Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Msichana mdogo anashikilia ishara inayosema Zo Kwe Zo, wito wa kitaifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,  ikimaanisha kuwa wanadamu wote ni sawa.

UN yapongeza tangazo la kusimamisha mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

OCHA/Yaye Nabo Sène
Msichana mdogo anashikilia ishara inayosema Zo Kwe Zo, wito wa kitaifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikimaanisha kuwa wanadamu wote ni sawa.

UN yapongeza tangazo la kusimamisha mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza tangazo la upande mmoja la kusitisha mapigano katika eneo lote la Jamhuri ya Afrika ya Kati – CAR kuanzia tarehe 15 Oktoba 2021, lililotangazwa leo na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadéra.

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wake Stéphane Dujarric imeeleza kuwa Katibu Mkuu amekaribisha hatua hiyo muhimu, ambayo inaendana na mipango ya pamoja ya amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati iliyopitishwa na mkutano wa kimataifa juu ya ukanda wa Maziwa Makuu mnamo tarehe 16 Septemba.

Dujarric ameeleza kuwa “Katibu Mkuu ametoa wito kwa wahusika wote nchini humo na makundi mengine yote kuheshimu mara moja usitishwaji huu wa mapigano na kurejesha juhudi za kuendeleza utekelezaji wa Mkataba wa Kisiasa wa 2019 wa Amani na Upatanisho.”

Pia anahimiza pande zote kushirikiana kwenye mazungumzo kwa lengo la kujenga na kuwa na ujumuishi wa kisiasa kwa nia ya kufanya maendeleo yanayoonekana katika mchakato wa amani na upatanisho katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameahidi kuendekea kujitolea kuhamasisha jamii ya kimataifa kusaidia Serikali na watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika harakati zao za amani, upatanisho, na maendeleo.