Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia inasaidia vijana kusambaza bidhaa wanazotengeneza

Mawe ya Jasi tayari yamepondwa yakisubiri kusagishwa kuwa unga unaotumika kutengeneza chaki za ubaoni na mikanda ya jasi ya kupamba dari za nyumba.
UN
Mawe ya Jasi tayari yamepondwa yakisubiri kusagishwa kuwa unga unaotumika kutengeneza chaki za ubaoni na mikanda ya jasi ya kupamba dari za nyumba.

Teknolojia inasaidia vijana kusambaza bidhaa wanazotengeneza

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania vijana wajasiriamali katika mkoa wa Singida wameitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, TEHAMA kama njia mojawapo ya kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu, SDG hususan kipengele cha teknolojia cha lengo namba 17 la kuimarisha mbinu za utekelezaji wa malengo na kuchochea ubia wa kimataifa.

Miongoni mwa vijana hao ni mjasiriamali Simon Sirillo ambaye akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, amesema,“Kwa mfano mimi ninazalisha unga wa jasi au gypsum tunachaka jasi kwa maana kwamba tunatengenza chaki na unga wa mikanda ya kupamba au ujenzi wa  dari za nyumba. Huu ni ubunifu lakini bila kutumia TEHAMA tunaweza kuishia kuzalisha tu na tusifanikiwe. Kwa hiyo teknolojia inatakiwa katika ubunifu wetu tulio nao, kwa maana tunatumia gharama ndogo za uzalishaji na viwanda vyetu ni vidogo. Ili tuweze kwenda mbali zaidi tunahitaji kutumia teknolojia ili kukuza ubunifu wetu na uvumbuzi wetu kwa ujumla.”

Kwa hivyo akatoa wito kwa vijana wenzake akisema, "tuangalie ni kwa namna gani tunaweza kwenda sambamba na TEHAMA. ili tuweze kufanikiwa katika mambo yetu hatupaswi kuicha mbali Teknolojia kwa sababu inatusaidia kutengeneza mizigo yetu, bidhaa zetu, kuzisambaza na kuziuza ndani ya jamii yetu, ndani ya nchi yetu na hata nje ya nchi kwa ujumla.”

Lengo namba 17 la SDGs lina mbinu mbalimbali za kuwezesha kufanikisha malengo yote ya maendeleo endelevu na teknolojia ni miongoni mwa mbinu hizo ambapo Umoja wa Mataifa kupitia wavuti wa SDGs unasema teknolojia rahisi na rafiki kwa mazingira “zinawezesha kuchagiza biashara na hivyo kuchangia katika kutokomeza umaskini.”