Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zikiripotiwa Eswatini, Guterres asihi pande kinzani zijadiliane

Mfalme Mswati III wa Ufalme wa Eswatini wakati akihutubia Baraza Kuu la un mwezi Septemba mwaka 2019
UN/Cia Pak
Mfalme Mswati III wa Ufalme wa Eswatini wakati akihutubia Baraza Kuu la un mwezi Septemba mwaka 2019

Ghasia zikiripotiwa Eswatini, Guterres asihi pande kinzani zijadiliane

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa kile kinachoendelea nchini Eswatini, ikiwemo hatua ya hivi karibuni ya kupelekwa kwa wanajeshi katika shule mbalimbali nchini humo.

Nini kinaendelea Eswatini

Kwa mujibu wa vyombo vya  habari, wanafunzi kwa zaidi ya wiki mbili nchini Eswatini wamekuwa wakiandamana  kudai demokrasia, maandamano ambayo pia yanaripotiwa kujumuisha wafanyakazi wa usafirishaji na wachuuzi wa mitaani.

Shule zimefungwa leo jumatatu baada ya serikali kutangaza mwishoni mwa wiki kuwa zitafungwa kwa kipindi kisichojulikana.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema Katibu Mkuu anatiwa hofu pia na ripoti ya matumizi ya nguvu kupita kiasi kufuatia maandamano yanayofanywa na wanafunzi nchini humo sambamba na kufungwa kwa shule kwa kipindi kisichojulikana.

Wito wa Guterres

“Kitendo hiki kinaathiri vibaya watoto na vijana. Nasisitiza umuhimu wa kuwezesha wananchi wa Eswatini kutekeleza haki zao za kiraia na kisiasa kwa amani. Nasihi serikali ihakikshe kuwa vikosi vya usalama vinatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu ikiwemo mkataba wa kimataifa kuhusu haki za mtoto, CRC,” amenukuliwa Katibu Mkuu Guterres.

Bwana Guterres pia amelaani aina zote za ghasia na vurugu na kusihi pande zote sambamba na vyombo vya habari wajizuie kusambaza taarifa zisizo za kweli, kauli za chuki na za kichochezi.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kushirikiana na serikali ya Eswatini na wanachi wake pamoja na wadau wote katika kusaka suluhu kwa njia ya amani.