wakazi katika maeneo  yaliyokumbwa na ukame huok Ifotaka kusini mwa Madagascar wakipokea msaada wa chakula kutoka WFP
© WFP/Tsiory Andriantsoarana
Wakazi katika maeneo yaliyokumbwa na ukame huok Ifotaka kusini mwa Madagascar wakipokea msaada wa chakula kutoka WFP

Maisha ya kila siku yamevurugwa

Hata hivyo, mabadiliko ya tabianchi yamevuruga misimu hiyo na kuathiri wakulima wadogo wadogo na majirani zao, amesema Alice Rahmoun, Afisa Mawasiliano wa WFP wakati akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya simu akiwa kwenye mji kuu wa Madagascar, Antananarivo .
“Bila shaka kuna mvua kidogo, wanaweza kuwa na matumaini na kupanda mbegu za mazao. Lakini mvua kidogo si mvua sahihi ya msimu,” amesema.

“Kwa hiyo, kile ninachoweza kusema ni kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi nchi ni dhahiri kabisa na mavuno hakuna mara kwa mara kwa hiyo watu hawana chochote cha kuvuna na hata kuimarisha akiba yao.”

Athari tofauti tofauti

Hivi karibuni Bi. Rahoun alitembelea kusini mwa Madagascar ambako WFP na wadau wak wanasaidia mamia ya maelfu ya wananchi kwa kuwapatia misaada ya muda mfupi na muda mrefu.
Madhara ya ukame yanatofautiana kati ya eneo na eneo, amesema akiongeza kuwa wakati baadhi ya jamii hazijapata msimu sahihi wa mvua kwa miaka mitatu, hali inaweza kuwa mbaya zadi kilometa 100 kutoka eneo hilo.

Amekumbuka kuona vijiji vikiwa vimezingirwa na mashamba makame, huku mimea ya viazi ikiwa imebadilika na kuwa rangi ya manjano au udongo kudokana na ukosefu wa maji.

Mlo ni nzige na majani ya dungusi kakati

“Katika baadhi ya maeneo bado wanaweza kupanda mazao lakini si rahisi kabisa kwa hiyo wanajaribu kupanda viazi vitamu. Lakini kwenye maeneo mengine, hakika hakuna kitu cha kuotesha hivi sasa kwa hiyo watu wanaishi kwa kula nzige, matunda na majani ya dungusi kakati,” amesema Bi. Rahmoun.   

“Na kwa mfano mmoja tu, majani ya dungusi kakati ni kwa ajili ya mifugo na si kwa ajili ya matumizi ya binadamu.”
“Hali ni mbaya zaidi kwa sababu hata majani hayo ya dungusi kakati nayo yanakauka kutokana na ukame, kwa sababu ya ukosefu wa mvua na maji, kwa hiyo inatia hofu kubwa,” amesema.

Mwanamke huyu akipita eneo kavu lenye mchanga mwingi huko Kusini mwa Madascar baada ya kujipatia mgao wa chakula kutoka WFP
© WFP/Tsiory Andriantsoarana
Mwanamke huyu akipita eneo kavu lenye mchanga mwingi huko Kusini mwa Madascar baada ya kujipatia mgao wa chakula kutoka WFP

Familia zinajikimu kwa shida

“Maisha duni ya familia nayo yanatia hofu na machungu, “Watu tayari wameanza kusaka mbinu za kuweza kuishi”, amesema.
“Na hii inamaanisha kwamba wanauza mifugo yao, ili waweze kupata fedha na kununua chakula, ilhali awali waliweza kupata chakula na kujilisha wenyewe kutokana na mazao ya shambani, kwa hiyo imebadili mfumo wa maisha ya watu,”

Rasilimali za thamani kama mashamba, au hata nyumba nazo pia zinauzwa. Baadhi ya familia zimeondoa watoto wao shuleni.

“Ni mkakati sasa wa familia kujikusanya na kutumika kama mbinu za kujipatia kipato wakihusisha watoto, kwa hiyo ni dhahiri kuna athari mbaya katika elimu,” amesema Bi. Rahmoun.

Kuwapatia misaada ya kuokoa maisha

WFP inashirikiana na wadau wa kibinadau na serikali ya Madagascar kuchukua aina mbili za hatua dhidi ya janga hili. Takribani watu 700,000 wanapata msaada wa kuokoa maisha ikiwemo chakula na vitu vingine vyenye virutubisho kukabili utapiamlo.

“Hatua ya pili ni ya muda mrefu ambayo itawezesha jamii kuweza kujiandaa na kuchukua hatua pindi janga linatokea tena na kujikwamua kutoka athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Bi. Rahmon akiongeza kuwa “kwa hiyo hii inajumuisha miradi ya mnepo kama vile miradi ya maji, tunajenga mifereji ya umwaguliaji, miradi ya kurejesha misitu na hata kuwapatia fedha kidogo kusaidia wakulima wadogo wadogo kujikwamua kutoka hali ya mavuno duni.”

WFP lengo lake ni kusaidia watu milioni moja kati ya sasa na mwezi Aprili mwakani na inasaka takribani dola milioni 70 kufanikisha operesheni zake. “Lakini tunashirikisha wadau wengi zaidi kusaka na kuchangia suluhu za athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii kusini mwa Madagascar.”

Ukame na umasikini umesababisha njaa kali kusini mwa Madagascar
© WFP/Tsiory Andriantsoarana
Ukame na umasikini umesababisha njaa kali kusini mwa Madagascar

COP26: Kipaumbele ni kuhimili changamoto za mazingira

Wiki moja ijayo, viongozi wanakutana huko Glasgow Scotland kwa ajili ya mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 ambako Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameita ni furs aya mwisho ya kubadil imwelekeo wa wimbi dhidi ya sayari ya dunia inayougua.
Bi. Rahmoun anasema WFP inataka ktumia mkutano huo kubadili mwelekeo wa hatua dhidi ya janga la Madagascar. Nchi lazima zijiandae dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na lazima zishirikiana kupunguza madhara  hayo kwa jamii zilizo hatarini zaidi kama zile za Kusini mwa Madagascar.

“COP26 pia ni fursa ya sisi kuziomba serikali na wahisani kupatia kipaumbele uelekezaji wa fedha kwenye miradi inayohusiana na kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kusaidia nchi kujenga mipango bora ya usimamizi n ahata Madagascar, kwa sababu kama hakuna kitakachofanyika, njaa itaendelea kwa kiwango kikubwa katika miaka ijayo kwa sababu mabadiliko ya tabianchi si kwa Madagascar pekee bali kwa dunia nzima,” ametamatisha Bi. Rahmoun.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter