Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko yanayoendelea Eswatini yanawaweka watoto njiapanda: UNICEF

Watoto nchini Eswatini wakicheza katika shule ya msingi mkoani Lobamba
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Watoto nchini Eswatini wakicheza katika shule ya msingi mkoani Lobamba

Machafuko yanayoendelea Eswatini yanawaweka watoto njiapanda: UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema linatiwa hofu kubwa kuhusu Watoto nchini Eswatini kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama kufuatia machafuko yanayoendelea.

Kwa mujibu wa Mohamed M.Fall mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika , hatua za kukabiliana na hali tete inayoendelea ni lazima kwanza ziheshimu na kulinda haki za msingi za Watoto chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za mtoto.

“Watoto wameendelea kubeba gharama za machafuko hayo, ikiwemo kutoka kwa  vikosi vya jeshi, shuleni na mitaani. Watoto wengine wameripotiwa kupata vilema, kuteswa na kukamatwa, hali ambayo inakwenda kinyume na uwajibikaji wa kisheria wa serikali kwa watoto na inaweza kuacha athari za kudumu au za muda mrefu za kimwili au kisaikolojia.”

Kwa mantiki hiyo afisa huyo wa UNICEF amesema “Tunatoa wito kwa wadau wote kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa wakati wote na licha ya mazingira ambayo wanaweza kujikuta nayo. Kufungwa kwa shule bila kikomo bado ni wasiwasi mkubwa kwani kuna athari mbaya kwa watoto kutokana na kupoteza masomo, afya ya akili na athari za kisaikolojia na hatari ya kuathiriwa na unyanyasaji na unyonyaji. Shule lazima zibaki wazi, miundombinu na mali zao zinapaswa kuheshimiwa, na lazima ziwe maeneo ya amani na mahali salama kwa watoto.”

Mkurugenzi huyo amesisitiza kwamba kuna haja ya haraka ya kuingilia kati kutoka kwa wadau wote wanaohusika.

Ameongeza kuwa mazungumzo yenye maana bado ni suluhisho bora zaidi ili kuepuka vurugu zaidi na usumbufu kwa huduma muhimu kwa watoto na wanawake. “Ni njia pekee ya kuhakikisha kuwa Eswatini inabaki kuwa nchi yenye amani ambayo watoto wanaweza kuishi na kufanikiwa. Kama ilivyosemwa na Nelson Mandela kwamba 'tabia halisi ya jamii inabainika kutokana na jinsi inavyowatendea watoto wake.' Tusisahau maneno hayo kamwe."