Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 5,000 wametawanywa Yemen wiki hii pekee:UNHCR

Wakimbi wa ndani wa hivi karibuni wakisubiri kupokea msaada wa kibinadamu huko Marib, Yemen
UN OCHA/GILES CLARKE
Wakimbi wa ndani wa hivi karibuni wakisubiri kupokea msaada wa kibinadamu huko Marib, Yemen

Watu zaidi ya 5,000 wametawanywa Yemen wiki hii pekee:UNHCR

Amani na Usalama

Watu zaidi ya 5,000 wametawanywa wiki hii pekee kwenye jimbo la Mashariki la Marib nchini Yemen kutokana na mapigano baina ya vikosi vya serikali na waasi wa Houthi limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kupitia ripoti yake ya hali ya kibinadamu nchini Yemen iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi UNHCR inasema “Inatiwa hofu kubwa na kuongezeka kwa mapigano ambayo yanasababisha maelfu ya familia kutawanywa kila mara. Familia 800 zilizo na watu zaidi ya 5,000 zimelazimika kukimbia machafuko hayo wiki hii pekee.”

Tangu kuanza kwa mwaka 2021 kwa mujibu wa UNHCR karibu watu 80,000 sawa na zaidi ya familia 13,000 wamelazimika kuzikimbia nyumba zao na kusaka hifadhi kwingineko nchini Yemen.

Kwa jumla, zaidi ya watu milioni 4 wamekuwa wakimbizi wa ndani. Kulingana na Umoja wa Mataifa, watoto na wanawake ni asilimia 76% ya jumla ya wakimbizi hao wa ndani au IDP.  

Takwimu za UNHCR zinaonyesha kuwa Wayemeni milioni 1.2 waliohama makazi yao wanaishi katika maeneo 1,800 ya malazi  maalum yaliyotengwa .

Jimbo la Marib ndio eneo ambalo tayari linahifadhi robo ya wakimbizi wa ndani milioni nne nchini Yemen.
Kwa kuongezea, UNHCR inasema nchi hiyo inahifadhi wakimbizi karibu 130,000 na zaidi ya waomba hifadhi 12,000.

Vizuizi vya misaada ya kibinadamu Marib

Mzozo nchini Yemen umesababisha kukatili maisha ya maelfu ya watu wengi wao wakiwa ni raia, na umesababisha kile Umoja wa Mataifa unachokiita kama mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Zaidi ya watu milioni 20 wanahitaji msaada nchini humo. Umoja wa Mataifa pia umeripoti kuwa watoto wanne kati ya watano wanahitaji msaada wa kibinadamu, au sawa na zaidi ya watoto milioni 11.

Licha ya hali hiyo vizuizi vya kusambaza misaada ya kibinadamu huwanyima zaidi fursa wale wanaohitaji zaidi msaada huo muhimu.  

Licha ya kuzorota kwa hali ya usalama, UNHCR inaendelea kutoa msaada kwa walio hatarini zaidi.

Baada ya kusimamishwa kwa muda kwa shughuli katika wilaya ya Al Jubah huko Marib kwa sababu ya wasiwasi wa usalama, Jumuiya ya ushirikiano wa kibinadamu, mdau mkubwa wa malazi wa UNHCR, ilianza tena usambazaji wa vitu visivyo vya chakula kwa familia 75 (watu 500) katika jimbo hilo na kwa familia zingine 149 (Watu 864) wanaoishi katika mji wa Marib.

Mwanamume aliyeyakimbia makazi yake kwasasa anaishi katika hema kwenye makazi yawakimbizi wa ndani huko Marbin nchini Yemen.
UN OCHA/GILES CLARKE
Mwanamume aliyeyakimbia makazi yake kwasasa anaishi katika hema kwenye makazi yawakimbizi wa ndani huko Marbin nchini Yemen.

Kuongezeka kwa watu waliokimbia makazi yao katika mazingira magumu

Kwa kuongezea, UNHCR ripoti inasema matokeo ya hivi punde ya mahitaji ya haraka ya UNHCR na tathmini ya mazingira magumu yanaonyesha ongezeko kubwa la udhaifu kwa wakimbizi wa ndani.

Kwa mwaka huu wa 2021 hadi mwezi Oktoba, UNHCR imefanyia tathimini kaya 150,000, na asilimia zaidi ya  90% miongoni mwao  inaripoti kuwa na mtu mmoja wa familia katika mazingira magumu, hii ni pamoja na karibu asilimia 25% ya watoto walio katika hatari.

Hawa ni watoto wasioambatana na wazazi au walezi na Watoto waliotengwa , walio nje ya shule, watoto wanaofanya kazi au watoto waliopuuzwa, wanaokabiliwa na unyanyasaji na unyonyaji.

Kulingana na UNHCR, hii inaonyesha matokeo yaliyoripotiwa na watendaji wa ulinzi wa watoto, ambao walionyesha kuwa asilimia 43 ya wanawake wako katika hatari na asilimia 25% ya wazee wanaoishi peke yao hawana msaada wa jamii.

Kwa kuongezea, kaya asilimia  32% ziliripoti kuwa na watu wenye mahitaji mbalimbali ya ulinzi, kama vile shida ya kisaikolojia, hofu ya kukamatwa au kuwekwa kizuizini na hali za unyanyasaji unaohusisha wanawake na wasichana.
"Matokeo haya ni makubwa zaidi kuliko mwaka uliopita, yakionyesha kuzorota kwa mazingira ya ulinzi kwa wale walioathiriwa zaidi na mzozo,"  limesema shirika la UNHCR.