Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Madagascar watoto hawakimbii huku na kule wala kucheza, bali machungu yametawala machoni mwao

Kila mwezi WFP inatoa mgao wa chakula kwa watu 750,000 Kusini mwa Madagascar
© WFP/Krystyna Kovalenko
Kila mwezi WFP inatoa mgao wa chakula kwa watu 750,000 Kusini mwa Madagascar

Nchini Madagascar watoto hawakimbii huku na kule wala kucheza, bali machungu yametawala machoni mwao

Msaada wa Kibinadamu

Eneo la Kusini mwa Madagascar likijulikana kama ‘Grand Sud” sasalinafanana na filamu ya kisayansi ya kutungwa, ni eneo kame kabisa, hakuna mtu anaishi na limetelekezwa. Ardhi imekumbwa na mfululizo wa vipindi vya ukame. Lakini wakazi wa eneo hili wanasema mwaka huu wa 2021 hali imekuwa mbaya zaidi.

Taswira halisi tunapatiwa na afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani, WFP, Krystyna Kovalenko aliyetembelea eneo hilo ambako maelfu ya watu wanakabiliwa na njaa.

Baada ya kipindi kirefu cha mwambo, mavuno yaliyosubiriwa kw ahamu yameliwa na wadudu.
© WFP/Krystyna Kovalenko
Baada ya kipindi kirefu cha mwambo, mavuno yaliyosubiriwa kw ahamu yameliwa na wadudu.

Nilikutana na wazee ambao maisha yao yote wameishi eneo hili la kusini mwa  Madagascar. Awali walilinganisha hali ya sasa na hali ilivyokuwa wakati wa ukame wa mwaka 1991. Lakini kadri nilivyozungumza nao, walinieleza kuwa hali ya sasa ni mbaya zaidi. Mwaka huu, kipindi cha mwambo kilikuwa ni kirefu kuwahi kushuhudia, ukame ulikuwa mkali na hata mavuno kidogo ambayo yalikuwepo yalishambuliwa na wadudu na hivyo kuchukua tumaini lao la mwisho la chakula kwa miezi ijayo.
Hali ni ya kukata tamaa na haina matumaini kabisa.

Mchanganyiko wa majani na udongo ndio chakula cha watoto  

Wazee na watoto wenye utapiamlo katika maeneo ya kusini ya Madagascar wako hatarini zaidi.
© WFP/Krystyna Kovalenko
Wazee na watoto wenye utapiamlo katika maeneo ya kusini ya Madagascar wako hatarini zaidi.

Tulitembelea vijiji vidogo vilivyoko maeneo ya ndani ambavyo hata barabara zinazounganisha zimeharibika. Kile tulichoshuhudia baada ya kuwasili ni mazingira ya kuvunja moyo ya watoto waliovimba matumbo kutokana na unyafuzi au utapiamlo uliokithiri. Nilishtushwa mno na ukimya katka vijiji hivi. Watoto hawakimbii wala kucheza, wameketi tu na kututazama. Machoni mwao ni huzuni na machungu mazito.
Katika kijiji kimokja, nilimuuliza mtoto mmoja ni lini alikuwa amekula chakula na kilikuwa ni chakula gani.

Alinionesha udongo mweupe ardhini. Mama yake akanieleza kuwa kitu cha mwisho kumlisha mwanae yalikuwa majani na mimea ambayo kwa kawaida si chakula lakini alifanya hivyo kwa sababu hakukuwa na kitu kingine cha kumlisha mwanae.

Alichemsha hayo majani na mimea akaongeza udongo na kupatia watoto wake huo mchanganyiko angalau wajaze matumbo yao.

Ni dhahiri kuwa mlo huo haukuwa na lishe yoyote na wamekuwa wanakula mlo huo kwa muda mrefu. Matumbo yao yaliyovimba na mikono miembamba ni dhahiri kuwa wanachokula hakina lishe yoyote. Hii ni dhahiri miongoni mwa watoto na wazee ambao wamechoshwa na njaa. Katu sitosahau kijana ambaye hakuweza kula kabisa chakula kwa kuwa hakuwa na nguvu hata ya kushika kijiko.

Kijana huyu ilibidi alishwe chakula kwa kuwa hakuwa hata na nguvu ya kushika kijiko na kujichotea chakula
© WFP/Krystyna Kovalenko
Kijana huyu ilibidi alishwe chakula kwa kuwa hakuwa hata na nguvu ya kushika kijiko na kujichotea chakula

Kadri tulivyokuwa tunapita makazi ya watu pamoja na vijiji, watoto wengi tuliowaona walikuwa na uzito mdogo. Takribani watu milioni 1.14 kusini mwa Madagascar wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa uhakika wa kupata chakula. Takribani 14,000 wako kiwango cha 5 cha njaa na hii ni mara ya kwanza watu wamefikia kiwango hicho cha juu cha njaa tangu kipimo hicho kianze kutumika mwaka 2016.

Msimu mwingine wa mwambo ndio umeanza mwezi huu wa Oktoba na hali itakuwa mbaya zaidi.
Chanzo cha janga la sasa kusini mwa Madagascar kwa mujibu wa WFP ni ukataji miji holela na mabadiliko ya tabianchi.