Tumejenga mfumo wa ulimwengu ambao unaongeza mgawanyiko kati ya mataifa – Uhuru Kenyatta
Tumejenga mfumo wa ulimwengu ambao unaongeza mgawanyiko kati ya mataifa – Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye ndiye ameongoza kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo tarehe 12 Oktoba 2021 kutokana na kwamba nchi yake ndio inakalia kiti cha urais wa Baraza hilo, amesema mizozo mingi ni kutokana na malalamiko yasiyosimamiwa vizuri.
Akiongea na waandishi wa habari nje ya Baraza, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema, "nchi nyingi leo zinaonekana kutoweza kusimamia utofauti. Tumejenga mfumo wa ulimwengu ambao unaongeza mgawanyiko kati ya mataifa lakini pia ndani ya mataifa. Mfumo ambao unaamini kuna jamii au jinsia ambazo ni duni, au bora, au dini zilizo karibu na Mungu kuliko nyingine. Kwa hivyo, hali nyingi za mizozo mbele ya Baraza letu la Usalama ni matokeo ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja ya malalamiko yaliyosimamiwa vibaya. "
Hapo awali katika Baraza, Katibu Mkuu António Guterres ameliambia Baraza la Usalama kwamba "bila kujumuisha mawanda mapana ya sauti tofautitofauti katika kila hatua" ya ujenzi wa amani, "amani yoyote itakuwa ya muda mfupi."
Bwana Guterres akihutubia mjadala wa wazi kuhusu utofauti, ujenzi wa serikali na utafutaji wa amani, mjadala ulioandaliwa na Kenya amesema, "amani haipatikani kwenye karatasi. Inapatikana kwa watu. Hasa, utofauti wa watu kutoka asili tofauti wanakusanyika pamoja ili kupanga masuala ya kawaida kwa ajili ya nchi. "
Aidha Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, "wakati kukosekana kwa usawa kupo katika kila nchi, hali hiyo ni kubwa zaidi katika nchi ambazo huduma za kijamii kama afya, elimu, usalama na haki hazipo."
Kinyume na hali hii, ameongeza, "janga la coronavirus">COVID-19 limeimarisha kukosekana kwa usawa, na limerudisha nyuma maendeleo na faida ya ujenzi wa amani."
Naye Rais wa Rwanda, Kagame kupitia hotuba yake amesisitiza jinsi ujenzi wa amani "sio biashara ya kiufundi tu bali ni ya kisiasa na ya kibinadamu na lazima izingatie hisia na kumbukumbu ambazo pande mbalimbali huleta kwenye meza."
Kuhusu hali ya Ethiopia, Rais wa mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amesema, "mapigano nchini Ethiopia yanapaswa kuingia katika usitishaji wa mapigano wa kudumu na kushirikishana katika mazungumzo ya kitaifa yanayojumuisha hasa kukubaliana kuhusu nini wanapaswa kufanya pamoja ili kufikia lengo muhimu zaidi la umoja na utofauti.
“Mwisho wa vita vya Biafra huko Nigeria mnamo mwaka 1970, viongozi mbalimbali wa kitaifa walitangaza kwamba wangefuata sera ya hakuna mshindi, hakuna aliyeshindwa. Ninaamini, mwenyekiti, kwamba hii ndiyo mahitaji ya Ethiopia. " Amesema Bwana Mbeki.