Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe 26 wapendekezwa kushauri WHO kuhusu vijidudu vipya, wananchi toeni maoni

Mfano wa virusi vya corona
Centers for Disease Control and Prevention
Mfano wa virusi vya corona

Wajumbe 26 wapendekezwa kushauri WHO kuhusu vijidudu vipya, wananchi toeni maoni

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, leo limetangaza jopo pendekezwa la watu 26 litakalopatia ushauri wa kisayansi shirika hilo kuhusu asili ya vijidudu na virusi vipya ikiwemo vile vinavyosababisha ugonjwa wa Corona, COVID-19.
 

Jopo hilo kwa kifupi, SAGO, litashauri WHO juu ya kuandaa mfumo mpya duniani wa kuainisha na kuongoza tafiti kuhusu vyanzo vya vijidudu vipya na vile vinavyorejea huko na vyenye uwezo wa kusababisha majanga au kusalia muda mrefu duniani.

Akitangaza jopo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema wajumbe hao 26 ni miongoni mwa majina zaidi ya 700 yaliyopendekezwa na umma kufuatia tangazo la shirika hilo la kutaka mapendekezo ya wataalamu na wamechaguliwa kutokana na ujuzi na ubobezi wao katika nyanja mbalimbali pamoja na maeneo ya kijiografia na kijinsia.

Madaktari wakimpa huduma mgonjwa wa virusi vya corona, COVID-19
Yang Yi
Madaktari wakimpa huduma mgonjwa wa virusi vya corona, COVID-19

“Kutambua wapi vijidudu vipya vinatokea ni muhimu katika kuzuia milipuko ya siku za usoni yenye uwezo wa kusalia muda mrefu duniani na inahitaji utaalamu wa aina tofauti tofauti.” Amesema Dkt. Tedros.

Akifafanua jukumu la SAGO, Dkt. Maria Van Kerkhove ambaye ni mshauri wa kiufundi WHO kuhusu COVID-19 amesema jopo hilo linapaswa kufanya tathmini ya haraka kuhusu “hapa tulipo, kile tunachofahamu na ambacho hatufahmau na kipi kinapaswa kufanyika haraka.”

Dkt. Maria amesema kufuatia ujumbe wa mwisho wa WHO nchini China wakati wa kutathmini chanzo cha COVID-19, “kulikuwepo na zaidi ya makumi kadhaa ya mapendekezo ya tafiti zinazopaswa kufanywa. Tunatumai kupata taarifa mpya kuhusu tafiti hizo ili hatimaye tuweze kusema sasa kitakachofuatia ni hiki. Kwa hiyo jopo hili litashauri WHO kuhusu hatua hizo za haraka zinazopaswa kufuata na WHO itashirikiana na nchi yoyote mwanachama ikiwemo China kufanya kila kinachopaswa kufanyika.”

Amesisitiza kuwa SAGO siyo ujumbe mwingine wa WHO akifafanua kuwa, “kumekuwepo na sintofahamu kuhusu hilo. SAGO ni jopo la ushauri kwa WHO na bila shaka watatoa mapendekezo kuhusu timu zozote zinazotakiwa kuundwa, na kumbuka SAGO si kwa ajili ya janga la sasa, bali kwa majanga yoyote au milipuko yoyote ijayo.”

Kwa mujibu wa mchakato wa WHO, kutakuwepo na mashauriano ya wiki mbili na wananchi ambapo shirika hilo litapokea maoni juu ya wajumbe pendekezwa.

Iwapo mtu anataka kutoa maoni kuhusu wajumbe hao awe amefanya hivyo kupitia anwani pepe SAGO@who.int hadi tarehe 27 mwezi huu wa Oktoba.

Wajumbe hao wanatoka nchi mbalimbali akiwemo Dkt. Rosemary Sang wa Kenya ambaye anafanya kazi katka taasisi ya taifa ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu, KEMRI.