Mabadiliko ya hali ya hewa kwa mfano ukame yanasababisha athari za kiuchumi miongoni mwa wakulima.

Afrika inakabiliwa na hatari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi:WMO

UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Mabadiliko ya hali ya hewa kwa mfano ukame yanasababisha athari za kiuchumi miongoni mwa wakulima.

Afrika inakabiliwa na hatari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi:WMO

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika mbalimbali na kuratibiwa na shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO imesema mabadiliko ya mifumo ya mvua, kuongezeka kwa joto na hali mbaya ya hewa kumechangia kuongezeka kwa ukosefu wa chakula, umaskini na watu kutawanywa barani Afrika mwaka 2020 huku hali mbaya ikizidishwa nachangamoto za kijamii, kiuchumi na kiafya ziliyosababishwa na janga la COVID-19.

Ripoti hiyo “Hali ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika 2020” inaangazia hatari inayolikabili bara hilo lakini pia inaonyesha jinsi uwekezaji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mifumo ya tahadhari mapema, na huduma za hali ya hewa, vinaweza kuwa na faida. 

Petteri Taalas, katibu mkuu wa WMO, amesema viashiria vya hali ya hewa barani Afrika wakati wa mwaka jana vilidhihirisha hali ya joto linayoendelea kuongezeka, kupanda kwa kasi kwa kina cha bahari, hali yam baya ya hewa, na matukio mabaya ya hali ya hewa kama vile mafuriko, maporomoko ya ardhi na ukame. 

Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania kama unavyoonekana kutoka nchini Kenya
World Bank/Curt Carnemark
Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania kama unavyoonekana kutoka nchini Kenya

Kupungua kwa barafu 

Ripoti imeonya kwamba "Kupungua kwa kasi kwa barafu za mwisho zilizobaki mashariki mwa Afrika, ambazo zinatarajiwa kuyeyuka kabisa katika siku za usoni, kunaashiria tishio la mabadiliko ya tabianchi yasiyoweza kurekebishwa kwa mfumo wa dunia”. 

Milima mitatu tu barani Afrika imefunikwa na barafu ambayo ni mlima Kenya, Mlima Rwenzori nchini Uganda, na Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania. Ingawa barafu ni ndogo sana kuweza kuchukua nafasi ya hifadhi kubwa za maji, WMO ilisisitiza umuhimu wake katika utalii na kisayansi. 

Hivi sasa, viwango vya kupungua kwa barafu hiyo ni vya juu kuliko wastani wa kimataifa na kutoweka kabisa kwa barafu kunawezekana ifikapo miaka ya 2040. 

“Barafu katika mlima Kenya inatarajiwa kuisha kabisa miaka 10 mapema zaidi ya ilivyotarajiwa hapo awali,” limesema shirika la WMO likiongeza kuwa “hali hiyo  itaifanya mlima huo kuwa moja ya safu za kwanza za milima kupoteza kabisa kifuniko cha barafu kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za binadamu.” 

Ukame na umasikini umesababisha njaa kali kusini mwa Madagascar
© WFP/Tsiory Andriantsoarana
Ukame na umasikini umesababisha njaa kali kusini mwa Madagascar

Mamilioni wako hatarini 

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya WMO, tume ya Muungano wa Afrika AU, Tume ya uchumi ya Afrika (ECA) kupitia kituo cha sera za hali ya hewa Afrika (ACPC), mashirika ya Umoja wa Mataifa , na mashirika ya kisayansi ya kimataifa na ya kikanda. 

Imetolewa wakati wa kikao cha mkutano mkuu wa WMO unaoendelea mtandaoni, kabla ya kuanza kwa mkutano wa COP26 wa mabadiliko ya tabianchi, ambao unafunguliwa huko Glasgow, Scotland, chini ya wiki mbili zijazo. 

Kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi kunavuruga maisha na uchumi, amesema Joseph Leonel Correia Sacko, kamishna wa uchumi vijijini na kilimo wa tume ya Muungano wa Afrika. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WMO, makadirio yanafafanua kuwa ifikapo mwaka 2030, hadi watu milioni 118 maskini kabisa barani Afrika watakabiliwa na ukame, mafuriko na joto kali, matukio ambayo ytazuia maendeleo ya kuelekea kupunguza umaskini na ukuaji wa uchumi. 

"Katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kupunguza zaidi pato la taifa (GDP) kwa hadi asilimia 3%, ifikapo mwaka 2050," ameongeza. 

"Hii inaleta changamoto kubwa kwa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na vitendo vya kuyathabiti kwa sababu sio tu hali za maisha zinazidi kuwa mbaya, lakini pia idadi ya watu wanaoathiriwa inaongezeka." 

Ripoti hiyo ilikadiria kuwa uwekezaji katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ungegharimu kati yadola bilioni  $ 30 hadi $ 50 kila mwaka kwa miaka kumi ijayo, au asilimia mbili hadi tatu ya pato la taifa, DGP. 

Waandishi wa ripoti hiyo wamesema utekelezaji wa haraka wa mikakati ya kukabiliana na hali hiyo Afrika utachochea maendeleo ya kiuchumi, na pia kuongeza ajira zaidi kama sehemu ya kujikwamua na janga la COVID-19

Kufuatilia vipaumbele vya mpango wa Muungano wa Afrika wa kujikwamua kwa kuzingatia mazingira pia utaruhusu kujikwamua ambako ni endelevu lakini pia kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.