Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Drogba kupeperusha bendera ya WHO kupitia michezo kwa afya

Didier Yves Drogba Tébily, mwanasoka mashukuru duniani kutoka Côte d’Ivoire.
UN/maktaba
Didier Yves Drogba Tébily, mwanasoka mashukuru duniani kutoka Côte d’Ivoire.

Drogba kupeperusha bendera ya WHO kupitia michezo kwa afya

Afya

Mwana kandanda mashuhuri duniani kutoka nchini Côte d’Ivoire, Didier Drogba leo ametangazwa kuwa balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO akijikita katika michezo kwa ajili ya afya, halikadhalika kumulika thamani ya michezo hususan kwa vijana.
 

Drogba anayetambulika kwa uchezaji soka wa kulipwa akiwa timu ya Chelsea ya Uingereza na mshindi mara mbili wa tuzo ya mchezo bora wa mwaka barani Afrika 2006 na 2009 amekuwa na rekodi ya muda mrefu ya kushiriki katika kampeni za afya kama vile mifumo ya maisha yenye afya, kampeni dhidi ya ugonjwa wa Malaria na pia dhidi ya Ukimwi.

Nitachagiza michezo kwa afya duniani- Drogba

Uteuzi wake wa kushika wadhifa huo umetangazwa leo huko Geneva, Uswisi na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya afya kwa ajili ya mashindano ya kombe la dunia la soka huko Qatar mwaka 2022.

Mwanasoka mashuhuri duniani Didier Drogba ametangazwa kuwa Balozi Mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO
WHO/Christopher Black
Mwanasoka mashuhuri duniani Didier Drogba ametangazwa kuwa Balozi Mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO

Akizungumza baada ya kutangazwa, Drogba amesema, “ni heshima kubwa kwangu kuungana na WHO na kuunga mkono kazi yake ya kusaidia watu kufikia kiwango cha juu kinachowezekana cha afya, hususan kwa vijana. Nimefaidika na kushuhudia uwezo wa michezo katika kuishi maisha yenye afya na nimejizatiti kufanyakazi na WHO katika mchakato huu duniani kote.” 

Kwa upande wake Dkt. Tedros amempongeza Drogba akisema “yeye si tu mwanasoka mashuhuri bali pia amejitolea kuchagiza afya na maendeleo endelevu ya jamii na hivyo kuunga kwake WHO kunaweza kusaidia kupunguza ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs kupitia uchechemuzi wa mifumo ya maisha inayozingatia afya bora ikiwemo kufanya mazoezi na michezo kwa wote.”

Bingwa ndani na nje ya uwanja

"Didier amethibitisha kuwa ni bingwa na mleta mabadiliko ndani na nje ya uwanda wa mpira, tunafurahi sana yeye kuwa mchezaji ndani ya timu yetu na kusaidia jamii duniani kote kufunga magoli kupitia michezo kwa ajili ya afya ya mwili na akili,” amesema Dkt. Tedros akiongeza kuwa Drogba atasaidia pia kuhamasisha jamii ya kimataifa kusongesha michezo kama mbinu muhimu ya kuimarisha afya ya mwili na akili kwa ustawi wa watu wote sambamba na kusaidia juhudi za kujikwamua kutoka katika janga la Corona au COVID-19.

Mwanasoka mashuhuri duniani Didier Drogba (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus baada ya kutangazwa hii leo huko Geneva, USwisi  kuwa balozi mwema wa shirika hiilo
WHO/Christopher Black
Mwanasoka mashuhuri duniani Didier Drogba (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus baada ya kutangazwa hii leo huko Geneva, USwisi kuwa balozi mwema wa shirika hiilo

Takwimu zinatisha

Takwimu za sasa zinaonesha kuwa barubaru 4 kati ya 5 na mtu mzima 1 kati ya 4 hafanyi mazoezi. “ukosefu wa mazoezi ya mwili unaathiri mifumo ya afya, mazingira, maendeleo ya uchumi, ustawi wa jamii na maisha bora. Mazoezi ya mara kwa mara ikiwemo kupitia michezo kunasaidia kupunguza shinikizo la dam una hatari ya kupata mshtuko wa moyo, kisukari na magonjwa mengine ya saratani,” imesema WHO.
Drogba anaungana na mabalozi wengine wa WHO akiwemo bingwa wa soka kutoka Brazil, Alisson Becker;  muasisi wa wakfu wa Bloomberg, Michael Bloomberg ambaye pia amewahi kuwa Meya wa jiji la New York, nchini Marekani, na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown.