Skip to main content

Je chakula ulacho kinalinda afya yako na sayari dunia au ndio kinasambaratisha? 

Robo ya chakula kinachozalishwa hakitumiki
FAO/Giulio Napolitano
Robo ya chakula kinachozalishwa hakitumiki

Je chakula ulacho kinalinda afya yako na sayari dunia au ndio kinasambaratisha? 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo tarehe 16 mwezi Oktoba ni siku ya chakula duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, anasema siyo siku tu ya kukumbushana umuhimu wa chakula kwa kila mkazi wa dunia, bali ni siku ya kutoa wito wa kufanikisha uhakika wa kila mtu kuwa na chakula. 

Mifumo ya uzalishaji chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.
© FAO/Petterik Wiggers
Mifumo ya uzalishaji chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.

"Hii leo takribani asilimia 40 ya wakazi wa dunia, sawa na watu bilioni 3 hawana uwezo wa kupata mlo wenye afya, njaa inaongezeka halikadhalika utapiamlo na utipwatipwa,” anasema Katibu Mkuu kupitia ujumbe wake wa siku ya leo. 

Madhara ya kiuchumi kutokana na ugonjwa wa Corona au COVID-19 yamefanya hali kuwa mbaya zaidi na janga limeongeza watu wengine milioni 140 wasio na uwezo wa kupata chakula wanachohitaji. 

Na wakati huo huo, vile ambavyo chakula kinazalishwa, kinaliwa na vile vile kutupwa kinasababisha madhara makubwa katika sayari ya dunia. 

Kikundi cha wanawake mkoani Kigoma nchini Tanzania wakiwa kwenye mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za vyakula kwa kutumia viazi lishe.
FAO Tanzania
Kikundi cha wanawake mkoani Kigoma nchini Tanzania wakiwa kwenye mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za vyakula kwa kutumia viazi lishe.

“Hii inaongeza shinikizo la kihistoria katika rasilimali zetu za asili, tabianchi na mazingira asilia na kutugharimu matrilioni ya dola kila mwaka,” amesema Guterres. 

Katibu Mkuu anasema kupitia maudhui ya mwaka huu ya siku ya chakula duniani ambayo ni “Matendo yetu ndio mustakabali wetu,”  ni dhahiri kuwa jamii uwezo wa kuleta mabadiliko uko mikononi mwa binadamu. 

Amerejelea mkutano wa mwezi uliopita kuhusu mifumo ya vyakula ambapo viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walikutana na kupitisha ahadi za kijasiri za kurejebisha mifumo ya chakula. 

Wanawake wakishiriki kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi nchini Bangladesh
UNDP Bangladesh
Wanawake wakishiriki kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi nchini Bangladesh

Lengo likiwa ni kuhakikisha vyakula bora na vyenye lishe vinapatikana kwa kila mtu. Halikadhalika ,mifumo hiyo ya uzalishaji chakula kuanzia shambani hadi mezani iwe na tija zaidi, yenye mnepo na endelevu. 

“Tunaweza sote kubadili vile ambavyo tunakula chakula, na kuwa na chaguo la kiafya zaidi kwa ajili yetu na kwa sayari yetu,” amesema Katibu Mkuu akitanabaisha kuwa kupitia mifumo ya uzalishaji chakula, kuna matumaini. 

Na hivyo “katika siku ya chakula duniani, ungana nasi tunapoahidi kuchukua hatua za kimabadiliko ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu kupitia mifumo bora ya uzalishaji chakula ambayo inatoa hakikisho la lishe bora, mazingira bora na maisha bora kwa kila mtu.”