Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatuza familia ya mmarekani mweusi ambaye seli zake zilitumika kisayansi

Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus anaikaribisha familia ya Henrietta Lacks kwa mazungumzo maalum katika makao makuu ya WHO huko Geneva na kuwakabidhi tuzo maalimu kwa mchango wa Henrietta Lacks
WHO
Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus anaikaribisha familia ya Henrietta Lacks kwa mazungumzo maalum katika makao makuu ya WHO huko Geneva na kuwakabidhi tuzo maalimu kwa mchango wa Henrietta Lacks

UN yatuza familia ya mmarekani mweusi ambaye seli zake zilitumika kisayansi

Haki za binadamu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, Dokta Tedros Ghebreyesus ametoa tuzo maalum kwa marehemu Henrietta Lacks mwanamke mmarekani mwenye asili ya Afrika kutokana na seli zake kubadili ulimwengu wa sayansi ya matibabu baada ya kutumika kufanya utafiti wa saratani ya kizazi. 

Katika hafla maalum iliyofanyika mjini Geneva Uswisi Dkt. Tedros ameikabidhi tuzo hiyo kwa mtoto wa Henrietta Lacks, Lawrence Lacks pamoja na wanafamilia wengine na kueleza shirika lake limeamua kutoa tuzo hiyo ikiwa ni ishara ya shukran kwa namna seli hizo zilivyoweza kusaidia dunia lakini pia ni njia ya WHO kukiri mabaya yaliyofanyika kwa mama huyo ambaye seli hizo zilichukuliwa bila ridhaa yake na kufanywa siri kwa muda mrefu. 
 
Dokta Tedros amesema “simulizi ya Henrietta Lacks imetolewa na watu mbalimbali kwa namna mbalimbali huku wengi wao wakijaribu kuficha jina lake na asili yake ya Afrika ndio maana hii leo WHO tumeamua kutoa tuzo hii mbele ya familia yake, ili familia iweze kueleza kwa maneno yao wenyewe kwa kuwa WHO inaamini alichofanyiwa Henrietta si sawa” 
 
Henrietta Lacks alifariki tarehe 4 mwezi Oktoba mwaka 1951, sawa na miaka 70 iliyopita  kwa ugonjwa wa saratani ya kizazi akiwa na umri wa miaka 31. 
 
Wakati akipatiwa matibabu seli zake zilichukuliwa na kufanyiwa utafiti maabara, ambapo zimeweza kutoa chanjo ya saratani ya kizazi, kutumika katika kutafuta chanjo ya Corona na magonjwa mengine mengi pamoja na vipodozi. 

Sababu za WHO kutoa Tuzo 

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO ametaja maeneo matatu ambayo wameona si sawa na hivyo kuamua kutoa tuzo hiyo ikiwa ni njia mojawapo ya kutambua mchango wake.

Mosi, aliishi katika muda ambao ubaguzi wa rangi ulikuwa halali katika jamii. “Ubaguzi wa rangi unaweza kuwa si halali katika jamii nyingi kwa sasa lakini bado umetapakaa katika nchi nyingi” amesema Dkt. Tedros. 
 
Pili Henrietta Lacks alifanyiwa unyonywaji. Yeye ni mmoja kati ya wanawake wengi wa rangi ambao miili yao ilitumika vibaya kwa ajili ya sayansi. “Aliweka imani yake kwenye mfumo wa afya ili aweze kupata matibabu lakini mfumo ukachukua kitu kutoka kwake bila ya yeye kujua wala kutoa ridhaa.” 
 
Na tatu Teknolojia ya matibabu, utaalamu wa matibabu kiteknolojia uliozalishwa kutokana na ugunduzi kwa kutumia seli walizochukua kwa Henrietta Lacks umeendelea kutumika kwa udhalimu zaidi kwasababu hausambazwi kwa haki duniani kote. 
 
Dokta Tedros amesema “Seli za Henrietta ndio zimekuwa msingi wa ugunduzi wa chanjo dhidi  ya virusi vinavyosababisha saratani ya kizazi, au HPV ambayo inaweza kuondoa saratani ile ile ya kizazi iliyomletea umauti lakini kwenye nchi zenye kiwango kikubwa chanjo dhidi ya saratani ya kizazi hazipatikani kwa kiwango kinachotakiwa.” 
Ameongeza kuwa si saratani pekee, seli zake zimeendelea kutumika kwa miaka zaidi ya 70 na mpaka sasa zinaendelea kutumika. 
 
“Seli zake pia zimetumika kwenye utafiti kuhusu COVID-19 kutafuta mbinu za kusambaratisha janga hili lakini chanjo hazisambazwi kwa usawa kwa nchi za uchumi wa chini na wakati”. 

Familia ya Henrietta Lacks 

Akizungumza kwa niaba ya familia, Victoria Baptiste ambaye ni kitukuu wa Henrietta Lacks amesema wanaishukuru WHO kwa kutoa heshima ya haki kwa familia yao. 

“Tunashukuru sana kwa kutambuliwa huku kihistoria kwa mchango wake, na heshima aliyopewa sababu ya matokeo chanya na ya kushangaza ya seli zake ambayo yamekuwa na mchango wa kudumu. Mchango wa Henrietta ambao mwanzo ulikuwa umefichwa sasa unapewa heshima anayostahili duniani kote.” 

Familia hiyo imemshukuru Dkt Tedros Ghabreyesus pamoja na madaktari wote WHO kwa kutambua mema yote yaliyofanywa na seli zilizochukuliwa kwa Henrietta Lacks.