Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 667 zahitajika kusaidia mgogoro wa kiuchumi: UNDP

Mizozo na kutokuwepo kwa usalama nchini Afghanistan kumewaacha watoto katika hatari kubwa kuwahi kutokea
© UNICEF/Shehzad Noorani
Mizozo na kutokuwepo kwa usalama nchini Afghanistan kumewaacha watoto katika hatari kubwa kuwahi kutokea

Dola milioni 667 zahitajika kusaidia mgogoro wa kiuchumi: UNDP

Msaada wa Kibinadamu

Uchumi wa Afghanistan unakua, kwa wote isipokuwa asilimia tatu ya kaya nchini humo zinatarajiwa kushuka chini ya mstari wa umaskini katika miezi ijayo, umesema Umoja wa Mataifa.

Ili kuwasaidia Waafghanistan wa kawaida, leo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP limetangaza kuzindua mfuko wa "uchumi wa watu", ili kutoa msaada unaohitajika haraka wa pesa.

Mfuko huo utatumia michango iliyozuiliwa tangu kundi la Taliban kuchukua mamlaka mwezi Agosti mwaka huu.  

Ujerumani tayari imeahidi dola milioni 58 kati ya zaidi ya dola milioni 660 zinazohitajika kwa miezi 12 ijayo, amersema mkuu wa UND, Achim Steiner alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo.

"Kuna watu milioni 38 ambao hawawezi kuhakikishiwa uhai wao kwa msaada tu  kutoka nje . Lazima tuingilie kati, lazima tuimarishe uchumi wa watu na pia zaidi ya kuokoa maisha, tunapaswa pia kuokoa jinsi ya kujikimu kimaisha. Kwa sababu vinginevyo, tutalazimika kukabiliana na hali wakati wa msimu wa baridi na hadi mwaka ujao ambapo mamilioni kwa mamilioni ya Waafghanistan hawawezi kubaki nchini mwao, majumbani mwao, katika vijiji vyao na kuishi."

Kukusanya rasilimali

UNDP sasa inawasiliana na wafadhili wengine kukusanya rasilimali, amesema Bwana Steiner na kuongeza kwamba "Majadiliano katika wiki chache zilizopita yamezingatia jinsi tutakavyopata njia ya kuweza kukusanya rasilimali hizi kwa kuzingatia shinikizo la kiuchumi ambao sasa linaibuka na kujitolea mara kwa mara kwa jamii ya kimataifa kutowaacha nyuma watu wa Afghanistan".

Kuzuia zahma kubwa

Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alihimiza dunia kuchukua hatua katika wakati huu wa "kujenga au kubomoa" nchi hiyo.  

Wakati aliporudia kusema kwamba "msaada wa kibinadamu unaokoa maisha", mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alionya kwamba "haitasuluhisha shida ikiwa uchumi wa Afghanistan utaanguka".

Mfuko huo ni sehemu ya programu mpya kwa nchi hiyo inayoitwa ABADEI, ambayo inaashiria mnepo wa jamii.

UNDP inasema mfuko huo unatarajiwa kuchangia kuzuia janga la kibinadamu na uchumi wa nchi hiyo kusambaratika kabisa kwa kusaidia idadi ya watu walio hatarini zaidi na nusuru kuanguka kwa biashara ndogondogo nchini Afghanistan.

ABADEI itaona UNDP, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yakitoa suluhisho katika jamii ambazo zinasaidia hatua za haraka za kibinadamu.

Mbali na ukame wa muda mrefu na athari za janga la COVID-19, Afghanistan inapambana na machafuko yaliyosababishwa na mabadiliko ya kisiasa ya sasa.
UNDP Afghanistan
Mbali na ukame wa muda mrefu na athari za janga la COVID-19, Afghanistan inapambana na machafuko yaliyosababishwa na mabadiliko ya kisiasa ya sasa.

Kuendeleza uchumi wa ndani

Bwana Steiner ameongeza kuwa "Nchi inahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu, lakini pia tunahitaji kufanya uchumi wa eneo kuendelea, hii ni jambo la msingi kuhakikisha kuwa watu bado wana maisha na wanahisi kuwa wana maisha ya baadaye katika jamii zao.”

Fedha taslimu za ndani zitapewa moja kwa moja kwa vikundi vya jamii na kwa wafanyikazi wa Afghanistan katika programu za kazi za umma, kama za kukabiliana na ukame na kudhibiti wa mafuriko.

Misaada pia zitapewa biashara ndogondogo na mapato ya msingi ya muda yatalipwa kwa wazee na watu wenye ulemavu walio hatarini, ameongeza Kanni Wignaraja, mkurugenzi wa ofisi ya Kanda ya ASsia Pasifiki wa UNDP.

“Hii itawawezesha watu kukaa, kuishi na kufanya kazi katika ardhi zao na katika nyumba zao na kuwaruhusu kupata kipato na kuwapa heshima na hadhi ambayo wanastahili na kuitaka", amesema Bi Wignaraja.
Msaada wote utakaotolewa utategemea tathmini zisizo na upendeleo zinazofanywa kwa kushirikiana na viongozi wa jamii na bila kuingiliwa na mamlaka.