Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Posta Tanzania yaenda na wakati, yasafirisha damu salama kwa ‘drones’ 

Shirika la Posta Tanzania na huduma za kidijitali
Posta Tanzania
Shirika la Posta Tanzania na huduma za kidijitali

Posta Tanzania yaenda na wakati, yasafirisha damu salama kwa ‘drones’ 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania shirika la posta nchini humo, liko katika mwelekeo sahihi wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ikiwemo lile la 3 la afya njema na ustawi wa jamii kwa kuhakikisha damu salama inapatikana kule inakohitajika. 

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania, Dkt, Aishatu Kijaji
UN Video/Screen shot
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania, Dkt, Aishatu Kijaji

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini humo, Dkt, Aishatu Kijaji amesema hayo wakati ulimwenguni ukiadhimisha siku ya posta kwa kupatia kipaumbele suala la ubunifu kwa maendeleo ya sekta hiyo adhimu. 

“Katika lengo la tatu la afya bora na ustawi wa jamii tunaona shirika letu la posta likishirikiana na taasisi ya Bill Clinton katika kusafirisha damu salama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo hii tunaona kwa mchango huu wa posta ni rahisi sasa damu salama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Tunavyojua damu inahitajika maeneo mengi, pengine una damu salama eneo X na mahitaji ni eneo Y. Kwa hiyo tukitumia ndege zisizo na rubani au Drones ambazo tunaanza kuzitumia katika shirika la Posta kusafirisha damu salama, kwa hiyo tunaona mchango mkubwa na hivyo  katika sekta ya afya tunakwenda kufanikisha lengo hili la afya njema na ustawi wa jamii ambalo ni lengo namba 3 la SDGs.” 

Tunavyojua damu inahitajika maeneo mengi, pengine una damu salama eneo X na mahitaji ni eneo Y. Kwa hiyo tukitumia ndege zisizo na rubani au Drones ambazo tunaanza kuzitumia katika shirika la Posta kusafirisha damu salama, kwa hiyo tunaona mchango mkubwa na hivyo  katika sekta ya afya. Dkt. Aishatu Kijaji- Waziri Tanzania

Dkt. Kijaji akazungumzia ubunifu katika lengo namba 8 la kazi na ukuaji wa uchumi akisema, “tunaona kabisa shirika la Posta limeanzisha programu nyingi za kufanyia shughuli zake kwenye maeneo ya mtandao. Inatengeneza ajira kwa vijana na wanawake wa Tanzania na hawa ni wa kitanzania wakishirikiana na dunia na mataifa mbalimbali, wanatengeneza ajira kupitia kununua biashara na kutengeneza mitandao mbalimbali kuona ni jinsi gani tunashirikiana na dunia na katika ukuaji huo tunatengeneza kazi nyingi na ukuaji wa uchumi kupitia mtanzania mmoja mmoja na taifa letu kwa ujumla.” 

Kwa mujibu wa Waziri Kijaji, ofisi za Posta zimefungua huduma za intanenti ambazo ni bei nafuu na hivyo kuwezesha vijana kujipatia huduma hizo kwa urahisi na kwamba, “mtu anakwambia ukitaka huduma za intaneti ya bei nafuu na salama nenda Posta. Kwa hiyo tumeona mchango wa ofisi za Posta zilizoko Tanzania nzima kwenye wilaya zetu. Tunaona vijana wetu wamejifunza kutoka Posta kwenda kuanzisha vituo vingine vya kutoa huduma za intaneti na ajira tunazitengeneza.” 

Waziri Kijaji akatamatisha kwa kufafanua maudhui ya siku ya posta mwaka huu na utekelezaji wa malengo endelevu akisema “lengo namba 9 na lengo namba 10 la SDGs linaloongelea ubunifu, viwanda na miundombinu katika kuongeza usawa kama tunavyofahamu kauli mbiu ya siku ya posta duniani ni ubunifu kwa Posta endelevu, tunaona shirika letu limeweka vituo mbalimbali vya intaneti katika ofisi za posta nchini kote, na matumizi haya ya teknolojia mpya  yanawezesha watanzania wenye viwanda vidogo vidogo kusafirisha bidhaa zao ziweze kuchakatwa na kupata bidhaa za mwisho na zifike zinakohitajika. Kwa hiyo tunaona tunaona ubunifu huu utasaidia kufanikisha SDGs na kujenga usawa kwa watanzania.  

Huduma za posta mtandao nchini Tanania zimefungua ajira kwa vijana.
Huduma za Posta Tanzania/Screen shot
Huduma za posta mtandao nchini Tanania zimefungua ajira kwa vijana.

Na alipoulizwa ana ujumbe gani kwa wasemao kuwa Posta imepitwa na wakati na inakufa, Waziri Kijaji amesema, “huduma za posta duniani zilianza miaka ya 1800 na muda unakwenda na mambo yanabadilika vivyo hivyo huduma za posta. Tumeona mtu yuko Tanzania anaagiza bidhaa kutoka nchi za nje, kitu ambacho miaka ya 1800 hakikuwezekana. Sasa kutokana na uchumi wa kidijitali na posta ya kidijitali tunaona hilo linawezekana. “ 

Amesema shirika la Posta limekuwa mstari wa mbele likibadilika na wakati na kwamba, ni juzi tu tumezindua Posta Mtandao na wananchi wanaendelea kufurahia na Posta inashiriki katika biashara mtandao.”