Nini kifanyike sekta ya usafirishaji ifanikishe Ajenda 2030? Guterres afunguka

14 Oktoba 2021

Sekta ya usafirishaji duniani bado inaendelea kuchangia katika utoaji wa gesi chafuzi duniani na hivyo kukwamisha  harakati za kufikia malengo ya kupunguza ongezeko la joto kutozidi nyuzi 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa kauli hiyo kwa njia ya video hii leo wakati akihutubia mkutano wa pili wa kimataifa kuhusu usafirishaji endelevu duniani ulioanza leo huko Beijing China.
 

Guterres amesema ingawa katika kipindi cha miezi 18 janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limepunguza usafiri wa njia ya barabara kwa asilimia 50 huku ule wa anga ukipungua kwa theluthi moja ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, na hivyo kumaanisha ajali chache za  barabarani, hewa safi na kupungua kwa utoaji wa hewa chafuzi, mafanikio hayo hayakuwa endelevu.

“Usafirishaji ambao unachangia zaidi ya robo ya hewa chafuzi duniani, ni muhimu katika kurejea katika mwelekeo sahihi. Lazima tupunguze matumizi ya hewa chafuzi katika njia zote za usafirishaji ili tuweze kufikia lengo la kutotoa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050,” amesema Katibu Mkuu

Ameongeza kuwa ingawa nchi wanachama kupitia shirika la kimataifa la usalama wa anga, ICAO  na lile la usafirishaji majini, IMO, zimechukua hatua za awali za kushughulikia utoaji wa hewa chafuzi katika sekta ya usafirishaji majini na angani, bado vipaumbele vyao haviendani na lengo la kuhakikisha joto halizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kwa mujibu wa Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia mkutano wa usafirishaji huko Beijing kwa njia ya Video kutoka New York, Marekani.
UN China Office/ Zhao Yun
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia mkutano wa usafirishaji huko Beijing kwa njia ya Video kutoka New York, Marekani.

Nini kifanyike usafirishaji nao uchangie SDG?

Guterres akaona ataje mambo muhimu ya kurejesha sekta ya usafirishaji katika mwelekeo wa makubaliano ya Paris akisema, “mosi, kuondokana na utengenezaji wa injini za magari zinazotumia nishati chafuzi kama vile mafuta ya dizeli ifikapo mwaka 2035 katika nchi za viwanda na kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2040. Kwa upande wa meli, suala la kuwa na meli zisizotoa hewa chafuzi ndio iwe chaguo pekee na ziwepo ifikapo mwaka 2030 ili ifikapo mwaka 2050, sekta ya usafirishaji majini iwe haitoi kabisa hewa chafuzi.”

Halikadhalika kampuni za usafirishaji wa anga zianze kutumia nishati endelevu ili kupunguza kwa asilimia 65 kiwango cha uchafuzi wa hewa zitolewazo na ndege za abiria ifikapo mwaka 2050.

Katibu Mkuu amesema kila mdau ana jukumu la kufanya kuanzia mtu mmoja mmoja kubadili tabia za safari hadi sekta ya wafanyabiashara ili kurekebisha mfumo wa utoaji wa hewa ya ukaa.

Alama za barabarani pamoja na taa za kuongoza magari na waenda kwa miguu ni moja ya mambo ya kuwezesha waenda kwa miguu kuwa na amani kutembea na hivyo kupunguza matumizi ya magari kama pichani huko San Francisco nchini Marekani.
Unsplash/Yoel J Gonzalez
Alama za barabarani pamoja na taa za kuongoza magari na waenda kwa miguu ni moja ya mambo ya kuwezesha waenda kwa miguu kuwa na amani kutembea na hivyo kupunguza matumizi ya magari kama pichani huko San Francisco nchini Marekani.

Serikali kwa upande wake ziweke motisha kwa wale wanaotumisha usafiri usiochafua mazingira ikiwemo kodi nafuu na kuweka kanuni kali kwenye miundombinu ya usafiri na manunuzi ya vifaa vya usafiri na usafirishaji.

Pendekezo la pili ni kuondoa pengo la kupata barabara bora na salama akisema “kusaidia zaidi ya watu bilioni 1 kuweza kuwa na barabara zilizotengenezwa vizuri na maeneo ya watembea kwa miguu na waendesha baiskeli na kuwepo pia na usafiri wa umma wa kuaminika.”

Tatu, ni kujenga mnepo katika mifumo ya usafirishaji akimaanisha “uwekezaji katika kujikwamua dhidi ya COVID-19 lazima ulenga usafirishaji endelevu na kutoa fursa za ajira zenye hadhi na fursa kwa jamii zilizo pembezoni. Usafiri wa umma lazima uwe msingi wa mienendo ya safari mijini. Kila dola inayowekezwa kwenye barabara ya kawaida, inafungua fursa mara tatu zaidi za ajira badala ya kujenga barabara mpya kuu.”

Mkutano wa pili wa kimataifa wa sekta ya usafirishaji endelevu duniani ulifanyika miaka mitano iliyopita huko Ashgabat, Turkmenistan.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter