Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimu wa baridi ukijongea hali yazidi kuwa mbaya Afghanistan:UNHCR

Wakimbizi wa ndani wakipokea misaada ya kibinadamu mjini Kabul, Afghanistan
© UNHCR/Tony Aseh
Wakimbizi wa ndani wakipokea misaada ya kibinadamu mjini Kabul, Afghanistan

Msimu wa baridi ukijongea hali yazidi kuwa mbaya Afghanistan:UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Mgogoro wa kibinadamu unazidi kuwa mbaya nchini Afghanistan na ufadhili wa fedha unahitajika haraka ili kusaidia watu milioni 20 limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. 

Mwezi mmoja tangu kuzinduliwa ombi la dola milioni 606 lililoongozwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mshikamano na watu wa Afghanistan, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa ni asilimia 35 tu ya fedha ambazo zinahitaji kufadhili shughuli kwa miezi miwili ijayo ndio zimepokelewa. 

Hatua hiyo inafuatia wito kutoka kwa mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alioutoa jana Jumatatu kwa jamii ya kimataifa akiitaka kujitolea kwa ajili ya uchumi unaosambaratika wa Afghanistan na kuzuia kuanguka kwake, ambapo athari zake "sio kwao tu bali ulimwengu wote watalipa gharama kubwa kwa hilo". 

Maoni ya Katibu Mkuu yalikuja kabla ya mkutano wa leo Jumanne wa G20 wa viongozi wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda, ambayo viongozi wao wanazungumzia hali ya Afghanistan, baada ya Taliban kupindua Serikali hapo 15 Agosti mwaka huu. 

Kituo kipya cha misaada

Akizungumza kutoka Kabul, msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema kuwa shirika hilo lilikuwa likijaribu kuanzisha kituo cha misaada nje kidogo ya mpaka wa Afghanistan ili kusambaza misaada kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi wa ndani wa nchi hiyo. 

Bwana Baloch ameelezea kuwa uchumi wa Afghanistan “uko katika hatihati ya kuporomoka", na kwamba anguko hili linapaswa kuepukwa kwa gharama yoyote, haswa ukizingatia kwamba sasa msimu wa baridi ukiingia. 

"Kwa hivyo, rasilimali zinahitajika kufika Afghani zaidi na zaidi, namaanisha, unapozungumza juu ya nusu ya idadi ya watu nchini humo wanategemea misaada ya kibinadamu, sasa ni milioni 20, na idadi hiyo inaongezeka siku hadi siku. Tunahitaji rasilimali hizo haraka iwezekanavyo." Ameongeza Baloch 

Wakimbizi wa ndani wakisimama kwenye mstari kusubiri mgao wa msaada mjini Kabul, Afghanistan
© UNHCR/Tony Aseh
Wakimbizi wa ndani wakisimama kwenye mstari kusubiri mgao wa msaada mjini Kabul, Afghanistan

Usafirishaji wa Ndege

Msemaji wa UNHCR amesema shirika hili limepanga kufanya safari tatu za ndege ili kuongeza msaada kwa Afghanistan katika kipindi kijacho. 

"Mizigo itasafirishwa kwa ndege kwenda Termez, Uzbekistan, na baadaye kusafirishwa kwa malori kupitia eneo la mpaka wa Hairatan hadi Mazar-i-Sharif. Usafirishaji wa ndege utabeba misaada ya kibinadamu inayohitajika haraka. Ndege ya kwanza inatarajiwa kuwasili katikati ya mwezi huu wa Oktoba. ” 

Mtu mmoja kati ya wawili anahitaji msaada

Kwa mujibu wa takwimu za UNHCR mwanzoni mwa mwaka 2021, watu milioni 18 nchini Afghanistan walihitaji msaada wa kibinadamu, nusu ya idadi ya watu wa nchi hiyo.

Maafisa wa misaada wa Umoja wa Mataifa wanasisitiza kwamba "fursa ya kusaidia ni finyu", kwani ni asilimia tano tu ya kaya wana chakula cha kutosha kila siku, na zaidi ya nusu ya watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kupata utapiamlo mkali katika mwaka ujao. 

Ukame mkali na changamoto katika kilimo vimeongeza hatari ya ukosefu wa chakula huku msimu wa baridi ukikaribia, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu wa masuala ya kibinadamu (OCHA).