Skip to main content

Chonde chochonde Libya anzisheni haraka mpango kunusuru wakimbizi na waomba hifadh:UNHCR

UNHCR inatoa msaada wa dharura kwa waomba hifadhi na wakimbizi walioathirika na operesheni yakamata kamata inayoendeshwa na serikali huko Tripoli, Libya
© UNHCR/Mohamed Alalem
UNHCR inatoa msaada wa dharura kwa waomba hifadhi na wakimbizi walioathirika na operesheni yakamata kamata inayoendeshwa na serikali huko Tripoli, Libya

Chonde chochonde Libya anzisheni haraka mpango kunusuru wakimbizi na waomba hifadh:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, leo imeihimiza serikali ya Libya kushughulikia mara moja hali mbaya ya waomba hifadhi na wakimbizi kwa njia ya kibinadamu na ya haki.

Shirika hilo linasema Misako na kamatakamata inayofanywa na mamlaka mwezi huu inalenga maeneo yenye wakazi wengi wakimbizi na waomba hifadhi ambayo imesababisha vifo kadhaa, maelfu kuzuiliwa, na wengi wakiachwa masikini na  bila makazi.

Vincent Cochetel, mwakilishi maalum wa UNHCR kuhusu hali ya eneo la Mediterranea ya Kati na Magharibi amesema “Tangu kuanza kwa misako na kukamatwa na maafisa wa Libya mwezi Oktoba, tumeshuhudia kuzorota kwa kasi kwa hali inayowakabili wanaotafuta hifadhi na wakimbizi walio hatarini huko Tripoli. Mamlaka ya Libya lazima ije na mpango mzuri unaoheshimu haki zao na kubainisha suluhisho la kudumu. "

Watu zaidi ya 3000 wametawanywa

"Watu wapatao 3,000 hivi sasa wamepata hifadhi nje ya kituo cha kutwa cha jamii (CDC) huko mjini Tripoli, ambako UNHCR na washirika wake wamekuwa wakiwapa msaada wa matibabu na huduma zingine. Hali ni ya hatari sana. Wengi waliathiriwa na msako huo, ubomoaji wa nyumba zao, na wametoroka kizuizini katika hali mbaya. Wengine wamejiunga na kikundi hicho wakitumaini kuhamishwa. Wengi wameachwa bila makazi na kupoteza mali zao zote kutokana na operesheni ya usalama na sasa wanalala kwenye baridi na katika mazingira yasiyo salama kabisa. Hii haikubaliki kabisa.”

UNHCR na washirika walilazimika kusitisha operesheni zao katika kituo hicho cha kutwa cha jumuiya kwa sababu za ulinzi na usalama, lakini wakabaki wakishiriki mazungumzo na wawakilishi wa waandamanaji nje ya CDC kuelezea msaada mdogo ambao wanaweza kuutoa, ukiwa ni pamoja na msaada wa pesa na chakula.

Pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, UNHCR iko tayari kusaidia mpango wa dharura wa hatua ambao unaweza kusaidia kupunguza mateso mabaya yanayowakabili  waomba hifadhi na wakimbizi nchini Libya.

UNHCR inaendelea kutoa wito kwa mamlaka kuheshimu haki za binadamu na utu wa watu wanaoomba hifadhi hadhi na wakimbizi, waache kuwakamatwa kiholela na kuwaachilia wanaowashikilia kutoka kizuizini.

UNHCR yakaribisha kuanza safari za kuwahamisha

Shirika la UNHCR pia limekaribisha idhini ya kuanza tena safari za uokoazi wa kibinadamu, lakini linaonya kuwa hazitoshi.

“Haya ni maendeleo mazuri kwa baadhi ya wakimbizi walio katika mazingira magumu zaidi, ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kwa miezi kadhaa kuondoka. Timu zetu tayari zinafanya kazi ya kuhakikisha safari za ndege hizo za kibinadamu zinaanza haraka iwezekanavyo," amesema  Cochetel na kuongeza kuwa  “Lakini pia tunahitaji kuwa wakweli, kwani mahali tunakowahamishia au safari za uokoazi zitawafaidisha idadi ndogo tu ya watu. "

Zaidi ya wakimbizi 1000 walio katika mazingira magumu na wasaka hifadhi kwa sasa wanapewa kipaumbele kwa safari hizo za kibinadamu na wanasubiri zianze tena. UNHCR inaendelea kuisisitiza jamii ya kimataifa kutoa njia zaidi za kisheria salama za kutoka Libya.