Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wanawake wanufaika wa mradi wa WFP wakitengeneza sabuni huko Kabalo jimboni Tanganyika nchini DRC.

Nalima na kushona cherahani kujikomboa mimi na wanawake wenzangu: Mkimbizi Felicitee

© WFP/Arete/Fredrik Lerneryd
Wanawake wanufaika wa mradi wa WFP wakitengeneza sabuni huko Kabalo jimboni Tanganyika nchini DRC.

Nalima na kushona cherahani kujikomboa mimi na wanawake wenzangu: Mkimbizi Felicitee

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkimbizi Felicitee Anibati kutoka Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo ambaye kwa sasa anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Makpandu, ni mama, mkulima na mjasiriamali mwenye mafanikio ambaye sasa anawasaidia wanawake wenzie kufika alipo yeye.

Felicitee anasema aliwasili Mapandu mwaka 2018 kama mkimbizi na alipenda sana kilimo, mwaka 2020 alianza kulima mahindi na akafanikiwa kuvuna gunia 9 ambapo aliuza 4 na yaliyosalia yalimfaa kwa chakula na familia yake.

Baada ya kupitia madhila mengi ya vita Felicitee amebwaga moyo wake katika ene hili na faida anayoipata baada ya kuuza mazao akaamua kuanzisha biashara ya ujasiriamali wa ufundi cherahani unaomfaa yeye na wanawake wenzie.

“Nilinunua pia cherahani na nimejenga pia nyumba tatu kwa kutumia fedha ninazopata. Na hela kidogo iliyosalia nikaanzisha kikundi cha wanawake ambao sasa tunashona pamoja. Tunanunua vitambaa na kushona nguo ambazo tunaziuza.”

Hakuishia hapo akiba inayopatikana Felicitee akaamua kuwasaidia wanawake wengi zaidi kwa kuanzisha bekari ya kuoka na kupika vitu mbalimbali yakiwemo maandazi na hatua hiyo anasema inampa ujasiri mkubwa wa kufanyakazi kwa bidii.

Felicitee anaishukuru sana jamii inayowahifadhi kwani anasema bila upendo na ushirikiano wao asingeweza kuwa alipo, lakini pia analishukuru shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ambalo linahakikisha wakimbizi wanapata fursa waendako.