Skip to main content

Mkataba wa amani Sudan Kusini bado kitendawili kwa wakazi wa Tambura

Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini
UNMISS
Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini

Mkataba wa amani Sudan Kusini bado kitendawili kwa wakazi wa Tambura

Amani na Usalama

Licha ya kutiwa saini kwa makubaliano mapya ya amani nchini Sudan Kusini mwaka 2018, mapigano bado yanaendelea katika maeneo tofauti tofauti nchini humo ikiwemo mji wa Tambura jimboni Equatoria Magharibi na hivyo kukwamisha harakati za kufikisha huduma za matibabu na wakimbizi wa ndani kuzidi kutaabika.

Video ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS inaanza kwa taswira ya uharibifu katika kituo cha afya mjini Tambura, uharibifu uliofanywa na vikundi vilivoyjihami.

Ili kuendeleza huduma za afya, UNMISS imeanzisha kambi ya muda katika eneo hilo na  wananchi wanaokimbia machafuko katika vijiji vyao wanapata hifadhi na huduma nyingine muhimu lakini changamoto sasa ni huduma ya afya.

Halawia Martin, muuguzi katika katika eneo hilo la Tambura. “Hospitali imeharibiwa hasa wodi za wanawake, wanaume, maabara na wodi ya uzazi. Kila kitu kimeibwa. Darubini za kuchunguza ugonjwa nazo zimeharibiwa, dawa za virusi vya ukimwi VVU na mashine ya kupima wagonjwa wa VVU na kifua kikuu pia ziliharibiwa. Sasa, tunakabiliwa na changamoto kwa sababu ya vita hii, tunakufa kwa sababu ya ukosefu wa dawa. Watoto wanaougua malaria hawawezi kutibiwa. ” 
  
Na vipi kuhusu huduma za wagonjwa wasiolazwa ? "Hatuna huduma ya wagonjwa kwa wagonjwa wasiolazwa hapa kambini. Huduma iko mbali na ikiwa mtu ni mgonjwa hatuwezi kusaidia. Hatuwezi kwenda kwenye kituo cha afya kwa sababu hakuna usalama. Huduma kwa wagonjwa hao inahitajika kwa watoto wenye utapiamlo. Mtoto kutoka idara ya wagonjwa wasiolazwa kwa kawaida hupelekwa kwenye Kituo cha uangalizi lakini hatuna chochote sasa. Vifaa vyote vimeharibiwa. Kwa hivyo, ni ngumu sana. " 
 
Marcello Danyeso ni afisa ufuatiliaji katika kaunti hii na anasema ni vigumu kupata rufaa kwa sababu ijapokuwa wanalo gari la kusafirishia wagonjwa, bado hawawezi kuwasafirisha wagonjwa kuwapeleka Yambio kutokana na barabara kutokuwa salama.

"Hivi sasa tunafanya kile tunachoweza kwa sababu hatuna vifaa vyote, kama maabara ya kumuongezea mtu damu." Maabara inatumika kufanya uchunguzi na kumpatia mgonjwa. Vifaa vyetu vya maabara viliharibiwa vyote. Hivi sasa tunachofanya hapa ni kufanya uchunguzi wa haraka wa malaria.” 

Wakati UNMISS na washirika wengine wa masuala ya kibinadamu wakifanya kila wawezalo kuwaweka watu salama na kuhakikisha mahitaji yao ya kimsingi yanatimizwa, maafisa wa kaunti hapa Tambura wanasema ukosefu wa utulivu una athari mbaya kiafya kwa waliokimbia makazi yao.